Jamhuri yapewa siku 14 kukamilisha mashitaka kwa watumishi wa halmshauri

Baadhi ya washtakiwa wakipanda gari
Muktasari:
Mahakama ya wilaya Kigoma yatoa siku 14 kwa upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili watumishi 11 wa halmashauri mbalimbali nchini.
Kigoma. Mahakama ya Wilaya Kigoma, imetoa siku 14 kwa upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi na michakato yote inayohusiana na shauri linalowakabili watumishi 11 wa halmashauri mbalimbali nchini.
Katika shauri hilo namba 3 la mwaka 2023 washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 11 likiwemo kosa la utakatishaji zaidi ya Sh463.5 milioni.
Washtakiwa hao ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Athumani Msabila, Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dodoma Frednand Filimbi, Salum Juma, Moses Zahuye watumishi kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Watumishi hao wameshindwa kutimiza vigezo vya kupata dhamana.
Wengine waliokidhi masharti ya dhamana ni Joel Shirima, Jema Mbilinyi, Kombe Kabichi, Frank Nguvumali, wote kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Bayaga Ntamasambilo kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Akitoa maelekezo kwa Jamhuri leo Januari 29, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama, Hassan Momba amesema kesi hiyo ina muda mrefu na kila siku inatajwa bila kuendelea hatua nyingine.
Amesema hiyo sio misingi ya jinai hivyo siku 14 zinaweza kuwatosha kujipanga na kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo kuliko kila siku watuhumiwa wanapelekwa mahakamani hapo na kurudi mahabusu.
Upande wa mashtaka kupitia wakili wa Serikali, Antia Julias akisaidiana na Flora Lukas, wamesema wapo katika hatua za mwisho kukamilisha upelelezi huo na kesi hiyo itaanza kusikilizwa mara baada ya kukamilika.
Kwa upande wake wakili wa utetezi, Sadik Aliki ameeleza kusikitishwa kwake na mwenendo wa kesi hiyo akisema ina muda mrefu bila kuonesha matumaini yeyote.
Naye wakili Eliutha Kivyiro amesistiza kama upande wa mashtaka hauna nia ya kuendelea na shauri hilo ni vema waliondoe mahakamani kwa kuwa kinachoendelea kwa sasa ni kama watuhumiwa wameshakutwa na hatia wakati bado kesi hiyo haijasikilizwa.
Shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 7, 2023 na kusomewa mashtaka ambapo washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote ambao walikuwa wakishtakiwa kwa makosa 11.
Makosa hayo 11 ni pamoja na kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kugushi nyaraka, kutakatisha fedha, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh463.5 milioni.