Uamuzi kesi ya watumishi halmashauri wakwama, hati kubadilishwa

Muktasari:
- Mahakama ya Wilaya Kigoma, imeuagiza upande wa Jamhuri kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka kwa kuiandika upya na kuiwasilisha mahakamani Januari 29, 2024 ili kutoa uamuzi ya hoja zilizowasilishwa na mawakili wa utetezi.
Kigoma. Mahakama ya Wilaya Kigoma imeshindwa kutoa uamuzi katika kesi ya watumishi 11 wa halmashauri akiwemo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga Athumani Msabila, ikiutaka upande wa Jamhuri kufanya mabadiliko ya hati ya mashtaka na kuiwasilisha mahakamani hapo Januari29, 2024.
Hatua hiyo imekuja baada ya Januari 4, 2024 mawakili wa upande wa utetezi kuwasilisha rasmi hoja ya kuwatoa wateja wao kwenye kosa la utakatishaji fedha washtakiwa namba 2 na 3 ambao ni Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Tamisemi Dodoma.
Mawakili hao wamedai kuwa watuhumiwa hao hawakuhusika na kosa namba 10 la utakatishaji fedha.
Akitoa maelekezo hayo leo Januari 26, 2024, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya hiyo, Hassan Momba ameutaka upande wa mashtaka ufanye mabadiliko kwenye hati ya mashtaka ili aweze kutoa uamuzi wa nini kifanyike kwa watuhumiwa hao.
Katika shauri hilo namba 3 la mwaka 2023, washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 11 ikiwemo kosa la utakatishaji fedha Sh463.5 milioni, na kesi hiyo ilifika leo kwa ajili ya kutolewa uamuzi kuhusu na hoja zilizokuwa zimewasilishwa na mawakili wa utetezi.
Washtakiwa watano wametimiza masharti ya dhamana na wako nje ni pamoja na Joel Shirima, mshtakiwa namba 7, Jema Mbilinyi mshtakiwa namba 8, Kombe Kabichi mshtakiwa namba 9 na Frank Nguvumali mshtakiwa namba 10.
Washitakiwa hao wanatoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji na Bayaga Ntamasambilo mshtakiwa namba 11 kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.
Washtakiwa sita wanaoendelea kusota mahabusu ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Igunga, Athumani Msabila, Aidan Mponzi na Tumsifu Kachira kutoka Ofisi ya Rais Tamisemi Dodoma.
Wengine ni Frednand Filimbi, Salum Juma, Moses Zahuye kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Shauri hilo lilifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Novemba 7, 2023 na kusomewa mashtaka dhidi yao na hawakutakiwa kujibu chochote.
Makosa hayo 11 ni pamoja na kula njama kwa nia ya kutenda kosa, kugushi nyaraka, kutakatisha fedha, matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia Serikali hasara ya Sh463.5 milioni.