Jatu yaingia soko la hisa, mtaji wa soko waongezeka

Monday November 23 2020
dse pic

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE Moremi Marwa

By Ephrahim Bahemu

Dar es Salaam. Mtaji wa soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) umeongezeka na kufika Sh15 Trilioni baada ya kuorodhesha kwa kampuni mpya ya kilimo iitwayo Jatu Plc ambayo imeweka soko hisa zake zaidi ya milioni mbili zenye thamani ya zaidi ya Sh1 bilioni.

Jatu Plc imeorodhesha leo Novemba 23, 2020 kwa mara ya kwanza ambapo hisa zilizolipwa 2,164,349 zimeorodhesha zikiwa na thamani ya Sh1.08 bilioni.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa DSE Moremi Marwa amesema kuorodheshwa kwa Jatu ni kielelezo cha namna ambavyo soko hilo linaweza kutumiwa na makampuni hasa madago na ya kati kuongeza wigo wa wawekezaji na kupata mitaji ili kukuza uwekezaji.

Ofisa mtendaji mkuu wa Jatu Plc Peter Isare amesema kuorodheshwa kwa kampuni hiyo kunafungua milango mingi ya fursa kufanya zaidi ya wanachokifanya sasa.

"Tutaibua fursa nyingi za kiuchumi kwa wengi hususani vijana.Uzuri tunafanya uwekezaji wa kilimo na bidhaa yetu ni chakula, hakuna mtu asiyekula hivyo tuna matumaini ya kupata faida kwa manufaa ya wanahisa wetu," amesema Isare.

Advertisement