Jengo la mapadri lateketea kwa moto Dar

Muktasari:
Moto wateketeza jengo la makazi ya mapadri katika Seminari ya Segerea. Hata hivyo, hakuna aliyepoteza maisha au kujeruhiwa katika tukio hilo. Jumla ya vyumba 14 vya mapari vimeungua pamoja na mali zilizokuwa ndani yake.
Sehemu ya jengo la makazi ya mapadri wa Seminari ya Mtakatifu Karol Lwanga ya Segerea limeteketea kwa moto jana usiku Januari 16, 2019.
Jengo hilo la ghorofa moja lilishika moto katika sehemu ya juu kuanzia saa 4:50 usiku ambapo shughuli za uokoaji zilianza lakini hawakufanikiwa kuokoa vitu katika jengo hilo.
Akizungumza na gazeti hili leo Januari 17, 2019, mkuu wa shule hiyo (rekta), Padri Tobias Ndabhatinya amesema moto huo ulianza wakati mapadre wakiwa kwenye chumba cha majadiliano na wenzao wawili walikuwa wamelala.
Amesema ghafla wakasikia sauti ya cheche lakin wakapuuzia baada ya muda wakasikia harufu ya moshi. Walipotoka waliona chuma kimoja kimeshika moto huku ukiwa umesambaa sehemu kubwa ya chumba hicho ambacho hakikuwa na mtu.
"Baada ya kuona moto tulianza jitihada za kuwaokoa wenzetu wawili waliokuwa ndani. Tulifanikiwa kuwashusha kwa kamba kwa sababu wakati huo moto ulikuwa umesambaa sehemu kubwa."
"Tunashukuru Mungu hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha au kuumia katika tukio hili lakini vitu vyote vya mapadri wetu kama vile nguo, kompyuta na vitabu vimeteketea kwa moto," amesema Padri Ndabhatinya.
Amesema jumla ya vyumba 14 vya juu ambavyo vilikuwa vinakaliwa na mapadri vimeungua lakini vyumba vya chini viko salama hasa baada ya moto huo kuzimwa baada ya kupungua nguvu.
Shuhuda wa tukio hilo, George Liberatus amesema moto ulikuwa mkubwa katika sehemu ya paa, jambo lililowatisha na kusitisha uokoaji mpaka moto ulipopungua, tayari vitu vyote vikiwa vimeteketea.
Seminari hiyo imetembelewa na maaskofu kutoka Baraza la Maaskofu (Tec) ambao wametoa pole na kuahidi kuwasaidia mapadri walionusurika ili wapate malazi na mavazi wakati hatua nyingine zikichukuliwa.
Kiongozi wa ujumbe huo ambaye pia ni askofu wa jimbo la Geita, Flavian Kasala amesema tukio hilo limewagusa maaskofu na kwamba watajadili jinsi ya kuwasaidia mapadri hao wakati mipango mingine ikiendelea.
"Kunahitajika utulivu na kupanga kipi kianze kushughulikiwa kwanza halafu mipango mingine ya muda mrefu ifuate. Tutakuwa na kikao cha dharura kujadili jinsi ya kuwasaidia mapadri ambao wameunguliwa mali zao," amesema Askofu Kasala.