Jeshi la Zimamoto latangaza mabadiliko tozo za ukaguzi

Thursday August 11 2022
moto pic

Msemaji wa Jeshi la zimamoto na Uokoaji, Puyo Nzalayamaisi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

By Mainda Mhando

Dodoma. Jeshi la zimamoto na uokoaji nchini Tanzania limeongeza maeneo ya kukusanya tozo za ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto katika maeneo ya vituo vya usafirishaji, karakana na sehemu za kufua nguo (dry cleaner).

 Awali maeneo hayo hayakuwa kwenye mpango wa keshi hilo linalokusanya tozo katika maeneo zaidi ya 200.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Agosti 11, 2022 na msemaji wa jeshi hilo, Puyo Nzalayamaisi wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Puyo amesema, licha ya kuongeza maeneo hayo jeshi hilo limeondoa tozo za ukaguzi wa usalama dhidi ya majanga ya moto kwenye transfoma, mashamba ya mkonge, kahawa na chai.

Aidha, jeshi hilo limefanya mabadiliko ya gharama za tozo kwenye maeneo mengi yakiwemo maduka, shule, viwanda, makazi, Ofisi, nyumba na tozo za usomaji ramani wa majengo.


Advertisement

“Kwa mfano sehemu kama maduka awali walikuwa wanalipa Sh 40,000 lakini sasa hivi watalipa Sh 20,000 kwa maduka ya rejareja na Sh30,000 kwa maduka ya jumla” amesema Puyo.

Pia amesema awali sehemu za saluni walikuwa wanalipa Sh40,000 lakini sasa watalipa Sh20,000 na wachimbaji wadogo migodini waliokuwa wanalipa zaidi ya Sh600,000 watalipa Sh100,000 kwa skweamita 0 hadi 200 na Sh200,000 kwa skweamita 2001 hadi 4000.

Katika mabadiliko mengine Jeshi hilo limeondoa utaratibu wa Jeshi kuwafuata wananchi kwaajili ya ukaguzi badala yake wananchi watawajibika kutuma maombi ya ukaguzi kwenye ofisi za zimamoto zilizopo kwenye mikoa yao.

“Kwa mujibu wa kanuni hii sasa mteja ana wajibu wa kufika kwenye Ofisi zetu zilizopo kwenye Mikoa yao ili wawekewe mpango kazi wa kukaguliwa huku tukiwa kwenye maboresho ya mifumo ili wateja wetu baadae waweze kuomba kupitia mtandao (Personal online application),” amesema

Advertisement