Jitihada kuuzima moto mlima Kilimanjaro zaendelea

Muktasari:
- Askari zaidi 300 wamepelekwa katika mlima Kilimanjaro kuudhibiti moto uliozuka jana Ijumaa usiku katika eneo la Karanga Camp lililopo mita 3963 kutoka usawa wa bahari.
Moshi. Askari zaidi 300 wamepelekwa katika mlima Kilimanjaro kuudhibiti moto uliozuka jana Ijumaa usiku katika eneo la Karanga Camp lililopo mita 3963 kutoka usawa wa bahari.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema mpaka sasa moto huo haujasababisha madhara yoyote katika shughuli za utalii na kwamba jitihada za kuudhibiti zinaendelea mpaka sasa.
"Jana majira ya saa mbili na tatu usiku kulitokea moto mkubwa katika mlima wetu wa Kilimanjaro katika upande wa Karanga na moto ulikuwa mkubwa sana kutokana na upepo mwingi unaokuwepo jioni.
"Mimi pamoja na kamati ya usalama baada ya kupata taarifa hizi tulianza kushughulika mara moja kuhakikisha moto hausambai kwenye maeneo mengi ya mlima na tuliichukua tahadhari kubwa kwasababu ya watalii ambao wapo mlimani,"
Amesema mpaka sasa hakuna mtalii yoyote aliyepata madhara "Mimi nimefika mpaka geti la Mweka wageni wanashuka na wengine wanapanda kupitia geti la Marangu, jitihada ambazo tumezichukua kama mkoa ni kwamba tumeongeza nguvu kwenye eneo la tukio na tayari tumepeleka askari wetu zaidi ya 300 kusaidia kuudhibiti moto ili usiendelee kusambaa.
"Tunachokifanya sasa tunazuia moto usiingie kwenye msitu mkubwa na tayari taratibu zote zinaendelea kuudhibiti moto huu," amesema mkuu huyo wa mkoa.
Babu amesema watafanya uchunguzi kujua ni kitu gani kinachosababisha moto huo kutokea katika mlima huo.
Akizungumza Kamishina wa Uhifadhi Kanda ya Kaskazini, Betrita James amesema baada ya kupata taarifa za kuonekana kwa moto huo, menejimenti ya Kinapa ilianza kukusanya nguvu kazi na vifaa, pamoja na timu ya watu 350 kutoka Chuo cha Taaluma ya Polisi Moshi, Chuo cha Mweka, askari kutoka kikosi cha Zima Moto, Jeshi la Akiba na wadau wengine kuuzima moto huo.
"Taarifa za moto tulizipata jana usiku kwamba moto ulizuka eneo la karanga na hadi kufikia asubuhi umeendelea na umeendelea eneo la Baranko na Millenia na kutokana na upepo mkali uliokuwepo usiku unaelekea eneo la jangwa na barako, tayari watu 350 wapo eneo la tukio wakiendelea na jitihada za kuudhibiti"
Akizungumza kaimu kamanda wa jeshi la zima moto na uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro Abraham Ntezidyo amesema jitihada za kuuzima moto huo zinaendelea na kwamba baada ya kutoka eneo la tukio kufanya tathimini, wataangalia uwezekano wa kutafuta ndege kwa ajili ya kuzima moto huo.
"Kutokana na moto kusambaa, kuna watu wapo eneo kuelekea geti la mweka kwa sababu moto unaelekea kushuka chini, lakini pia unaelekea upande wa kilema hivyo kuna timu ya watu na askari wapo upande huo kuudhibiti"