JK aeleza alivyopambana na udumavu enzi za uongozi wake

Rais mstaafu Jakaya Kikwete akikabidhi vidonge milioni 22 vya matone vya vitamini A kwa Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel jijini Dar es Salaam leo Machi 13 2024. Kulia ni mwakilishi wa Balozi wa Canada, Helen Fytche.  Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

Takwimu zinaonyesha watoto wenye udumavu Tanzania ni asilimia 30

Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesimulia namna alivyopambana na changamoto ya udumavu alipoingia madarakani mwaka 2005, inayosababishwa na lishe duni.

Kikwete  ambaye ni mjumbe wa bodi ya kimataifa ya lishe (Nutrition International) iliyopo nchini Canada amesema aliikuta nchi ikiwa na asilimia 42 ya watoto wenye udumavu na mpaka anaondoka madarakani aliacha udumavu ukiwa asilimia 34.

Kikwete amesema hayo leo Jumatano Machi 13, 2024 wakati wa makabidhiano rasmi ya vidonge  milioni 22 vya matone ya vitamini A kati ya Shirika la Nutrition International na Wizara ya Afya.

"Tuna tatizo kubwa la udumavu, asilimia 30 iliyopo sasa ni jitihada zilizofanyika kwa awamu. Nilipoingia madarakani nilikuta asilimia 42 ya watoto wana udumavu, tulipoondoka mwaka 2015 ilikuwa asilimia 34 na sasa imefika 30. Bado tupo nyuma sana asilimia 30 ni tatizo hii ina maana asilimia 30 ya watoto nchini kimo chao hakifanani na umri wao,” amesema Kikwete.

“Kuna ukondefu, uzito wao haufanani na umri wao lakini tuna tatizo kubwa la upungufu wa damu anaemia kwa watoto ni asilimia 59."

Amesema Shirika la Nutrition International lililopo Canada linatoa vidonge milioni 500 duniani kote kila mwaka na Tanzania hupata vidonge milioni 22.

Akizungumza Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amesema nchi inapopambana na udumavu pia inaendelea kuhamasisha watu wale lishe na siyo shibe.

"Tunapopambana na udumavu kwa watoto sasa hivi, watu wazima wamekula na kushiba kiasi kwamba wamenenepa sana.

"Watu wanachanganya lishe na shibe, wengi sasa hivi wanashiba kiasi kwamba anakua mnene lakini anakosa vitamini muhimu mwilini," amesema.

Mwakilishi wa Balozi wa Canada, Helen Fytche amesema mwaka 2020 zaidi ya watoto milioni 100 duniani  walikosa vitamini A kutokana na Uviko-19 na ili kusaidia nchi 16 mwaka 2021 walitoa dozi 124 zilizosaidia kuzuia vifo 32 milioni.

Amesema uongezaji wa vitamini A huimarisha mfumo wa kinga kwa watoto chini ya miaka mitano na kuepusha vifo vinavyoweza kuepukika na kinga magonjwa ya kawaida ikiwamo surua na kuharisha.

Amesema wanaiunga mkono Serikali katika kutekeleza sera na miongozo ya kimataifa na kuwajengea uwezo wahudumu wa afya ngazi ya jamii, kwa kuwa kwa sasa chanjo ya kitaifa imezidi asilimia 98 ijapokuwa kwa mwaka 2020 ilishuka kutokana na janja la Uviko-19.

Mkurungenzi wa Kinga Wizara ya Afya Dk Tumaini Haonga amesema Tanzania ilianza kutoa huduma ya matone ya vitamini A miaka 37 iliyopita.

Amesema  wakati wote wamehakikisha huduma inatolewa kwa watoto kuwafanya wawe na kinga imara ya mwili na kuimarisha uwezo wa macho kuona.

Amesema pamoja na matone hayo wamekuwa wakitoa elimu kwa kinamama kuwaongezea vyakula mbalimbali kama mbogamboga, mafuta ya mawese, nyama kama maini na karoti ili kuimarisha vitamini hiyo.

"Takwimu zinaonyesha asilimia 44 ya watoto chini ya miaka mitano wana changamoto ya ukosefu wa vitamini A kutoka kwenye milo, ndiyo maana tunatoa kwa watoto wa miezi sita  mpaka 56 yaani miaka mitano.

"Kila baada ya miezi sita tunatoa Juni na Desemba siku zote 31 za mwezi na tunawafikia watoto milioni 10, mwaka huu tunalenga kuwapata milioni 11 kwa dozi zote mbili," amesema.