Joel alivyoona fursa kilimo parachichi

Joel alivyoona fursa kilimo parachichi

Muktasari:

  • Unadhani kila kijana anatamani kuwa mmachinga wa kuchuuza bidhaa barabarani au masokoni?




Unadhani kila kijana anatamani kuwa mmachinga wa kuchuuza bidhaa barabarani au masokoni?

Wakati mtazamo wa vijana wengi ukiwa ni huo wa kuchuuza bidhaa, Joel Baraza ana mtazamo mwingine.

Anaingia katika orodha ya vijana wachache walioamua kujishughulisha na biashara katika sekta ya kilimo.

Joel ni mkulima aliyeamua kutafuta misha kupitia biashara ya kuuza miche ya mazao mbalimbali, hasa parachichi. Katika mahojiano haya, Joel, anayeishi Mbinga mkoani Ruvuma anaeleza safari ya kilimo anayosema kuwa aliianza mwaka 2017.


Swali: Umeanza lini harakati za kilimo na nini kilikusukuma kuingia kwenye kilimo?

Jina langu halisi ni Joel Baraza Daud. Kwa jina la mradi najulikana kama Joe Parachichi. Makazi yangu yapo katika Mji wa Mbinga na ndipo ninapoendesha mradi wangu wa kitalu cha miche ya miparachichi.

Harakati hizi za kilimo nilianza mwaka 2017. Nilianza kupanda na kuzalisha miche ya matunda aina mbalimbali kama parachichi, maembe, papai, machungwa, tofaa, matunda na migomba. Nilianzia na ekari tatu huko Songea.

Kilichonisukuma kuingia kwenye kilimo ni dhamira yangu ya moyoni juu ya kuleta mabadiliko ya kilimo hususani kupanua wigo, kutoka kilimo kilichozoeleka cha nafaka kwenda kilimo cha matunda aina mbalimbali na mbogamboga.


Swali: Unadhani kilimo ni mahala sahihi kwako?

Jibu: Kilimo ni mahala sahihi kwangu. Na pia ni mahala sahihi kwa watu wengi, pamoja na wewe. Kilimo kinaajiri takribani asilimia 75 ya Watanzania na kinachangia karibia asilimia 25 ya uchumi wa Tanzania.

Kilimo kinatupa chakula na mazao mengine ya msingi katika maisha ya binadamu kama vile pamba kwa ajili ya mavazi, ngozi tunayotumia kwa mahitaji mengi katika maisha yetu na mengine mengi.


Swali: Unajivunia mafanikio gani tangu uanze kilimo?

Jibu: Kwa sasa hivi jitihada zangu nimezielekeza kwenye kilimo cha matunda, hususan parachichi. Pamoja na kuwa kilimo hiki kimekuwa dhamira yangu ya moyoni, kilimo cha matunda kinalipa.

Katika kilimo hiki, mimi nazalisha miche ya kisasa ya matunda ya aina mbalimbali, ikiwamo parachichi, maembe, machungwa, mapera, malimao, mipapai na kadhalika.

Kiasi kikubwa cha mafanikio yangu nayahesabu kwa idadi ya miche ya matunda na mboga ambayo nimewahi kuzalisha na kuitoa kwa wakulima kwenda kuipanda mashambani mwao.

Hadi sasa nimeshatoa zaidi ya miche 20,000 ya matunda mbali mbali. Katika hiyo, miche 8,000 ni ya miparachichi, 4,000 miembe, 3,000 michungwa, 2,000 mipera, 2,000 mipapai na mingine kwa matunda mengineyo, yakiwamo passion 500 na stafeli 500.

Wateja hao wapo katika maeneo mbalimbali, yakiwa ni pamoja na Mbinga, Njombe, Mbeya, Iringa, Morogoro na Arusha.

Vilevile, mafanikio yangu makubwa yapo katika kutoa elimu kwa watu mbalimbali juu ya kilimo hiki, ikiwamo waumini katika makanisa na wanafunzi katika shule za msingi na sekondari.

Kwa yote ambayo nimefanya, hili la elimu kwa watoto ni la mafanikio makubwa zaidi, kwani linajenga utamaduni na uelewa mkubwa kwa watoto ambao watakua nao hata katika maisha yao ya baadaye.


Swali: Kuna changamoto unazokabiliana nazo?

Jibu: Changamoto katika kilimo ni nyingi. Kubwa katika huu mradi wangu ni wananchi kuwa na kilimo cha jadi cha kujikimu zaidi kuliko kilimo cha kisasa, kibiashara. Hii inasababisha upandaji wa matunda na mboga kuwa chini na hivyo kiasi cha miche inayochukuliwa kuwa kidogo.

Pia, wananchi wengi wa Mbinga ni wakulima wa kahawa. Hilo ni zao la biashara ambalo limeshika hatamu kiasi kwamba uelewa na imani kuwa matunda na mboga vinaweza kuwa mazao mbadala uko chini. Inachukua muda na nguvu kubwa kueneza uelewa huu.

Changamoto nyingine ni kukosekana kwa masoko ya uhakika na bei rafiki kwa mkulima. Hii inawasumbua wateja wangu, na inasababisha nami pia kupungukiwa mauzo katika kitalu changu.

Suala jingine napenda niliongelee kwa sasa ni upatikanaji mdogo na bei kubwa za pembejeo na za zana bora na za kisasa za kilimo. Hii inasababisha wakulima kuwa na mashamba madogo madogo kiasi kwamba idadi ya miche inayochukuliwa inakuwa michache.

Hata hivyo, wito wangu kwa Watanzania tuingie katika kilimo cha kisasa na cha kibiashara kwa mazao tofauti tukizingatia mbinu za kilimo zenye tija zaidi.

Tutumie utaalamu na mbinu za kisasa ili kilimo chetu kiwe na tija zaidi. Tujenge, tuendeleze na kuyatumia masoko ya ndani kwa kiwango kikubwa tukiongezea thamani mazao yetu ili kuimarisha uchumi wetu zaidi. Biashara imara katika soko la ndani itatupa nguvu ya kwenda katika soko la kimataifa kwa ushindani na uwezo mkubwa zaidi wa majadiliano ya kibiashara.


Swali: Una matarajio gani katika siku za baadaye?

Jibu: Kadiri tunavyoendelea kuelimishana, kupeana mbinu mbalimbali za kilimo na kuhamasishana kupanua wigo wa uchumi wa kilimo kwa kuongeza tija na uwingi wa mazao, naona uchumi mkubwa zaidi wa kilimo.

Natarajia kuona jamii yenye afya bora na uchumi imara zaidi ukichagizwa na mazao mbadala kwa biashara yaliyoongezewa thamani na kuuzwa katika bidhaa zake za thamani kubwa zaidi.


Swali: Unadhani kilimo cha parachichi kinaweza kuwatoa wakulima kiuchumi?

Jibu: Kwa hakika kilimo cha parachichi kina nafasi kubwa ya kuwanyanyua wananchi. Parachichi ni tunda lenye fursa za kipekee kiafya na limepata umaarufu mkubwa dunia nzima.

Pamoja tuna hili kuliwa kwa ajili ya manufaa yake kiafya, mwilini, lina sifa ya kuweza kukamuliwa mafuta ya kupikia ambayo hayana madhara mwilini. Mafuta hayo yanauzwa kwa bei nzuri na yenye faida kubwa kwa mkulima.

Parachichi pia linaweza likatengenezwa na kutoa vipodozi kama vile mafuta ya kujipaka ambayo ni mazuri sana kwa ngozi. Pamoja na hayo yote, tunda hili linaweza kutengenezwa siagi ya kupakwa kwa mkate, ambayo ni salama zaidi kuliko siagi nyingi zinazotumika ulimwenguni.

Tunafahamu pia kuwa kuku wakila tunda hili wanapata manufaa mengi, ikiwa ni pamoja kinga dhidi ya maradhi na magonjwa mbalimbali na pia wanaongeza utagaji wa mayai.

Mawasiliano: 0763 00 00 41 au 0654 51 12 99.