Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

John Heche: Tukiingia madarakani, Chadema tutaleta sera, fikra mpya

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, John Heche akihutubia moja ya mikutano ya hadhara ya chama hicho.

Muktasari:

Chadema imezindua kampeni ya operesheni +255 Katiba Mpya Okoa Bandari Zetu katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Bukoba Julai 28, 2023. Baada ya uzinduzi huo, viongozi wa chama hicho wamegwanyika katika makundi mawili, moja likiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe na likingine la Makamu Mwenyekiti wake, Tundu Lissu wakifanya mikutano ya hadhara katika wilaya tofauti mkoani Kagera.

Mwanza. MJumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadea), John Heche amewaomba Watanzania bila kujali tofauti zao kiitikadi kukipa chama hicho fursa ya kuongoza Serikali kupitia sanduku la kura ili kilete sera na fikra mpya katika uongozi, ujenzi wa uchumi na maendeleo ya Taifa.

Akihutubia mkutano wa hadhara eneo la Kibindi Wilaya ya Biharamulo leo Julai 30, 2023, Heche amesema Tanzania haistahili kuendelea kuwa maskini miaka zaidi ya 60 baada ya Uhuru kwa sababu imejaaliwa kila aina ya utajiri kuanzia madini, mbuga na hifadhi za wanyama, bahari, maziwa, mito inayotiririsha maji kipindi chote cha mwaka, ardhi yenye rutuba, misitu na eneo nzuri la Kijiografia.

“Tuna ardhi nzuri na kubwa yenye rutuma, hali nzuri ya hewa, maziwa na mito inayotirisha maji kipindi chote cha mwaka. Tuna madini ya Tanzanite yanayopatikana Tanzania pekee dunia, tunayo dhahabu, nickel, almasi, gesi, mbuga za wanyama na mlima Kilimanjaro. Hatustahili kuwa maskini.

Mbunge huyo wa zamani wa Tarime Vijijini amedai kinachokosekana kuwa ni sera na uongozi bora, hivyo akawaomba Watanzania kukipumzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) akidai kimechoka na hakina sera wala fikra mpya za kuongoza Taifa.

Akizungumzia bei ya mazao ya kilimo, mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) ameahidi kuwa chama hicho kikuu cha upinzani kikiingia madarakani kitafuta ushuru na tozo zote zinazopunguza mapato ya wakulima.

Alisema Tanzania inastahili kupata bei nzuri ya mazao yake ikiwemo kahawa, lakini hali ni tofauti kulinganisha na mataifa jirani inayouza mazao yake katika soko lile lile la dunia inakouza Tanzania.

‘’Kwanini Uganda inanunua kahawa kwa bei kubwa kuliko Tanzania wakati sote tunategemea soko moja la Kimataifa? Ni dhahiri kuwa wenzetu wameondoa kodi na tozo kwenye mazao ya kilimo. Chadema tukiingia madarakani tutafuta kodi na ushuru zinazopunguza mapato ya wakulima,’’ amesema Heche

Ahadi ya maisha bora kwa Watanzania pia imetolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alipohutubia mikutano tofauti ya hadhara wilayani Kyerwa.

Huku akishangiliwa na umati uliokuwa ukimsikiliza wakati wa mkutano uliofanyika eneo la Nkwenda Wilaya ya Kyerwa, Mbowe amesema huduma bora za maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara, hasa vijijini ni miongoni mwa vipaumbele vya Chadema itakapoingia madarakani.

Kiongozi huyo mkuu wa upinzani ametaja suala la wakazi wa maeneo ya mipakani kukosa namba na vitambulisho vya Taifa kuwa kero nyingine itakayoshughulikiwa katika siku za mwanzo za uongozi wa Chadema ikishinda uchaguzi na kuongoza Serikali.

Huku akiahidi kuwasilisha kero hiyo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Mbowe ameonyesha kusikitishwa kupokea kilio cha wakazi wa Mkoa wa Kagera na maeneo ya mpakani kuhusu namba na vitambulisho vya NIDA

Mbunge huyo wa zamani wa Hai mkoani Kilimanjaro amegusia pia suala la umasikini wa kipato kuwa eneo lingine litakalopewa kipaumbele Chadema ikiingia madarakani.

‘’Umaskini umetamalaki miongoni mwa Watanzania kote nchini; ukienda Kilimanjaro, Arusha, Mtwara, Tanga, Mara, Ruvuma, Dodoma na kila eneo, kilio ni umasikini wa kipato. Chadema tukiunda na kuongoza Serikali tutaleta sera na fikra mpya kuwezesha wananchi kutumia fursa na rasilima zilizopo kujimarisha kiuchumi,’’ amesema Mbowe