Joto la uchaguzi 2025 lapanda Mbeya Mjini

Dar es Salaam. Joto la Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 limeanza kufukuta baada ya wabunge, akiwemo Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kuanza kuomba mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi.

Dk Tulia amewasilisha maombi hayo serikalini kuomba jimbo la Mbeya Mjini aliloanza kuliongoza mwaka 2020 akimpokea Joseph Mbilinyi, maarufu Sugu wa Chadema na kuibua mjadala mkali mitandaoni.

Taarifa za kuwepo maombi hayo yanayofanyiwa kazi zilielezwa bungeni jana katika kipindi cha maswali na majibu.

Mjadala ulioibuka kuhusu maombi hayo unatokana na ushindani uliopo katika jimbo hilo ambalo Sugu aliipokonya CCM mwaka 2010 na kuliongoza kwa vipindi viwili kabla ya Dk Tulia aliyejitosa mwaka 2020 kulirejesha kwenye himaya ya chama tawala.

Sugu aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza wa hiphop kushinda ubunge mwaka 2010 akipata kura 46,411 na kumbwaga mpinzani wake, Benson Mpesya wa CCM alipata kura 24,327.

Katika uchaguzi wa mwaka 2015, Sugu alitetea nafasi hiyo na kuibuka kidedea akiwa na kura 108,566 zilizomwezesha kuwa mbunge aliyechaguliwa kwa kura nyingi kuliko wote katika majimbo 264.

Mwaka 2020, Sugu alijikuta akilikosa jimbo hilo baada ya Dk Tulia kulichukua akipata kura 75,225 dhidi Sugu aliyepata kura 37,591.

Tangu wakati huo, wamekuwa kwenye mchuano mkali wa kisiasa, huku Sugu kwa nyakati tofauti amekuwa akisikika akisema, wana-Mbeya bado wanamhitaji na wakati wa uchaguzi ukifika atatii maagizo yao na tayari amekuwa akifanya mikutano jimboni.

Wakati mchuano wa jimbo hilo na mengine ukiendelea, hasa baada ya mikutano ya hadhara kuruhusiwa, jana Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga alilieleza Bunge kuwa Serikali imekwishapokea maombi ya Dk Tulia kuhusu mgawanyo ya jimbo hilo.

Nderiananga alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Sophia Mwakagenda.

Mwakagenda alisema Jimbo la Mbeya Mjini ni kubwa sana, lina kata zaidi ya 36 na lina wapigakura wengi. “Je, ni lini Serikali itapanga kuligawa jimbo hilo ili liweze kuweka urahisi wa mbunge husika, waweze kugawana namna ya kulitumikia jimbo hilo?”

Kufuatia swali hilo, Naibu Waziri Ummy akijibu, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaendelea na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 na muda utakapofika, wataangalia vigezo na masharti ili kuona kama jimbo hilo linafaa kugawanywa.

“Serikali tunatambua, nikuhakikikishie Mbunge wa Mbeya Mjini ambaye ni Spika wetu Tulia, ameshawasilisha suala hili na lipo mezani, kwa hiyo muda utakapofika NEC italitazama pia jimbo la Mbeya Mjini.”

Hata hivyo, Mwananchi lilipomtafuta Spika Dk Tulia likitaka kujua lini alituma maombi hayo, simu yake iliita bila kupokewa.

Mapema katika swali la msingi, Mbunge wa Kilindi (CCM), Omari Kigua naye aliyetaka kufahamu ni lini Serikali italigawa jimbo hilo lililopo Mkoa wa Tanga.

Akijibu swali hilo, Nderiananga alisema NEC ipo katika maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, hivyo kwa kuzingatia taratibu na vigezo na muda utakapofika itatoa tangazo rasmi kwa wadau wote wa uchaguzi juu ya kuanza kwa mchakato huo ili wadau wawasilishe maoni na maombi yao.

Suala hilo la mgawanyo wa majimbo halikuishia hapo, pia wabunge wengine waliouliza maswali ya nyongeza walitaka majimbo yao yagawanywe kutokana na ukubwa ni maeneo, akiwemo Emmanuel Mwakasaka (Tabora Mjini) na Boniphace Butondo (Kishapu), wote kutoka CCM.

Akijibu maswali hayo, naibu waziri aliwatoa hofu wabunge hao kuwa suala hilo litafanyiwa kazi na kuwa maeneo hayo yako mengi.

“Tutayafanyia kazi wabunge, karibuni na wadau wa uchaguzi wengine tutoe maoni tutafanya vizuri kwenye eneo hilo,” alisema Nderiananga.

Maandalizi ya uchaguzi huo yaligusiwa pia na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Aprili 5, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/24 aliposema pamoja na shughuli nyingine, Serikali italifanyia maboresho Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Pia, kuboresha mifumo ya menejimenti ya uchaguzi, kuendelea na mchakato wa marekebisho ya sheria za uchaguzi, kuandaa kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani na kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi.


Mjadala wakolea

Baada ya Taarifa za majibu ya Nderiananga kusambaa, mjadala ulihamia mtandaoni, hususan maombi ya Spika Tulia ya kugawanywa jimbo la Mbeya Mjini, akitajwa anataka kumkimbia mshindani wake kisiasa, Sugu.

@Humphrey kweka6 akichangia habari hii kwenye ukurasa wa Instagram wa gazeti hili alisema, “ni bora hilo jimbo ligawanywe tu, maana vita vya Sugu na Tulia vitakuwa vikubwa mno.

“Sugu tunapenda awe bungeni na Tulia tunapenda awe bungeni, sasa kama vigezo vinakidhi kwa nini lisigawanywe tu.”

Hata hivyo, @josephatheniel alisema, “kuna haja ya kupunguza idadi ya majimbo na idadi ya watu kwa mjini (majimbo) yawe na idadi kama ya Mbeya Mjini. Yote yenye watu pungufu yaunganishwe. Wabunge wasiogope kupoteza majimbo.”

Mwingine ni @Issa3jr4 aliyesema, “Tulia amechungulia 2025” huku @manengokennedy akiandika, “shughuli imeanza, Jongwe ni noma.”

Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini (Chadema) ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Godbless Lema alisema jimbo hilo hata likigawanywa watamfuata Dk Tulia hukohuko anapogombea.

Hata hivyo, Sugu alipotafutwa kuhusu suala hilo alisema asingependa kuzungumza suala hilo labda wakati mwingine, lakini Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwasote ‘China’ alisema maombi ya kuligawa jimbo hilo ni jambo jema lenye nia ya kuleta maendeleo, lakini hata likigawanywa wataweka wagombea kwenye majimbo yote.


Mitazamo ya wasomi

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Dk Richard Mbunda alisema haoni kama kuna mantiki kugawa majimbo ya uchaguzi kwa sababu nchi zenye idadi kubwa ya watu kama India, China, Bangaladesh zingekuwa zinagawa majimbo kila uchao.

“Tunatakiwa tuanze kujizuia kuingia kwenye mtego wa kugawana hayo majimbo ili kupeleka wawakilishi wengi bungeni kwa sababu mwisho wa siku tutakuwa na Bunge kubwa lenye watu wengi. Wanatumia gharama kubwa kuendesha Bunge, badala ya pesa kupeleka kwenye miradi ya maendeleo inayowagusa moja kwa moja wananchi,” alisema.

Wakili Rainery Songea alisema zipo sababu mbili za kutaka mgawanyo wa majimbo, ikiwemo ukubwa wa jimbo usioendana na uwezo wa mbunge kulisimamia na kulihudumia na ajenda ya kisiasa ambayo upepo wake huangaliwa kwa kupima nguvu ya upinzani; labda kwa sasa Chadema wana nguvu hapa, tukisema tugombanie wote kuna uwezekano nikapoteza. Sasa hii kama una ushawishi unaweza kutengeneza mazingira ya kuligawanya,” alisema.

Hata hivyo, alikubaliana na wabunge hao kuwa jimbo la Mbeya Mjini ni kubwa na kwamba suala la msingi ni kuwa na majimbo ambayo wananchi wanaweza kuhudumiwa kwa wakati muafaka.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie alisema kama majimbo yanayoombwa kugawanywa yamekidhi vigezo basi ifanyike hivyo na hakuna haja ya kuhofia gharama kwa sababu demokrasia ni gharama.