Spika Tulia ataka ‘mahasimu’ wake kujitathmini

Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson

Muktasari:

  • Spika wa Bunge, Tulia Acksoni azungumzia mgawanyo wa jimbo lakae la Mbeya Mjini, awataka wanaonyemelea kupima kina cha maji kama kinawatosha ili kuingia katika mchakato.

Dar es Salaam. Hatimaye Spika wa Bunge, Tulia Ackson amevunja ukimya kwa kusema wanaotaka kugombea ubunge Mbeya Mjini wapime kina cha maji kama kinawatosha waingie kwenye kinya’ng’anyiro.

Spika Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Mbeya Mjini ametoa kauli hiyo leo Mei 4, 2023 Alhamisi wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha runinga nchini akiwa katika makazi yake Jijini Dodoma.

Katika mahojiano hayo Dk Tulia ameeleza sababu za kutaka jimbo hilo kugawanywa akisema suala hilo halihusu Mbeya Mjini pekee bali katika majimbo mbalimbali makubwa na hatua hiyo itasaidia kusogeza huduma karibu.

“Ubunge wangu haijalishi jimbo limegawanya au halijagawanywa, mimi ndio Mbunge kama nilimtoa mtu (Sugu) katika kata 36, hataweza kunitoa kata zikiwaa chache kweli? Mbona itakuwa mtihani, zikibaki kata 36 nitawafyeka.

“Nisingeshangaa kujadiliwa na wao, tena napenda sana wao wameanzisha huo mjadala nimefurahi na wanaposema watanifuata, nataka wajipime kama wanaona kina cha maji cha kinawatosha waje, kama niliwatoa na kata 36 wataniweza wapi na kata chache? amehoji Dk Tulia.

Kauli hiyo imekuja baada ya jana Jumatano, Bunge kutaarifikiwa kuwa kiongozi huyo ni miongoni wa wabunge waliowasilisha maombi ya kugawa majimbo yao ili kuwa mawili kutokana na ukubwa na wingi wa watu na hivyo kurahisisha shughuli za maendeleo.

Taarifa hiyo ilitolewa na bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda.

Katika swali la nyongeza kwa Serikali, Mwakagenda, aliuliza ni lini serikali italigawa jimbo la Mbeya mjini kutokana na ukubwa wake.

Jana baada ya kusambaa kwa taarifa hiyo, mjumbe wa kamati ya Chadema, Godbless Lema alisema hata jimbo la Mbeya Mjini likigawanywa watamfuata Dk Tulia huko huko anapogombea.

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 uliolalamikiwa na vyama vya upinzani, Dk Tulia alishinda kwa kura 75,225 dhidi ya Sugu 37,591 aliyeongoza jimbo la Mbeya Mjini kwa miaka 10 mfululizo kuanzia mwaka 2010/20.

Dk Tulia aliyewahi kuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba, amesema aliyeulizwa swali hilo jana bungeni Mwakagenda apewe sifa yake, kwa sababu jimbo likigawanywa huduma zinazongezeka kwa wananchi.

“Kwa mfano sasa hivi jimbo la Mbeya Mjini lina kata 36, kama litawagawanywa kata zitakuwa katika majimbo mawili na wabunge tutakuwa wawili. Kimsingi jimbo limejaa, lakini huu mchakato sio wa Mbeya pekee.

“Wabunge wengi wanaodai mgawanyo wa majimbo hawajaibuka tu, zipo sababu za msingi ambazo ni kuwasogezea wananchi huduma. Yakiwa majimbo, vigezo vinaongezeka na baadaye zinaweza kuwa halmashauri ambapo kila moja itakuwa na yake na hivyo kutoa huduma zote kwa wananchi,” amesema.