Juma Nature: Hata nikifa leo nikafufuka, P Funk Majani ni sehemu ya maisha yangu

Juma Nature: Hata nikifa leo nikafufuka, P Funk Majani ni sehemu ya maisha yangu

Muktasari:

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Juma Nature, maarufu Sir Nature, amesema kama kuna vitu hatavisahau maishani mwake ni kukutana na mtayarishaji wa muziki P Funk Majani.

Msanii wa muziki wa kizazi kipya Juma Nature, maarufu Sir Nature, amesema kama kuna vitu hatavisahau maishani mwake ni kukutana na mtayarishaji wa muziki P Funk Majani.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Nature alisema kuna wakati hata hakumbuki vizuri walivyokutana, ingawa alikuja kung’arisha maisha yake.

“Haikuwa kazi rahisi kumfikia Majani, kwanza ile rangi unajua ukimgusa anatema ung’eng’e, lakini mimi aliponisikiliza alikubali kipaji changu na nikaanza kufanya naye kazi”alisema Nature.

“Namba moja ndio hilo la kukutana na P Funk kwa sababu ni tukio lililosababisha mimi niwe Juma Nature Kirobotooooo. Pia nilivyoachana na mke wangu, sipendi sana kuongelea maisha yangu yasiyohusu muziki, lakini hilo liliniumiza sana lilipotokea na siwezi kulisahau, sema kama mwanaume unapiga moyo konde maisha yanaendelea. Na la tatu ni jinsi nilivyopokea tuzo ya muziki kutoka Afrika kusini mwaka 2007.” anasema.

Mwaka 2007 Nature alitunukiwa tuzo ya msanii bora kutoka Afrika Mashariki kupitia wimbo wake wa “Mugambo”. Tuzo hiyo ya Channel O Music Video Awards pia inafahamika kama Spirit of Africa Music Video Awards.

Alisema wapo watu wengi wa kuwakumbuka katika safari yake ya maisha, akiwemo marehemu Ruge Mutahaba ambaye alitoka mikononi mwake kuelekea kwa P Funk.

Alisema aliimba nyimbo nyingi hadi alipotoa wimbo uliomtambulisha katika kiwanda cha muziki “Jinsi kijana anavyobadili tabia”, ndipo Mutahaba, alimjumuisha katika kundi alilokuwa akilisimamia liitwalo Smos Vibes, lililokuwa na wasanii wakongwe kama Judith Wambura, maarufu “Lady Jay Dee”, Mr Paul na ZB.

“Hapa ndipo P Funk Majani aliponiona na kuhitaji nifanye naye kazi, huwezi amini nilipoondoka na kundi likavunjika, ambapo Mr Paul na Lady Jay Dee, wakawa wanafanya kazi na lebo nyingine.

Alisema hapa sasa ndiyo alikubali kuwa Majani ni Mkono wa Mungu, kama wengi wanavyomuita.

“Tukatengeneza albamu ya “Nini Chanzo” ambayo ilikuwa na wimbo wangu ulionitambulisha katika muziki wa “Jinsi Kijana anavyobadili tabia”.

“Hapa ndipo nilipopaishwa kama siyo kuupaisha muziki wa Bongofleva, Majani alikuwa akitengeneza ngoma inakuwa ngoma kweli na anaisimamia mauzo yake.Kuhusu maisha anayoishi Nature anasema ni ya kawaida na yupo huru anaweza kwenda gengeni au dukani kununua mahitaji.

“Kama unavyoniona sina walinzi.haahaaa”anasema huku kucheka.

“Tatizo wasanii wa siku hizi wanafanya muziki hata hawaelewi uzito wake. Siku hizi mtoto anamaliza darasa la saba na mimba juu, haya mamiziki ya matusi tunayowasikilizisha watoto wetu yanachangia.” ameongeza.