Jumuiya ya Ismaili kutekeleza programu ya kutoa elimu ya mazingira

Mratibu wa Programu ya Utoaji Elimu ya Utunzaji wa Mazingira kutoka Jumuiya ya kimataifa ya Ismaili Civic, Shenzada Walli (kulia) akizungumza na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Muhimbili, Jovita Mushi (katikati) na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule ya Msingi Umoja wa Mataifa, Methodia Kibasa jijini Dar es Salaam juzi. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Jumuiya ya kimataifa ya Ismaili Civic imepanga kuyawezesha majiji matano nchini likiwamo Dar es Salaam kutekeleza program ya elimu ya utunzaji mazingira na mbinu za kujikinga na maambukizi ya Uviko-19.

Dar es Salaam. Jumuiya ya kimataifa ya Ismaili Civic imepanga kuyawezesha majiji matano nchini likiwamo Dar es Salaam kutekeleza program ya elimu ya utunzaji mazingira na mbinu za kujikinga na maambukizi ya Uviko-19.

 Majiji mengine yatakayonufaika programu hiyo endelevu itakayozinduliwa Jumapili ijayo ni Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Taasisi ya Nipe Fagio.

Siku hiyo ya uzinduzi, wanategemea zaidi ya watu 20,000 kutoka jamii ya Ismaili kujitolea kwa saa 10,000 kusaidia wananchi wanaowazunguka kwa mataifa 27 dunia ikiwamo Tanzania.

Akizungumza juzi kwenye maandalizi ya uzinduzi wa program hiyo itakayofanyika Shule za Msingi Muhimbili na Umoja wa Mataifa, Mratibu wa Kampeni hiyo, Shenzada Walli alisema wanaanzia kwenye shule hizo za msingi kwa kuwa ni sehemu nzuri ya kutoa elimu kwa urahisi.

“Programu yetu imejikita sehemu mbili kwanza kutoa elimu ya utunzaji mazingira na namna ya kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama Uviko-19, tunategemea kuanza kwenye majiji matano na elimu ya mazingira tutaanza kutoa,” alisema Walli.

Mtaalamu wa Mazingira kutoka taasisi ya Nipe Fagio, Willhard Shishikaye aliipongeza jumuiya hiyo kwa kampeni hiyo na kueleza wao watajikita kutoa elimu namna ya kutunza taka ngumu na laini.

“Tutawaeleza namna wanavyotakiwa kuzitunza kwa kuwa na sehemu maalumu ikiwemo kuandaa miundombinu ya majitaka ili kurejesha mazingira katika ubora utakaowavutia wanafunzi kusoa,” alisema Shishikaye.

Mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Muhimbili, Jovita Mushi alisema “ukarabati huo unaenda kuboresha mandhari ya shule zetu na itawasukuma wanafunzi kuendelea kujifunza zaidi kwa kuwa wanapenda kusoma sehemu nzuri tofauti na sasa mangi yamechakaa tofauti na shule zingine.”

Naye Woindumi Siyao, mwalimu mkuu msaidizi wa Shule ya Msingi Umoja wa Mataifa, alisema jumuiya hiyo imefanya jambo jipya ambalo hata taasisi zingine zinapaswa kuiga ili kuhamasisha kuboresha mzingira ya kujifunzia ambayo ni muhimu katika kuboresha elimu nchini.