Nafuu ya upimaji uviko-19: Madereva ni bure, watoto hawapimi

Nafuu ya upimaji uviko-19: Madereva ni bure, watoto hawapimi

Muktasari:

  • Serikali imesema kuanzia Septemba 19 madereva wa magari ya mizigo wote watapimwa kipimo cha haraka cha Uviko-19 (C19 RAT) bila malipo wanapoingia nchini, huku watoto chini ya miaka mitano, wafanyakazi wa ndege na wanaounganisha safari wakipewa nafuu ya kutopima.

Dar es Salaam. Serikali imesema kuanzia Septemba 19 madereva wa magari ya mizigo wote watapimwa kipimo cha haraka cha Uviko-19 (C19 RAT) bila malipo wanapoingia nchini, huku watoto chini ya miaka mitano, wafanyakazi wa ndege na wanaounganisha safari wakipewa nafuu ya kutopima.

Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kuhuisha mwongozo namba 7 uliotolewa Mei 4 mwaka huu na kutoa toleo namba 8, baada ya tathmini ya hali ya maambukizi ya Uviko-19 duniani na mahitaji ya upimaji wa ugonjwa huo nchini.

Taarifa iliyotolewa na Mganga Mkuu wa Serikali Dk Aifelo Sichwale, ilieleza kuwa hayo ni makubaliano yaliyofanywa na wizara za afya Tanzania na Zanzibar.

Miongoni mwa mambo muhimu yaliyozingatiwa katika mwongozo huo ni pamoja na kutohitajika kwa cheti cha RT-PCR wala kipimo cha (C19RAT) kwa watoto chini ya miaka mitano, wafanyakazi ndani ya ndege na abiria wanaounganisha safari.

Abiria wanaoingia nchini kupitia usafiri wa nchi kavu watawajibika kuwasilisha cheti halali cha kuthibitisha kuwa hawana maambukizi ya Uviko-19.

“Kuendelea na upimaji afya wasafiri wanaoingia nchini na upimaji wa Uviko-19 kwa kutumia kipimo cha haraka cha Covid-19 Rapid Antigen Test (C 19RAT) kwa baadhi ya wasafiri wanaotoka katika nchi zenye maambukizi makubwa, kulingana na mwenendo wa ugonjwa kwenye nchi wanazotoka. Serikali itakua ikiainisha nchi hizi mara kwa mara kupitia tovuti ya Wizara,” ilieleza.

Mwenyekiti wa chama cha wafanyakazi madereva Tanzania (TADWU) Schubert Mbakizao alisema, wamepokea kwa mikono miwili uamuzi huo wa Serikali huku akitaja baadhi ya changamoto.

“Tatizo ni mazingira ya vipimo kuwafikia madereva pale mpakani. Wizara inatutaka tutume taarifa saa 24 kabla ya kufika mpakani lakini tatizo kubwa madereva wengi hawana simu za kisasa,’’ alisema.