Masharti ya chanjo yaanza kuwabana wasafiri

Masharti ya chanjo yaanza kuwabana wasafiri

Muktasari:

  • Baadhi ya nchi za bara la Ulaya zimeanza kuweka vikwazo kwa wasiochanja chanjo ya Covid-19 baada ya kuchanja idadi kubwa ya raia wao, hata hivyo Wizara ya Afya imesema ni vema msafiri akauliza shirika la ndege analokwenda nalo pamoja na masharti ya nchi anayotembelea.

Dar es Salaam. Baada ya nchi mbalimbali kuchanja idadi kubwa ya watu wao chanjo ya corona, baadhi zimeanza kuweka masharti kwa wageni wanaoingia kuwa ni lazima wawe wamechanjwa dhidi ya virusi vya corona.

Nchi hizo sasa zimeanza kuweka masharti hayo kupitia baadhi ya mashirika ya ndege yanayobeba abiria, kuwa hawatakubali kumpokea raia yeyote ambaye hajachanjwa ili kudhibiti virusi hivyo kwenye nchi zao.

Hata hivyo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa ufafanuzi kuwa hakuna sharti la chanjo ya corona kwa wasafiri wanaokwenda nje ya nchi.

Kaimu Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini-Afya, Catherine Sungura amesema ni vema msafiri akauliza shirika la ndege analokwenda nalo pamoja na masharti ya nchi anayotembelea.

“Kwa zile nchi ambazo zinahitaji kipimo cha Covid-19 msafiri afanye kipimo hicho ndani ya saa 24 hadi 48 kabla ya kuanza safari.

“Upimaji unafanyika kwa msafiri kufanya booking kupitia pimacovid.moh.go.tz ambapo atachagua kituo cha upimaji. Baada ya upimaji majibu yatatumwa kwake kwa njia ya barua pepe aliyotumia wakati wa booking. Akifika Airport cheti hicho kitahakikiwa katika dawati la afya. Unashauriwa kujiepusha na vyeti feki,” amesisitiza.

Waliokwama wafunguka


Baadhi ya wasafiri waliokwama kusafiri kufuatia sharti hilo ambao hawakutaka majina yao yatajwe, wamesema walizuiwa wakiwa tayari wamefika katika viwanja vya ndege kwa ajili ya ukaguzi wa awali ‘check in’ kwenye madawati ya ndege husika.


“Nilipata usumbufu mkubwa wakati wa kusafiri pale KIA ‘Kilimanjaro International Airport’ niliambiwa nchi ninayokwenda iliyopo bara la Ulaya haikubali raia ambaye hajachanjwa,” amesema mmoja wa wasafiri hao aliyekwama wiki moja iliyopita.


Abiria waliokwama wamesema si nchi zote zina sharti hilo ila ni baadhi ya nchi.


Mmoja wa madereva teksi anayefanya shughuli zake katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA)-Terminal 3, Juma Abdul amesema kumekuwa na abiria kadhaa kukwama kusafiri kwa takribani mwezi mmoja sasa.

Soma hapa: Wanafunzi wakimbia shule wakiogopa chanjo ya Corona
“Hili suala limekuwepo kabla hata ya chanjo kuingia nchini, kuna abiria walikuwa wanasafiri na Emirates walikwama sababu hawakuwa wamechanjwa, niliwarudisha mimi mwenyewe walilalamika sana na hao wanazuiwa na mashirika ya ndege wanapofanya ukaguzi wa awali,” amesema Juma.


Juzi mwanahabari wa kujitegemea Pascal Mayala  aliandika andiko lake mtandaoni akisema japo chanjo ya corona ni hiari, lakini kwa watu wanaotumia usafiri wa anga kwa safari za kimataifa, chanjo ni muhimu.


“Ili upande ndege, ni lazima upime corona na kupewa cheti kinachoonyesha hauna. Hivyo chanjo ni muhimu ili kujiihakikishia usalama usiipate corona kirahisi , kwasababu siku hizi, ili usafiri nje ni lazima upime na kuonyesha cheti kuwa umepima na huna ndio unapanda ndege.

Ukichanja unazuia uwezekano wa wewe kupata corona kwa urahisi,” amesema Mayala.
“Zamani ukiingia tu Airport unawahi counter ya check in. Sasa ukiingia unaanzia meza ya vérification ya cheti cha kupima corona. Baada ya kuhakikiwa kuwa umepima na umekutwa huna ndio unaanza ukaguzi.


“Japo chanjo ya Corona ni hiari, kwa watu wanaosafiri safiri, ni muhimu sana hivyo hata kama ulipanga kuitumia hiyari yako usichanje, nakushauri kachanje!” aliandika Pascal Mayala.