Kaburi la Membe hili hapa

Mkuu wa Mkoa wa Lindi (mwenye ushungi wa njano), Zainabu Telack akipata maelezo kutoka kwa wajenzi wa kaburi la Bernard Membe lililopo katika kijiji cha Rondo Kata ya Chiponda.

Lindi. Ujenzi wa Kaburi la aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe atakayezikwa keshokutwa Mei 16, 2023 katika makaburi ya Kanisa Katoliki yaliyopo Kijiji cha Rondo Kata ya Chiponda uko katika hatua za mwisho kukamilika.

Kwa mujibu wa mafundi kaburi hilo linalojengwa kwa matofali ya block na marumaru asilimia kubwa ya ujenzi huo utakamilika leo na sehemu iliyobaki ya mfuniko wa zege itafanywa baada ya maziko.

Membe ambaye alifariki dunia Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Kairuki jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla anatarajia kuzikwa hapa katika Kijiji cha Rondo alichozaliwa miaka 70 iliyopita.

Akizungumza na Mwanachi Digital, leo Jumapili Mei 14, 2023 mdogo wa marehemu, Tasilo Membe, amesema mafundi kutoka Dar es Salaam kwa kushirikiana na wanakijiji wameifanya vizuri kazi ya kuchimba na kujenga kaburi hilo na wanaamini hakuna kitakachoharibika.

"Kazi imekwenda vizuri hivi sasa mafundi wanaweka marumaru na ninaamini hadi jioni watakuwa wamemaliza na tutakuwa tunasubiri mwili utakaoletwa kesho asubuhi kwa ajili ya taratibu nyingine na keshokutwa ndiyo tutazika," amesema

Tasilo amesema wanamzika Kaka yake katika makaburi ambayo yanatumiwa na familia yao walikozikwa wazazi wao (baba na mama) na jamaa wengine.

Amesema kaburi hilo liko katika eneo jirani na nyumbani kwa marehemu Membe na shule ya Msingi Chiponda aliyosoma na kila mara alikuwa akishiriki katika kuiboresha.

Mmoja wa mafundi wa kaburi hilo, Abdul Hamad amesema familia ndiyo hutoa maelekezo ya wanavyotaka kaburi husika lijengwe ikiwemo matumizi ya matofari na nakshi mbalimbali.

"Sisi tukishapata maelezo ya familia na eneo lilivyo tunaweza kushauri ikiwa tunaona kuna ulazima wa kufanya hivyo. Wengine wanaweza kukuambia tunataka ulaze tofari kuanzia chini mpaka juu, wengine wanaweza kukuambia ulaze za chini halafu za juu zinasimama, ujenzi wa makaburi hutofautiana kulingana na mahitaji ya wahusika" amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainabu Telack, aliyefika makaburini jioni kukagua ujenzi huo, amesema ameridhisha na ujenzi wake baada ya kuwahoji mafundi na familia ya Membe. 

Telack, amesema kuwa Lindi na wana Rondo wamempoteza kiongozi jasiri aliyejitolea kusaidia jamii yake katika sekta ya afya, elimu, miundombinu na uchumi.

"Ndugu yetu alionyesha kwa mfano namna ya kujitolea, leo hii tuna huzuni kubwa na kila tukiangaliana tunabaki kuulizana nani atarithi viatu vyake?, lililo muhimu kwetu ni kushirikiana bila kujali dini, kabila na itikadi za kisiasa" amesema

Amesema Membe licha ya wadhifa mkubwa aliokuwa nayo hakuacha kukumbuka jamii yake na kuiendeleza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

Mmoja wa waombolezaji, Fatuma Saidi, amesema anamkumbuka Membe alivyokuwa mstari wa mbele kusaidia vikundi vya kujikwamua kiuchumi.

"Alitamani sana sote tuendelee, kila ukikaa naye utaona yuko tofauti na viongozi wengine, kwake masilahi ya wengi ndiyo yalikuwa kipaumbele kwake" amesema

Shaban Hanga, amesema marehemu Membe, alichukia uvivu na kuomba omba na alitaka watu wajitegemee.

Naye mmoja wa wasaidizi wa marehemu Membe, Salum Kamiumba,  amesema Membe alikuwa mstari wa mbele kujenga nyumba za walimu, kukarabati shule, hospitali na miundombinu ili wana Rondo wajitegemee.

"Nimefanya naye kazi kwa zaidi ya miaka 20, alisaidia shughuli za kijamii akiwashirikisha rafiki zake kutoka ndani na nje ya nchi, tumepoteza mtu muhimu sana," amesema.

Kwa mujibu wa mdogo wa marehemu Membe, Tusilo mwili wa kaka yake unatarajiwa kupokewa kijiji Rondo kesho na utafikishwa nyumbani kwake ambapo taratibu mbalimbali za kifamilia zitaendelea na keshokutwa maziko yatafanyika.