Kagame awasha mwenge kukumbuka mauaji ya kimbari Rwanda

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakimshuhudia Rais wa Rwanda, Paul Kagame akiwasha mwenge wakati wa kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari Kigali, nchini Rwanda leo Aprili  07, 2024.

Muktasari:

  •  Marais kadhaa akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais mstaafu wa Marekani Bill Clinton wamehudhuria, siku hiyo ya Aprili 7 inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco), imeikabidhi Rwanda vyeti rasmi kwa maeneo manne ya kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ambayo yameongezwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia mwaka 2023.

Kigali. Rais Paul Kagame, leo Aprili 7, 2024, amewasha mwenge kwenye kumbukumbu ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari nchini Rwanda akiashiria simanzi kwa Taifa hilo na dunia kwa ujumla.

Tukio hilo linakumbusha jinsi ambavyo mauaji ya kimbari yaliyoanza Aprili 7, 1994 na kudumu kwa takriban siku 100 yalivyokuwa ya kuhuzunisha na yenye athari kwa jamii, ambapo watu takribani milioni moja wengi wakiwa kabila la Watutsi waliuawa nchini Rwanda.

Kuwasha mwenge ni ishara ya matumaini na mwanga, kuendeleza mwanga wa kumbukumbu kwa wale waliopoteza maisha yao, kuhakikisha kuwa historia haitasahaulika, na kudumisha ahadi ya kuhakikisha kuwa matukio kama hayo hayatokei tena.

Rais Kagame, kwa kuwasha mwenge, pia anasisitiza umuhimu wa umoja na uponyaji wa jamii ya Rwanda, pamoja na kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa kuheshimu tofauti za kitamaduni na kudumisha amani.

Kwa ujumla, tukio hilo la leo Aprili 7, 2024 ni ishara ya kumbukumbu, heshima, na ahadi ya kuhakikisha kuwa historia kama ile ya mauaji ya kimbari haitokei tena na taifa la Rwanda linaelekea kwenye  mustakabali bora na amani.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liliteua rasmi Aprili 7, kuwa Siku ya Kimataifa ya Kutafakari Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

Pia, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Audrey Azoulay amekabidhi kwa Serikali ya Rwanda vyeti rasmi kwa maeneo manne ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari yaliyoongezwa kwenye orodha ya urithi wa dunia mwaka 2023.

Kumbukumbu hiyo ambayo imefanyika leo Jumapili ya Aprili 7, 2024 Kigali nchini Rwanda, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton na Rais Samia Suluhu Hassan.

Aprili 3, 2024, Rais wa Marekani, Joe Biden alitangaza ujumbe wa Serikali ya Marekani ambao umehudhuria kumbukumbu hiyo inayofahamika kwa Kinyarwanda kama ‘Kwibuka 30’, ikimaanisha kumbukumbu ya miaka 30.

Viongozi wengine ambao wamehudhuria kumbukumbu hiyo ni marais, Salva Kiir (Sudan Kusini), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Petr Pavel (Jamhuri ya Czech), Andry Rajoelina (Madagasca), Mohamed Ould Ghazouani (Mauritanian) na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Pia, katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo, Shirika la kimataifa linalowakilisha Jumuiya ya Wayahudi la World Jewish Congress (WJC), katika nchi 100 kwenye Serikali, mabunge na mashirika ya kimataifa, limetoa taarifa inayosisitiza mshikamano wake na Rwanda katika kuadhimisha kumbukumbu hiyo.

“Mawazo yetu yako pamoja na wale wote walioathiriwa na suala hili la historia ya kutisha, waathirika, walionusurika na vizazi vyao. Tunaheshimu maisha yaliyopotea pamoja na nguvu ya kudumu ya wale walionusurika,” ilinukuliwa taarifa hiyo ya WJC.

Mahakama za usuluhishi

Katika kujaribu kurejesha utulivu na kuleta haki, Serikali ya Rwanda iliunda mfumo wa mahakama za usuluhishi wa jadi unaojulikana kama Gacaca. Mahakama hizo za Gacaca zilikuwa sehemu muhimu ya mpango wa kusuluhisha migogoro ya kitaifa na kuwafikisha wahusika wa mauaji ya halaiki mbele ya sheria.

Ingawa ilikabiliwa na changamoto nyingi, mfumo wa Gacaca ulifanikiwa katika kuleta haki na kusaidia mchakato wa kuponya jamii.

Mahakama hizo  zilifanikiwa sio tu katika kuleta haki kwa waathirika, lakini pia zilisaidia kujenga jamii imara na yenye amani.

Kupitia mchakato wa uwazi na ufanisi, watu wa Rwanda waliweza kukabiliana na maumivu yao na kuelekea kwenye njia ya upatanisho na umoja.

Yalisaidia kuweka msingi wa Rwanda mpya, ambayo ilijitahidi kuondokana na machungu ya zamani na kujenga mustakabali bora kwa vizazi vijavyo.

Kuhifadhi wahamiaji

Mauaji ya kimbari yameifanya Rwanda kuwa nchi yenye msimamo thabiti katika suala la kutoa hifadhi kwa wakimbizi.

Hatua hii ilichochewa na historia yake ya kutokuwa na amani kutokana na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Kupitia uzoefu wake wa kihistoria, Rwanda iligundua umuhimu wa kusaidia wakimbizi na wahamiaji, huku ikiamini kwamba kila mtu anastahili hifadhi na usalama.

Rwanda kwa sasa imeamua kuwachukua wahamiaji waliokimbilia Uingereza na kuwapa makazi nchini humo, chini ya mkataba kati yake na Serikali ya Uingereza.

Kwa kuchukua wahamiaji waliokwama Uingereza, Rwanda inaonyesha dhamira yake ya kusaidia katika mgogoro wa kimataifa wa wakimbizi.

Tahadhari matamshi ya chuki

Wakati Rwanda inaadhimisha miongo mitatu tangu mauaji ya kimbari mwaka 1994, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania, Pindi Chana amehimiza hatua za kimataifa dhidi ya matamshi ya chuki, ubaguzi na ghasia ili kuzuia kuenea kwa mauaji ya kimbari.

Waziri Chana amebainisha hayo leo jijini Dar es Salaam wakati mishumaa 30 ikiwashwa kama sehemu ya kumbukizi ya mauaji hayo yaliyogharimu maisha ya watu  milioni moja katika matukio ya kutisha ya 1994.

Akitafakari juu ya ukatili huo, Waziri Chana amesisitiza kushindwa kwa jumuiya ya kimataifa kuzingatia ishara za onyo za matamshi ya chuki na ubaguzi, na hivyo kusababisha madhara makubwa.

“Ninakumbuka vizuri ukaribu wa Tanzania kwenye mkasa huo, pia nikisimulia matukio ya kutisha yaliyoshuhudiwa kando ya Mto Kagera na wimbi la wakimbizi wanaotafuta hifadhi,” amesema.

Akitambua maendeleo ya Rwanda tangu siku hizo za mauaji, Chana ameupongeza uongozi wake na kusisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ili kuzuia ukatili huo usijirudie.

Mkuu wa Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Shabnam Mallick, ameunga mkono maoni hayo huku akisisitiza haja ya dharura ya umoja wa kimataifa dhidi ya itikadi kali, migawanyiko na chuki. 

Mallick ametoa pongezi kwa uthabiti wa walionusurika na vitendo vya ajabu vya watu wa kawaida ambao walihatarisha maisha yao ili kulinda wengine.

“Wakati Rwanda inaingia katika kipindi cha maombolezo na tafakari, ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa: kamwe dunia isishuhudie ukatili kama huu tena. Jumuiya ya kimataifa inapaswa kusimama kidete kupinga aina zote za chuki na ghasia,” amesema.

Wakati huohuo, Balozi wa Rwanda nchini Tanzania, Fatou Harerimana, amesisitiza dhamira ya kuhakikisha haitajirudia tena kote duniani. Licha ya changamoto hizo, ikiwa ni pamoja na kutafuta haki kwa wahalifu, Rwanda bado imejizatiti katika azma yake ya kuzuia mauaji ya kimbari popote pale duniani.

"Tuheshimu kumbukumbu ya waathiriwa kwa kusimama kidete kupinga chuki na migawanyiko, kuhakikisha kwamba masomo ya historia yanatuongoza kuelekea mustakabali wa amani na maridhiano," amesisitiza balozi Harerimana.