Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kahawa ya Tarime ya pili kwa ubora Tanzania, mkakati kuiboresha waanza

Baadhi ya akinamama wakichambua kahawa wilayani Tarime . Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Kahawa inayolimwa wilayani Tarime Mkoa wa Mara imeibuka mshindi wa pili kitaifa kwa ubora katika mashindanyo yaliyoendeshwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), mwaka huu.

Tarime. Baada ya kahawa ya Tarime mkoani Mara kupata ushindi wa pili kwa ubora wa kahawa nchini, Chama Cha Wakulima mkoani humo (Wamacu) kimeanza mikakati ya kuboresha kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza uzalishaji wake.

Kahawa hiyo iliibuka mshindi wa pili kitaifa katika mashindano yaliyohitimishwa mwishoni mwa Mwezi Oktoba 2023, Mjini Moshi ikitanguliwa  na kahawa ya Arusha shindano lililondeshwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB).

Meneja Mkuu wa Wamacu, Samuel Marwa amesema mjini hapa leo Novemba 9, 2023 kuwa uzalishaji wa zao hilo unatarajiwa kupanda hadi kufikia tani zaidi ya 600 mwishoni mwa msimu huu.

“Tayari tumeajiri maofisa kilimo watatu ambao watahakikisha wanawafikia wakulima kwa wakati na kutoa ushauri wa kitaalamu juu ya kilimo bora na cha kisasa, huu nao ni mkakati mmojawapo wa kuongeza uzalishaji, ubora  na mavuno pia,”amesema 

Amesema chama hicho kitahakikisha kinasambaza miche ya kahawa kwa wakulima wote wanaopenda kulima zao hilo akidai miaka ya nyuma wakulima wilayani Tarime waliacha kulima kahawa kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo soko na bei isiyoridhisha.

Marwa amesema baada ya jitihada zilizofanywa na Serikali ya mkoa hivi sasa uzalishaji wake  umeongezeka kutoka tani 280 mwaka 2020 hadi kufikia tani 317 mwaka huu na kwamba mbali na kuongeza uzalishaji pia wanatarajia kuwa na kahawa iliyokobolewa ambapo hivi sasa wana kahawa isiyokobolewa pekee.

Amesema ubora huo wa kahawa una faida nyingi hasa kwa  wakulima kwani pamoja na mambo mengine utapelekea kuwepo kwa soko la uhakika la kahawa kutoka eneo hilo.

Baadhi ya wakukima wamesema ubora huo umetokana na usimamizi thabiti uliofanywa na Wamacu muda wote kuanzia shambani hadi baada ya mavuno. 

"Tumefundishwa namna ya kuvuna kitaalamu kwamba hatutakiwi kuchuma kahawa iliyoiva tukachanganya na ambayo haijakomaa na hata kuanika kuna namna ya kuanika kitaalamu tumefundishwa,"amesema Steven Marco

Marco ametoa rai kwa Wamacu kuendelea kuhamasisha wakulima wengi zaidi waweze kulima zao hilo la biashara kwa maelezo kuwa wengi waliachana na kilimo hicho baada ya kuona hakina tija.

“Sasa hivi tumeuza kilo moja kwa Sh2,500 tofauti na zamani ambapo tulikuwa tukiuza kilo moja kwa Sh600 kwahiyo kutokana  na faida iliyopo huku kwenye kahawa wakulima wakipata elimu naamini wengi zaidi wataanza kulima,"amesema  Marwa Nyasirori

Jitihada za Mwananchi Digital kumtafuta Ofisa Kilimo Mkoa wa Mara, Lazaro Butilikwa kuzungumzia mikakati ya mkoa ya kuhakikisha uzalishaji wa zao hio unaongezeka hazikuzaa matunda.

Awali kahawa ililimwa Wilaya ya Tarime pekee lakini hivi sasa inalimwa wilaya za Butiama, Serengeti na Rorya.