Kamati Kuu Chadema yaanza kikao cha siku tatu, wagombea kanda nne wawasili Dar

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe  na Makamu wake, Tundu Lissu wakijadiliana kabla ya kuanza kikao cha Kamati Kuu leo Mei 11, 2024 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

  • Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kimeanza katika ofisi za makao makuu mapya ya chama hicho chini  ya Mwenyekiti Freeman Mbowe huku wagombea wa nafasi mbalimbali ndani ya kanda nne wakiorodhesha majina yao kwenye makao makuu ya zamani, Ufipa Wilaya ya Kinondoni.

Dar es Salaam. Kikao cha Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza mchana huu katika ofisi za mpya za makao makuu ya chama hicho, Mikocheni wilayani Kinondoni.

Kikao hicho pamoja na mambo mengine, kitafanya mchujo wa wagombea kwenye nafasi mbalimbali kwenye ngazi Kanda nne za Nyasa, Serengeti, Victoria na Magharibi huku wagombea wenyewe wakiripoti katika makao makuu ya zamani Mtaa wa Ufipa, Kinondoni.


Baadhi ya wajumbe wa kamati Kuu ya Chadema wakiwa kwenye kikao kilichoanza leo Mei 11, 2024 jijini Dar es Salaam. Picha na Michael MatemangaKikao hicho cha siku tatu kilichoanza leo Jumamosi Mei 11, 2024, mbali na usaili na mchujo huo, kitakuwa na ajenda za kupokea taarifa ya chaguzi katika ngazi mbalimbali za chamana tathmini ya maandamano na.

Suala jingine ambalo linatajwa huenda likajadiliwa ni  kauli ya Makamu Mwenyekiti wake Bara, Tundu Lissu  aliyoitoa Me 2 mwaka huu mkoani Iringa, kuhusu uwepo wa fedha zilizomwagwa kwenye uchaguzi wa ndani wa Chadema kwa lengo  la kuvuruga uchaguzi huo.

Katika hotuba yake siku hiyo Lissu alisema: “Leo kwenye uchaguzi kuna hela ya ajabu, ninyi mnafikiri hiyo hela ni ya wapi? Mnafikiri hiyo hela ni ya nani? Mnafikiri hiyo hela itatuacha salama? Ukitaka kujua kwamba hatuko salama, fuatilia mitandaoni,” amesema Lissu.

Kauli hiyo ya Lissu iliibua mjadala kutoka kwa wadau mbalimbali waliotaka mamlaka husika kulifanyia uchunguzi suala hilo, kwa kuwa vitendo vya rushwa havikubaliki kwenye chaguzi.

Uchaguzi wa kanda hizo za awamu ya kwanza, unafanyika baada ya kukamilisha mchakato katika ngazi ya chini ya msingi hadi mkoa.

Miongoni wa wajumbe wanaohudhuria kikao hicho ni Godbless Lema, Mchungaji Msigwa, John Mnyika (katibu mkuu), Grace Kiwelu, Suzan Kiwanga, Benson Kigaila na Said Issa Mohamed (makamu mwenyekiti – Zanzibar.


Hali ilivyo Ufipa, Kinondoni

Katika hatua nyingine, baadhi wagombea katika nafasi mbalimbali za kanda wameripoti katika ofisi za makao makuu ya zamani, Mtaa wa Ufika, kinondoni kwa ajili ya taratibu mbalimbali za kiuchaguzi.

Mwananchi Digital imeshuhudia wagombea hao wakijiandikisha katika daftari maalumu kama ambavyo barua wa wito ilivyowataka, ili kutambua uwepo wao.

Maazimio ya kikao hicho yanatazamiwa kutolewa na Mbowe muda wowote baada ya kukamilika.