Kamati ya Bunge yaagiza fidia mgodi wa Nickel iharakishwe

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Tembo Nickel, Benedicto Busunzu akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Nishati na wenzao wa Kamati ya Madini, Ardhi, Maliasili na Utalii wakati alipokuwa akiwaonyesha ramani ya Wilaya ya Ngara na eneo lilipo mgodi wa madini ya Nickel. Wajumbe wa Kamati hizo wametembelea mradi huo Novemba 14, 2023. Picha na Alodia Dominick

Muktasari:

Zaidi ya Sh26.5 bilioni zitatumika kulipa fidia wananchi kupisha mradi wa kuchimba Nickel wilayani Ngara inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali yenye asilimia 16 na mwekezaji anayemiliki asilimia 84.

Ngara. Kamati za Bunge za Nishati na ile ya Madini, Ardhi, Maliasili na Utalii imeagiza mchakato wa malipo ya fidia kwa kaya 1,339 zinazoishi jirani na mgodi wa Tembo Nickel uliopo Wilaya ya Ngara mkoani Kagera zinazotakiwa kuhama ukamilike harake kuwezesha mradi huo kuanza.

Agizo hilo limetolewa leo Novemba 14, 2023 na Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mzava mara baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji kutoka kwa Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Tembo Nickel, Benedicto Busunzu kuwa hadi sasa, ni kaya zaidi ya 800 kati ya 1,339 ndizo zimesaini mkataba wa kukubali kupokea fidia.

‘’Mchakato wa fidia unapaswa kuharakishwa na ikiwezekana malipo yafanyike kwa wote kwa awamu moja ili wananchi wapishe utekelezaji wa shughuli za uchimbaji; tusisubiri hadi miezi mitatu kama mpango wa sasa unavyoeleza,’’ amesema Mzava

Waziri wa Madini, Antony Mavunde ameunga mkono agizo hilo kwa kuutaka uongozi wa Tembo Nickel kuharakisha mchakato wa malipo ya fidia kuwezesha wananchi kuhama kwenda maeneo mengine kuanzisha maisha mapya kupisha mradi huo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Awali, katika taarifa yake, Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Tembo Nickel, Benedicto Busunzu amewaeleza wajumbe wa kamati kuwa fidia kwa wananchi wanaotakiwa kuhama kupisha uchimbaji wa madini ya Nickel inatarajiwa kutolewa kuanzia sasa na kukamilika ndani ya kipindi cha miezi mitatu ijayo.

‘’Malipo yote yatafanyika kwa njia ya benki na wahusika wamefungua akaonti zitakazotumika kuwaingizia fedha za fidia. Kaya zaidi ya 800 wameshasaini mikataba kukubali fidia,’’ amesema Busungu

Amesema katika mpango huo, kaya 990 zitafidiwa mashamba huku kaya nyingine 349 zitajengewa nyumba maeneo watakayopendekezwa na wahusika.

Zaidi ya Sh26.5 bilioni zitatumika kulipa fidia wananchi kupisha mradi wa kuchimba Nickel wilayani Ngara ambao Serikali inamiliki asilimia 16 huku mwekezaji akimiliki asilimia 84.

Akizungumzia faida na manufaa kwa jamii jirani, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa ameutaka uongozi wa mgodi huo kutoa tenda ya huduma na bidhaa zinazopatikana nchini, hasa Wilaya ya Ngaza na Mkoa wa Kagera ili Watanzania wanufaike kiuchumi na uwepo wa rasilimali ya madini ya Nickel katika maeneo yao.

Madini ya Nickel inapatikana katika Kata za Kata za Rwinyana, Bugarama na Bukiriro wilayani Ngara na mkataba wa kuyachimba ulitiwa saini mwaka 2021.