Kamati ya Bunge yaridishwa na Duwasa

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na hatua za utekelezaji wa miradi ya maji katika eneo la Nzuguni unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji imeridhishwa na hatua za utekelezaji wa miradi ya maji katika eneo la Nzuguni unaotekelezwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa).

Katika hatua za kukabiliana na changamoto ya maji kwenye Jiji la Dodoma hasa eneo la Nzuguni.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dk Christine Ishengoma wakati wa ziara yao baada ya shughuli za bunge walipotembelea visima vya maji vilivyochimbwa Nzuguni ili kupunguza makali ya mgao.


“Tumetembelea eneo hili la Nzuguni ambalo wananchi wake walikuwa na changamoto kubwa ya maji, hatimaye tatizo hili linaenda kutatuliwa kupitia visima hivi vitano vilivyochimbwa vinavyotoa maji safi na salama yasiyo na chumvi,” amesema Dk Ishengoma

Pia, amewaomba Duwasa kumaliza mradi huo ndani ya miezi sita kama walivyoahidi ili wananchi wasiendelee kuteseka na kero.

Hata hivyo, kamati inaridhishwa na jitihada za kuongeza vyanzo vya maji ili kupunguza makali ya mgao ambao umekuwa ni tatizo kubwa kwa makao makuu ya nchi.

“Kwa sasa hapa Dodoma walikuwa na shida sana ya maji, tunaona Serikali inajitahidi kutatua tatizo hili, na kabla ya miezi sita mradi utakamilika ili kupunguza adha kwa wananchi,” amesema

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema wizara hiyo iliwaelekeza wataalam wake kuyatafuta maji popote yalipo ili kuhakikisha Kata ya Nzuguni inaondokana na ukosefu wa huduma za maji safi, salama na yenye kutosheleza.

“Nishukuru kazi kubwa imefanyika inatupa matumaini eneo hili la Nzuguni, Ilazo na Kisasa ni maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na upatikanaji wa maji,” amesema Aweso

Amesema wzara inahakikisha fedha za mradi huu zitaendelea kutoka kwa wakati na imewaelekeza Duwasa kuhakikisha wanaaanzisha mradi mkubwa wa kujenga tanki litakalohifadhi lita milioni mbili na kutandaza mtandao wa mabomba wa zaidi ya Kilomita sita.

"Niwahakikishie kuwa suala la upatikanaji wa majisafi, salama na toshelevu kwa Dodoma ni jambo la dharura, hivyo wizara haitakuwa kikwazo katika upatikanaji wa fedha," amesema

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo wa maji Nzuguni umegharimu Sh4.05 bilioni utanufaisha wananchi 33,969.

Amesema umeongeza uzalishaji wa maji jijini Dodoma kutoka lita milioni 67.8 hadi lita milioni 73.8 kwa siku sawa na ongezeko la asilimia 9.

“Mgao wa maji utaondoka kwenye maeneo ya Nzuguni, Ilazo na Kisasa, pia tutapeleka maeneo mengine ya Njedengwa, Mwangaza, Mapinduzi, Iyumbu, Mlimwa, Swaswa na Ipagala," amesema

Aidha, Mhandisi Aron amesema ili kulinda chanzo cha maji kwenye eneo hilo, Halmashauri ya Jiji la Dodoma inatarajiwa kufanya uthamini wa eneo hilo ambalo bado linamilikiwa na wananchi ili kuwalipa fidia.

Pia, ameishukuru wizara ya maji kwa kuwa tayari kutenga fedha za kutekeleza Mradi huu kwa haraka na kupunguza adha ya maji katika maeneo husika, kipindi miradi mikubwa ya Mtera na Farkwa ikiendelea kutekelezwa.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Godwin Mkanwa amewataka wananchi kuendelea kutunza vyanzo vya maji na kuwa na matumizi sahihi ya maji.