Kamati ya Bunge yataja sababu matumizi madogo dawa za kufubaza VVU

Bunge lataka ufumbuzi msongamano wa wafungwa, mahabusu

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Dawa za Kulevya imesema vituo vya kutolea huduma kuwa mbali kunachangia utoro wa kutumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Ukimwi na Dawa za Kulevya imesema vituo vya kutolea huduma kuwa mbali kunachangia utoro wa kutumia dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Mwenyekiti wa kamati hiyo,  Fatma Toufiq ameyasema hayo bungeni leo Jumanne  Aprili 13,  2021 wakati akiwasilisha maoni ya kamati kuhusu makadirio mapato na matumizi ya fedha ya ofisi ya waziri mkuu na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2021/22.

“Changamoto ya watu wanaoishi na VVU kutoroka matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU kwa kiasi kikubwa umechangiwa na umbali wa vituo vya kutolea dawa, gharama za usafiri kutokana na watumiaji wengi kuwa wakazi wa maeneo ya pembezoni mwa halmashauri zao,” amesema.

Ameitaja changamoto nyingine ni baadhi ya Wa-VVU kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu makazi yao na mawasiliano yao, kutokana na hali iliyopo ya unyanyapaa.

Amesema hali hiyo pia imechangia kwa baadhi ya watumiaji wa dawa hizo kwenda kuchukua  katika vituo vilivyo mbali na maeneo wanayoishi.