Kamati ya Bunge yataka fedha za mikopo kwa vijana zitolewe

Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeshauri, Fatma Toufiq wakati akiwasilisha maoni kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mwaka 2023/2024 Jumatano Aprili 5,2023. Picha na Merciful Munuo.
Dar es Salaam. Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeshauri Serikali kutoa fedha zote zinazopangwa kwa ajili ya mikopo kwa vijana baada ya kubaini katika kipindi cha miaka mitano ni asilimia 20 tu ya fedha ndizo zimetolewa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Toufiq ameyasema hayo leo Jumatano Aprili 5, 2023 wakati akiwasilisha maoni kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mwaka 2023/2024.
Amesema kamati ilibaini kuwa katika kipindi cha miaka kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2020/2021 Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu ilitengewa Sh5 bilionii lakini katika kipindi hicho imepokea Sh1 bilioni sawa na asilimia 20 tu ya fedha zilizotengwa kwa kipindi husika.
Amesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 kiasi kilichotengwa ni Sh1 bilioni lakini mpaka kufikia Februari 2023 hakuna kiasi cha fedha kilichokuwa kimetolewa.
Amesema kamati hiyo inashauri kuwa Serikali itoe fedha hizo kila mwaka na kwa wakati na kuongeza kiasi cha mtaji wa mfuko huu ili kuongeza idadi ya vijana wanaopata mkopo kupitia mfuko huo kupata mtaji wa kuanzisha shughuli za uchumi.
“Kutorejeshwa kwa mikopo inayotolewa kwenye Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kunapelekea kutofikiwa lengo la kuendelea kukopesha vijana wengine,” amesema.
Ameitaka Serikali iweke mikakati madhubiti ya kuhakikisha kuwa fedha zinazokopeshwa zinarejeshwa kwa wakati ili kuhakikisha kwamba lengo la kukopesha vijana wengi linafikiwa.
Aidha, kamati hiyo imetaka Serikali ihakikishe kuwa mfuko huo unatangazwa ili kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kuwezeshwa kupitia mfuko huu.
Kamati ilibaini kuwa mwenendo wa fedha za bajeti ya utekelezaji wa programu ya kukuza ujuzi nchini umekuwa ukishuka kutoka Sh18 bilioni mwaka 2019/2020 hadi kufikia Sh9 bilioni mwaka 2023/2024.
Amesema hali hiyo imesababisha kushuka kwa vijana wanufaika kutoka wastani wa vijana 42,000 hadi 12,000.
Amesema kamati yake inashauri kuwa Serikali iongeze bajeti ya programu hiyo ili kufikia malengo ya mpango wa maendeleo ya Taifa wa jumla ya vijana 681,000 wanaotakiwa kupata mafunzo ya ujuzi katika kipindi cha miaka mitano.