Kamishna azuia utoaji hati eneo lenye mgogoro Arusha

Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Arusha, Geofrey Mwamsojo

Muktasari:

  • Mgogoro unatajwa kuwapo kwa miaka 17 sasa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Silaa aingilia kati

Arusha. Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Arusha, amezuia kutolewa hati za umiliki wa ardhi katika eneo la ekari sita, lililopo Kata ya Olmoti jijini Arusha kutokana na kuwapo mgogoro kwa miaka 17 sasa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa wiki iliyopita alitembelea eneo hilo na kuzungumza na William Mollel, anayelalamika eneo lake kuvamiwa pamoja na la majirani wa eneo hilo.

Waziri alitoa siku 30 kwa Kamishna wa Ardhi Mkoa wa Arusha, Geofrey Mwamsojo kutatua mgogoro huo.

Katika mgogoro huo, familia ya Mollel inamtuhumu aliyekuwa Ofisa Ardhi Jiji la Arusha, Christopher Kitundu ambaye amehamishiwa Wilaya ya Tandahimba kuuziwa eneo hilo kinyume cha sheria na kuanza kuuza viwanja.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Januari 28, 2024, Kitundu amekana kuvamia eneo hilo na kueleza wanaomlalamikia waende mahakamani badala ya kumtuhumu kuvamia eneo lao.

"Sijavamia eneo la mtu, kama kuna wanaonilalamikia, basi waende mahakamani," amesema.

Akizungumza jana katika kikao cha kutafuta suhulu la mgogoro huo, Kamishna Mwamsojo akiwa na Ofisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Neema Uloma amesema ameamua kusitisha utoaji hati wa viwanja katika eneo hilo hadi suluhu itakapopatikana.

Amesema katika kutekeleza maagizo ya Waziri Silaa, kesho akiwa na maofisa wake, watafika tena eneo lenye mgogoro kuzungumza na pande zote na majirani ambao pia wanalalamika kumegwa ardhi yao.

"Tumepata taarifa kupimwa kwa eneo hilo na maofisa wetu wa ardhi, licha ya kuwapo mgogoro na kuanza kuuzwa viwanja, taratibu za kinidhamu zinaendelea na sasa tumesitisha utoaji wa hati," amesema.

Awali, Mollel amesema kwa miaka 17 wamekuwa katika mgogoro, baada ya Neeva Savoroi kuvamia eneo hilo la shamba.

Amedai baada ya kifo cha Savoroi, mkewe Leah Neeva aliendelea kulimiliki kinyume cha sheria na kumuuzia Kitundu.

Amedai suala hilo lilifikishwa katika Baraza la Ardhi la Kata kwa shauri namba S/2006 ambalo alishinda.

Amedai baadaye shauri lilihamishiwa Baraza la Ardhi Wilaya ambako pia alishinda. Walioshindwa wakakata rufaa Mahakama ya Rufani, ambayo mwaka 2013 iliamuru shauri hilo lirejeshwe Baraza la Ardhi la Kata.

"Hata hivyo wakati shauri lipo bado katika baraza la ardhi, Kitundu alitumia maofisa wenzake wa ardhi, kwenda kupima eneo hilo na kukata viwanja ploti namba 60-70 Block A, Plan No E/248/205 Agosti mwaka jana," amedai.

Amesema baada ya tukio hilo, walipeleka malalamiko baraza la ardhi na ofisi za Serikali Kata ya Olmoti, ambao walifika shambani na kuagiza kusitishwa upimaji, lakini maofisa hao walikaidi.

Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Kata ya Olmoti, Yusuph Abdalah amekiri kuwapo shauri la mgogoro huo. Hata hivyo, amesema mlalamikiwa aliyeuza eneo hilo, Leah Neeva ameandika barua ya kutokuwa na imani na baraza, hivyo hatashiriki katika shauri hilo.

Neeva akizungumzia eneo hilo, ameeleza ni la familia yake na waliuziwa na Mollel, ambaye analalamika kwamba wamevamia.