Migogoro ya ardhi, ndoa na mirathi yatawala Wiki ya Sheria

Mkazi wa Tabata Liwiti, Charles Kagaruki (kulia) akipata elimu ya msaada wa kisheria kuhusu mgogoro wa ardhi kutoka kwa Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Kituo Jumuishi cha Masuala ya Ndoa, Talaka, Mirathi  na Watoto, Jacob Sifa baada ya kutembelea banda hilo.  Picha na Tuzo Mapunda

Muktasari:

Wananchi wamejitokeza katika Wiki ya Sheria kutoa kero zao za ardhi, ndoa na mirathi huku Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kikisisitiza umuhimu wa wadau kuzingatia haki za binadamu na utawala wa kisheria

Dar es Salaam. Baadhi ya Watanzania wenye changamoto za ardhi, ndoa, mirathi na familia wamejitokeza kwa wingi kupata msaada wa elimu ya kisheria kwenye maadhimisho ya Wiki ya Kisheria inayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam,  yalianza Januari 24  na kilele chake kitaifa ni Februari mosi Jijini Dodoma ambako Rais Samia Suluhu Hasaan atakuwa mgeni rasmi.

Wakizungumza kwa nyakati baadhi ya Watanzania hao, wamesema baada ya kusikia wiki hiyo wameenda kupata ushauri na elimu katika maeneo yanayowatatiza kisheria.

"Mimi nasumbuliwa na mgogoro wa ardhi na jirani yangu tangu mwaka 2017, naishi maeneo ya Ubungo Housing, pale jirani yangu anataka kunidhulumu eneo langu, ameshavuka mpaka niliopanda minazi na anajua kuwa ni kosa, lakini amekimbilia Serikali za mitaa,” amesema Gabriel Lyimo.

Amesema licha ya kupeleka malalamiko yake ofisi ya Serikali ya mtaa, lakini ameona ni vema akafika kwenye maonyesho hayo kusudi apate ushauri na usaidizi wa kisheria ili aweze kumaliza suala hilo.

Amesema jirani yake huyo (hakumtaja jina) ni mbabe na mbishi kwake na alishawahi kuwaita hadi majirani kusuluhisha mgogoro huo, lakini anaona kama imeshindikana.

"Kwa hiyo nimekuja nipate msaada zaidi, sitaki kushindana naye, nimefika hapa Kituo cha Haki za Binadamu, nimeongea na wakili amenishauri chakufanya, ngoja nikatumie mbinu niliyoelezwa ikishindikana wameniambia nirudi kwao,” amesema Lyimo.

Mkazi wa Tabata Liwiti, Charles Kagaruki amesema  anasumbuliwa na mgogoro wa nyumba ya urithi iliyoachwa na baba yao ambaye kwa sasa ni marehemu.

Amesema amefika viwanjani hapo kuonana na mawakili kusudi wamshauri afanyeje kisheria.

“Tuliachiwa nyumba na eneo kubwa tu na baba yetu, lakini wenzangu wanne walinizunguka wakaiuza bila kunishirikisha, kila nikiwafuata wananizungusha. Sasa nilivyosikia wanasheria wapo hapa leo, nikaona nije wanisaidie,” amesema Kagaruki.

Hata hivyo, Sabina Ndimbo mkazi wa Mbagala amesema: “Mume wangu alifariki dunia ghafla na tulikuwa tunaishi kwenye ndoa, kuna mali tulizochuma pamoja lakini zingine nilizikuta, baada ya kufariki ndugu zake wanataka kuchukua kila kitu bila kunizingatia mimi.”

Hata hivyo, amesema licha ya kulifikisha hilo suala ofisi ya Serikali ya mtaa anakoishi bado hajapata majibu ya moja kwa moja.

“Sasa leo nimekuja hapa kuomba msaada kwa wataalamu wenyewe wa sheria wanisaidie kutatua mgogoro huu,” amesema Ndimbo.

 “Nina watoto wangu bado wadogo lakini shinikizo limekuwa kubwa nahitaji msaada wa haraka nimekuja wenzetu wanajua pengine naweza kupata haueni.”

 Msimamizi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, (LHRC) Ofisi za Kinondoni, Wakili Rose Nyatega amesema kituo hicho kinaendelea kusisitiza umuhimu wa wadau wote katika mfumo wa utoaji haki kuzingatia haki za binadamu na utawala wa kisheria katika utendaji kazi wake.

“Madukuduku ya wadau ni wengi wanaokuja kwenye banda letu, kwa hiyo bado tunaendelea na uchechemuzi katika mambo mbalimbali na  kusimamia maoni yetu  tuliyotoa kwa Tume ya Haki Jinai kuona kama yanafanyiwa kazi ili suala la haki ya binadamu inatamalaki nchini,”amesema Wakili Nyatega.

Wakili Nyatega amesema katika banda lao Watanzania wakienda wanapewa msaada wa kisheria na kuwapa vitabu vinavyotoa elimu ya haki za kibinadamu kwa lugha rahisi.

Hakimu Mkazi Mawandamizi kutoka Kituo cha Jumuishi cha Masuala ya Familia na Mirathi, Jacob Sifa amekiri katika banda lao kupokea zaidi ya Watanzania 60  wengi wao  wanaohitaji msaada wa kisheria kwenye eneo la mirathi na mgawanyo wa watoto.

“Wengi waliokuja hapa ni malalamiko ya watoto na mgawanyo wa mali na mirathi tunaona yanaanza tangu nyumbani kwao wanavyoshirikiana na mwisho wasiku yanakuja kujitokeza  katika kesi,”amesema Sifa.

Hakimu Jacob amesema suala la mgawanyo wa mali wao wanavyofanya maamuzi wanaangali nani alichangia mali nyingi.

 “Mwenye mchango mkubwa anapata kingi na mwenye mchango wa wastani anapata kidogo,”amesema Sifa.

Amesema kwenye suala la mgawanyo wa watoto wanazingatia masilahi ya mtoto zaidi kwa kuangalia aliyekuwa na mazingira mazuri kuliko mwenzake anapewa kipaumbele zaidi.

“Matunzo ya watoto yanategemeana kipato cha mtu anayetakiwa kupewa,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila aliyekuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maadhimisho hayo, amewaomba wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kupata msaada na elimu kwa mambo ya kisheri yanayowapa shida.

“Kama una changamoto ya kisheria si wakati wa kukaa nyumbani, ni muhimu kujitokeza katika maonesho haya kupata elimu badala ya kuendelea kulalamika mtaani,” amesema Chalamila.

Jaji Mfawidhi Kanda ya Dar es Salaam, Salma Magimbi amesema Mahakama Tanzania imetenga wiki hiyo kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwa bado uelewa wa Watanzania uko chini wa kisheria.

Madhimisho hayo yanakauli mbiu isemayo: “Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo jumuishi wa haki jinai.”