Majaliwa akomalia migogoro ya ardhi

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati akitoa hoja ya kuhitimisha bunge jijini Dodoma jana. Picha na Merciful Munuo

Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amerudia agizo lake kuhusu kuzichukulia hatua kali kampuni zilizopewa miradi ya upimaji ardhi katika majiji lakini hazijakamilisha kazi.

Agizo hilo linamtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kusitisha shughuli za kampuni hizo bila kujali kama walikuwa na mikataba au hawakuwa nayo, lakini kama wameshindwa kufikia malengo kwenye kazi zao waache kuendelea.

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana, alipohitimisha Mkutano wa 13 wa Bunge la 12, litakalokutana tena Januari 30, mwakani.

Alisema suala la migogoro ya ardhi halihitaji mjadala.

Hii ni mara ya tatu kwa Waziri Mkuu Majaliwa kuzungumzia masuala ya utendaji ndani ya Wizara ya Ardhi katika kipindi cha miezi miwili.

Hivi karibuni, aliwaita viongozi wa majiji yote na kuwataka wakamalize migogoro ya ardhi.

Mtendaji huyo mkuu wa Serikali, alikwenda mbali zaidi kwa kuwataja baadhi ya waliokuwa viongozi wa Jiji la Dodoma, akielekeza wahojiwe kutokana na matumizi mabaya ya fedha.

Kauli ya Waziri Mkuu ilisababisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kuanzisha alichokiita kliniki ya ardhi ambayo wataalamu wanakutana na wananchi kila kata kuzungumzia changamoto zao, huku nyingi zikionekana kutatuliwa.

“Namuagiza Waziri wa Ardhi aendelee kuwachukulia hatua viongozi wote ndani ya wizara hiyo ambao wanasababisha migogoro na uonevu wa kuchukua ardhi za wananchi ili iwe fundisho kwa watumishi wengine ndani ya Serikali,” alisema Majaliwa.


Maeneo ya Serikali

Waziri Mkuu pia alipiga marufuku matumizi ya ardhi ambazo zimetengwa kwa ajili ya shughuli za kiserikali, ikiwamo maeneo ya ukanda wa kijani akitaka mpango huo kabla ya kubadili matumizi yake, washirikishe kamati za ulinzi na usalama za wilaya.

Aliyataja maeneo ya Kigoma na Dodoma kwamba yana maeneo kama hayo.

Agizo lingine alilitoa kwa wakuu wa wilaya kote nchini, aliwataka kusimamia uandikishaji wa wakulima wenye kuhitaji mbolea na pembejeo ili taarifa zao ziingizwe kwenye mfumo.

Kwa upande wa kampuni zinazozalisha mbegu bora, alizitaka kuongeza kasi ya uzalishaji.

Viongozi hao wa wilaya pia wanatakiwa kuimarisha kamati za maafa kutoka ngazi ya vijiji ili inapotokea suala la maafa, hasa kipindi cha mvua, kusiwe na tabu wala mgongano wa jinsi ya kuwasaidia wananchi.

Kuhusu shule, aliwaagiza watumishi waliopewa dhamana ya kusimamia ujenzi wa madarasa wakamilishe ifikapo Novemba 30, mwaka huu, vinginevyo wahusika wachukuliwe hatua kwa kuwa fedha zilishapelekwa na hakukuwa na sababu ya kuchelewa kukamilisha kazi hiyo.

Aidha, Majaliwa alisisitiza wanufaika wa mikopo ya elimu ya juu kuendelea kuirejesha, huku akiwataka waajiri wasimamie mpango huo ili kuwawezesha wahitaji wapya kupata mikopo.

Waziri Mkuu alisema katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetenga Sh786 bilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya kati, ambapo kati ya fedha hizo, Sh731.3 bilioni zitatolewa kama mkopo kwa wanafunzi 220,376 wa shahada ya mbalimbali.

Nyingine ni Sh6.7 bilioni kwa wanafunzi 1,200 wanaofadhiliwa kwa mpango wa Samia Scholarship na kiasi cha Sh48 bilioni kwa wanafunzi wa stashahada zenye uhitaji mkubwa wa rasilimali nchini.