Kampuni za simu zapongeza uamuzi wa Serikali tozo za miamala ya simu

Dar es Salaam.  Watoa huduma za simu nchini, wamepongeza uamuzi wa hivi karibuni wa serikali wa kuangalia upya kodi za miamala ya simu iliyotokana na sheria mpya ya fedha ya mwaka 2021/22, huku wakisisitiza kuwa uamuzi huo utaongeza chachu katika uwekezaji ndani ya sekta hiyo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa chama cha waendesha huduma ya simu za mkononi Tanzania (Tamnoa), Hisham Hendi, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania.
Alisema wateja zaidi ya milioni moja hususani walioko vijijini walisitisha kutumia huduma za miamala ya simu kutokana na ongezeko la makato ambayo alisema yalitishia uhai wa biashara ya simu nchini.
 “Katika siku chache zilizopita tangu sheria ya fedha ilipoanza kutekelezwa Julai 15, mwaka huu, miamala ya wateja ilipungua kwa asilimia 45, jambo ambalo limeathiri mapato ya kampuni za simu na hivyo kupunguza kodi kwa serikali,’’ alisema na kuongeza:
“Tunaishukuru serikali kwa kuona umuhimu na binafsi tunampongeza Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yake kwa kusikiliza kilio cha wananchi.’’
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alifanya kikao na mawaziri pamoja na wadau wa sekta ya mawasiliano kutatua changamoto hiyo ambapo kikao hicho kilikuja na mapendekezo ya kutatua changamoto iliyojitokeza.
Itakumbukwa kuwa Waziri Mkuu aliunda timu ya watu kulifanyia kazi suala hilo na inaelezwa kuwa itakaa hivi karibuni na kampuni za simu na Benki Kuu ili kuangalia mambo yote yanayohusu kodi na kuyatafutia ufumbuzi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha,  Emmanuel Tutuba, timu hiyo inajumuisha mbali na wataalamu kutoka Benki Kuu, pia watakuwapo wa kutoka Mamlaka ya Mwasiliano Tanzania (TCRA), Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Hata hivyo, Hendi alisisitiza kuwa ana imani na matokeo na mapendekezo ambayo yatatolewa na timu hiyo huku akisisitiza kuwa kampuni za simu zitakuwa na uwezo mkubwa kibiashara hapa nchini.
Alisema Tanzania hivi sasa inajivunia ukuaji wa uchumi barani Afrika kutokana na uwekezaji mkubwa wa kampuni za simu.
Kulingana na takwimu za masuala ya mawasiliano zilizotolewa hivi karibuni na taasisi ya masuala ya mawasiliano ya GSMA, kunapokuwa na huduma nafuu za mawasiliano popote duniani, kuna uwezekano mkubwa wa kuboresha sekta mbalimbali hasa ya kilimo na afya.
Juma lililopita, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliueleza umma kwamba Rais Samia amesikiliza kilio cha wananchi na kutoa maelekezo ya namna ya kushughulikia suala hilo.