Kariakoo kwa moto, wafanyabiashara waibua mazito

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Yenga aeleza kuendelea kuacha hali ilivyo sasa Kariakoo ni sawa na kuipeleka ICU.

Dar es Salaam. Unapoingia soko la Kariakoo ni kawaida kukutana na watu kutoka mataifa mbalimbali kila mmoja akizungumza lugha yake akifanya manunuzi na hata wengine wakifanya biashara.

Ni kawaida pia kukuta raia wa kigeni wakiwa katika maduka wakiendelea na shughuli za uuzaji bidhaa mbalimbali, wakati mwingine wakisaidiwa na wazawa.

Baadhi ya raia hao wa kigeni wamekuwa wakifanya shughuli za uchuuzi kama wafanyavyo machinga, jambo ambalo limewaibua wafanyabiashara wakiitaka Serikali iingilie kati kusimamia masharti ya ujio wao nchini.

Wafanyabiashara waliozungumza na Mwananchi wamesema Tanzania inapaswa kunufaika kupitia uwekezaji unaofanywa na raia wa kigeni ikiwemo teknolojia na si raia hao kushindana na wazawa katika shughuli ndogondogo.

Katika eneo la Kariakoo hivi sasa ni kawaida kukuta baadhi ya raia wa kigeni wakiuza vijiko, yeboyebo, ‘kava’ za simu, biashara inayofanywa na wenyeji.


Mtazamo kisheria

Kwa mujibu wa Wakili Dominic Ndunguru, raia wa kigeni anapokuja nchini hutambulika kama mwekezaji au mfanyakazi wa kampuni fulani anayepewa kibali cha kazi na shughuli anazopaswa kuzifanya ni zile ambazo haziwezi kufanywa na raia wa ndani.

Mmoja wa wanasheria waliozungumza na Mwananchi walieleza kawaida kila mgeni anapokuja nchini kwa ajili ya makazi anapopewa kibali na ofisi ya uhamiaji huwa kinakuwa na daraja kulingana na shughuli atakazozifanya, hivyo namna nyepesi ya kushughulika na raia hao wa kigeni ni kuangalia wale ambao wanafanya kazi zilizo kinyume cha vibali vyao.

"Wengine huomba viza ya biashara ambayo inampa nafasi ya kuangalia mwenendo wa soko la bidhaa fulani au kujaribu bidhaa zake sokoni, katika mazingira kama hayo wengi hujikuta wakitumia fursa hiyo kufanya biashara kamili, badala ya kuangalia soko kama walivyokusudia," alisema mwanasheria huyo.

Mwanasheria mwingine, Peter Mukandi alisema kupitia sheria ya kazi, tume ya ajira imeainisha kazi zinazopaswa kufanywa na wageni, huku sheria ya uwekezaji ikimpa fursa mwekezaji kuja na baadhi ya wafanyakazi wake.

Malalamiko ya wafanyabiashara

Akizungumza leo Aprili 5, 2024 kwenye mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara mkoani hapa, Yusuph Yenga alisema soko ni kitu muhimu katika ukuaji wa uchumi na kama Watanzania ni vyema kulilinda soko kama la Kariakoo, ambalo linakuza uchumi wa nchi.

Alisema kuruhusu kuingiliwa soko hilo na watu wa nje wenye teknolojia zilizoendelea na kuwaacha wafanye kazi ndogo za watu wa ndani ni kuua uchumi na si kuukuza.

“Serikali iangalie hili suala la Wachina kufanya biashara ndogondogo, wawekezaji waje kwa ajili ya uwekezaji, waje na uwezo na si kuingilia kazi za watu wa ndani, ambazo Watanzania wanazitumia katika kukuza uchumi wao,” alisema Yenga.

Mfanyabiashara, Riziki Ngaga alisema kwa sasa kumekuwa na wimbi la watu wanaokuja kutoka mataifa mbalimbali, wanaoleta bidhaa kwenye makontena, wakichagua namna ya kuziuza.

Alisema baadhi wamekuwa wakiuza kwa namna ambayo inaweza kuifanya Serikali kupata mapato au kuyakosa.

“Wachunguzwe, haiwezekani Mchina anakuja kufanya biashara ndogo, kiuchumi nchi (Tanzania) inakua na inatarajiwa kurithi teknolojia, mgeni anapokuja kufanya biashara ndogo, Serikali haitengenezi ajira,” alisema Ngaga.

Alisema ni vyema kuwapo kwa mpango wa kutengeneza wafanyabiashara wakubwa ili nchi iweze kufanya biashara kimataifa kwa kuangalia sera na sheria zilizopitwa na wakati, kwani ndiyo zinawafanya wageni badala ya kuwa wawekezaji wanakuwa wachuuzi.

“Tunatarajia wawekeze katika viwanda kufanya miradi mikubwa ya barabara, tunapata wawekezaji ambao wanakuja kufanya biashara za kutandaza bidhaa kama wamachinga,” alisema Ngaga.


Alichosema Mkuu wa Mkoa

Akijibu hoja alipohitimisha baraza hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema Tanzania inapopokea mgeni kuja kuwekeza, kuna sheria zinazomsimamia, na zipo taratibu zinazomruhusu mfanyabiashara wa ndani kutumia fursa ya mwekezaji aweze kufanya biashara zake.

“Malalamiko ni watu wa nje kujihusisha na biashara za kichuuzi ambazo zingeweza kufanywa na wafanyabiashara wa ndani, tumeyapokea na eneo lililotajwa ni Kariakoo,” amesema na kuongeza:

“Tutaenda kuanza msako wa kawaida na kutoa elimu kubwa ili wafanyabiashara wa ndani waweze kujua namna gani wanaweza kunufaika na nchi yao, na wale wafanyabiashara wanaotoka nje kuja kuwekeza waweze kusaidia wafanyabiashara wa ndani kupata mali zinazozalishwa na uwekezaji wao.”

Kwa sababu malalamiko hayo yanahusu wageni, Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania, Paul Mselle amesema Idara ya Uhamiaji huwa inatoa kibali kwa ajili ya kuishi kwa raia wa kigeni ambao tayari wamepatiwa vibali vya kazi na Wizara ya Kazi baada ya kufika nchini.

Kuhusu linalofanywa Kariakoo na raia wa kigeni, amesema ni lazima kuthibitisha juu ya uwepo wake ili wajue kama wanafanya hivyo kihalali, na kujua kwa undani kama kitu hicho kipo au hakipo.

“Wageni wanapokuja kama wafanyakazi nchini huwa wanaombewa vibali vya kazi kupitia sehemu watakazofanyia kazi, sisi tunawapa kibali cha kuishi, huwa pia tunafanya operesheni kuangalia kama kuna wanaokiuka, na wanapobainika huchukuliwa hatua,” amesema Mselle.

Kuhusu raia wa kigeni kufanya uchuuzi badala ya uwekezaji, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri amesema ili mtu atambulike kama mwekezaji anatakiwa kuwa na mtaji wa kuanzia Dola 500,000 za Marekani (Sh1.29 bilioni) na kuendelea na hakuna sheria inayowazuia kufanya biashara za rejareja.


Kariakoo inaenda ICU

Unapokuwa eneo la Kariakoo ni rahisi kusukumwa huku na kule, kupigwa vikumbo jambo linaloweza kukunyima uhuru wa kufanya manunuzi.

Hali hiyo imekuwa kero kwa baadhi ya watu ndani ya eneo hilo, jambo linalowafanya kutafuta namna nyingine ya kupata kile wanachohitaji, ikiwemo kuagiza bidhaa kupitia mtandao.

Kero hiyo si kwa wanunuzi pekee bali hadi kwa wafanyabiashara wanaotaka kuwe na sehemu maalumu ya wamachinga ili soko lipumue.

Wameeleza kuendelea kuacha hali ilivyo sasa ni sawa na kuipeleka Kariakoo chumba cha uangalizi maalumu (ICU).

“Ni vyema kuandaa eneo la kuwaweka wafanyabiashara wadogo ili watu wakitaka kununua vitu vya bei rahisi, vilivyotumika kuwe na soko lake. Wajue watavipata wapi, Kariakoo liwe soko la maduka pekee,” alisema Yenga.

Alisema kwa sasa kuna uwekezaji mkubwa uliofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), zaidi ya nyumba 30 zinavunjwa ili kujenga maduka makubwa, mradi wa DDC unakuja ambao utatengeneza zaidi ya maduka 400.

“Kuna soko jipya la Kariakoo, ukijumlisha na watu waliopo sasa, kwa kila jengo kujengwa kuanzia chini ambako pia kuna maduka katikati itafika hatua hata watu kupita na kwenda kununua vitu haitawezekana,” alisema Yenga na kuongeza:

“Maana yake itazalisha magonjwa, badala ya kukuzwa kiuchumi watu watapata afya mbovu na hawataweza kujenga nchi yao. Dhana ya kusema unakua kiuchumi itakuwa imepotea. Tunaiomba Serikali kupitia baraza hili waweze kuainisha eneo haraka sana kwani Kariakoo iko ICU kwa hivi sasa.”


Majibu ya Chalamila

Mkuu wa Mkoa, Chalamila alisema msongamano uliopo sokoni hapo ndiyo ladha ya soko lenyewe.

“Ladha ya Kariakoo ni ule msongamnao wake, ladha ya biashara kwa sasa ni watu. Zipo biashara unazoweza kuzifanya kwa mtandao lakini kwa Karikaoo ziko tofauti ni ana kwa ana,” alisema Chalamila.

Alisema kutokana na msongamao uliopo wamekubaliana na watu wa sekta nyingine ikiwemo NHC kuendeleza majengo wanayomiliki kwa ubia wa serikali na sekta binafsi (PPP).

Amesema kwa muda mfupi soko la Kariakoo litatanuka zaidi kwa sababu kuna majengo yanayomaliziwa ambayo yatabeba pia wafanyabiashara.

Chalamila akieleza hayo, daktari na mtaalamu wa usalama sehemu za kazi, Godlove Godwin alisema sehemu ambayo ina mkusanyiko wa watu kama Kariakoo ni rahisi kupata magonjwa ya mlipuko iwapo yatatokea.

“Kwa watu wanaiongia na kutoka wanaweza kupata maambukizi ya magonjwa ya ngozi kutokana na mgusano wa watu na inawaweka watu hao pia katika hatari ya kupata magonjwa ya mlipuko ugonjwa wowote utakapotokea,” alisema.

Alisema kwa wanaofanya shughuli zao muda wote sokoni hapo wanakuwa katika hatari sawa na wachuuzi, lakini kupigwa na vumbi wanaweza kupata magonjwa ya mfumo wa upumuaji.

Amesema wakati mwingine magonjwa yanaweza kutokea kutokana na jua kali ikiwa muhusika hanywi maji ya kutosha.

Hali hiyo pia inaweza kuwaweka katika hatari ya kupata ugonjwa wa shinikizo la damu ikiwa hawatazingatia zaidi vitu wanavyopaswa kufanya wanapokuwa eneo hilo.

Mtaalamu wa masuala ya usalama, Paul Justus alisema uwepo wa msongamano mkubwa wa watu huweza kuchochea wizi mdogomdogo ambao watu hawawezi kuubaini kutokana na msongamano.

“Kunakuwa na utapeli wa kiasi kikubwa, kuwapo kwa uwezekano wa kutokea kwa ajili katika barabara ambazo zinapita eneo hapo. Kariakoo ni sehemu kubwa yenye watu wengi imepangwa lakini usalama katika masuala ya moto hayajazingatiwa, wangeweka hata mitambo ya kuzima moto,” alisema.

Alisema pia uwepo wa kamera za CCTV ndani ya eneo, ni suala lenye umuhimu mkubwa katika kudhibiti matukio hayo.