Katiba ilete muundo wa kibunge kutibu Muungano

Thursday April 28 2022
katibapiic
By Luqman Maloto

Hoja ya Katiba mpya inaendelea kuchukua nafasi kubwa. Wapo wanaosema tuanze na tume huru ya uchaguzi, wengine wanasimamia Katiba mpya ni sasa.

Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ziarani Marekani, baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini humo walisimama na mabango hotelini kwake yenye ujumbe unaosisitiza upatikanaji wa Katiba hivi sasa.

Rais Samia alijibu kuwa sauti zao alizisikia. Akawataka wawe na subira kungoja kikosi kazi kimalize kazi yao na suala hilo la Katiba litapatiwa ufumbuzi.

Kwa nini Katiba ilishindikana mwaka 2014? Kila hoja inaweza kuzungumzwa, lakini chanzo kikuu cha mvurugano wa kikatiba na hata kusababisha Katiba Inayopendekezwa idode ni idadi ya Serikali, mengine yote yalikuwa nyongeza na changamsha genge.

Chama cha Mapinduzi (CCM), kupitia viongozi wake, walikula yamini kuhakikisha idadi ya Serikali zinabaki mbili. Wakati huohuo, CCM wakanusa harufu ya uasi ndani yao, kwamba wapo wana-CCM wengi, hususan kutoka Zanzibar waliopigia chapuo Serikali Tatu.

CCM ikataka kudhibiti uasi huo kwa kupitia azimio la kupiga kura ya wazi, kwamba waasi wenye uthubutu wapigie kura Serikali Tatu huku wakionekana. Matarajio yalikuwa kwamba wengi wangepiga kura ya Serikali Mbili kwa sababu za woga.

Advertisement

Huo ndio ukawa mgogoro. Wapinzani walijua hilo ndiyo maana walipingana na agizo la kura za wazi. Hata wana-CCM waliotamani kuuasi uamuzi wa chama chao, hawakukubali kura za wazi kwa sababu waliona wangekosa uhuru wa kuchagua kwa matakwa yao, bali wangepiga kura kwa maslahi ya chama.

Kutokana na mvutano huo na kwa sababu wapinzani walijihesabu ni wachache na kuona wasingeweza kushindana na wana-CCM waliokuwa wengi ndani ya Bunge la Katiba, waliamua kususia vikao, kisha uamuzi huo ukachangia kudoda kwa Katiba Inayopendekezwa.

Sasa tuhoji, kwa nini CCM haitaki Serikali Tatu? Vipi wapinzani na Wazanzibari wengi wanang’ang’ana na Serikali Tatu? Je, kwa nini Wazanzibari ukitaka kuwachokoza uwaambie hadithi ya Serikali Moja? Serikali zikiwa tatu, maana yake inakuwepo ya Tanzania Bara, Zanzibar kisha ya Muungano. Rasimu ya Jaji Joseph Warioba ilieleza kuhusu uwepo wa Marais Watatu, mmoja wa Bara, mwingine Zanzibar halafu anakuwepo wa Muungano.

Kwa nini Wazanzibari waliona Serikali Tatu ni mwafaka kwao kuliko Moja? Ukiwa mfuatiliaji mzuri wa changamoto za Muungano na mijadala yake ni rahisi kupata majibu. Hoja kuu ni mamlaka na siyo vinginevyo.

Wazanzibari hawapendi Serikali moja na wameshakinai Serikali mbili kwa sababu ya mamlaka. Wanaona Serikali moja inaweza kusababisha kufichwa kabisa kwa Zanzibar, upande wa Serikali mbili ndiyo hizo wanaona wanabanwa na Tanzania Bara kiasi kwamba hawapumui.

Kuelekea kukusanya maoni ya Katiba, Zanzibar walikuwa na mchakato wao wa kukusanya maoni, Wazanzibari wakitakiwa kuchagua moja kati ya matatu, (a) Muungano uendelee kama ulivyo (b) Muungano wa Mkataba na (c) Waachwe wapumue.

Pamoja na Wazanzibari wengi kuridhia kwamba muungano uendelee, bado hoja kubwa ilikuwa kwamba manung’uniko juu ya muungano ni mengi, hasa upande wa Zanzibar.

Manung’uniko Bara si mengi kama Zanzibar. Tangu kuzimwa kwa hoja ya wabunge wa kundi la G55, walioibuka na hoja ya kudai Tanganyika miaka ya 1990 kisha kusambaratishwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mtetezi mkuu wa Tanganyika aliyekuwa amebaki ni Mchungaji Christopher Mtikila.

Tangu kifo cha Mtikila mwaka 2015, hayupo mwingine ambaye yupo mstari wa mbele kuidai Tanganyika. Upande wa Zanzibar, hoja ya kudai Zanzibar yenye mamlaka kamili haitarajiwi kukoma hivi karibuni. Ni wazi itaendelea kuwepo mpaka ufumbuzi utakapopatikana.

Hoja ni mamlaka na siyo kingine. Zanzibar wanahitaji kujiongoza wenyewe bila mwangwi wa Tanzania Bara. Na palipo na masuala ya Muungano, ionekane haki sawa kulingana na ushirika wa nchi mbili.

Ilivyo ni kwamba CCM Tanzania Bara wanaona kama kuna kikundi cha watu wa Zanzibar wenye kutaka kuviondoa visiwa hivyo kwenye muungano.

Sasa je, suluhu yake ni nini ili ifikie mahali Watanzania katika pande zote mbili wajione wanaishi kwenye muungano ulio salama kwa wote?

Serikali ya kibunge

Tanzania kwa muundo wa Serikali yake, imeshika mfumo wa nusu-urais (Semi-Presidential System), kwa hiyo kuna Rais ambaye ni Mkuu wa nchi lakini pia ni mkuu wa Serikali na Waziri Mkuu ndiye mtendaji mkuu wa Serikali.

Kwa nchi ambazo Serikali imechukua mfumo wa Kibunge (Parliamentary System) kama Uingereza na Ujerumani, Mkuu wa nchi siyo mkuu wa Serikali.

Ujerumani, Mkuu wa nchi ni Rais, Mkuu wa Serikali ni Kansela. Uingereza, Mkuu wa nchi ni Mfalme au Malkia halafu Mkuu wa Serikali anakuwa Waziri Mkuu.

Mfumo wa Serikali ya kibunge ni mwafaka kwa kumaliza changamoto za Muungano wa Tanzania. Katika Mfumo wa Serikali ya Kibunge, ipo mamlaka ya Mkuu wa nchi, vilevile ya Serikali.

Sasa basi, badala ya kuwa na Serikali tatu ambazo CCM hawazitaki, zibaki mbili. Badala ya kuwa na Serikali moja ambayo Wazanzibari wanaiogopa, ziwe mbili lakini zinazofanya kazi chini ya muundo wa kibunge.

Tanzania iwe na Rais mmoja ambaye ni Mkuu wa nchi ya Jamhuri ya Muungano, halafu Serikali zake ziongozwe na mawaziri wakuu. Waziri Mkuu au Waziri Kiongozi anakuwa Mkuu wa Serikali.

Serikali zinafanya kazi na Bunge kwa ajili ya uongozi wa nchi. Rais anakuwa Mkuu wa Nchi, vilevile Amiri Jeshi Mkuu. Vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinakuwa chini ya ofisi ya Rais. Kwamba Rais ndiye anakuwa nembo ya Muungano, wakati kila upande Serikali yake inafanya kazi kwa namna inavyojiamulia.

Faida zipo mbili; kwanza itaondoa manung’uniko kwani kila Serikali itajiendesha yenyewe kwa uhuru pasipo kuingiliwa na upande wowote. Katika mfumo wa kibunge, Mkuu wa nchi hana mamlaka ya kuingilia Bunge, Serikali wala Mahakama.

Mamlaka ya Mkuu wa nchi kuvunja Bunge inapobidi ni pale anapopewa maelezo kuwa mihimili ya Bunge na Serikali imeshindwa kuelewana au muda wa uhai wake unapofika kikomo. Faida ya pili ni Serikali kutoingilia Bunge na Mahakama. Kwa sasa, Rais ndiye mkuu wa nchi, vilevile mkuu wa Serikali, matokeo yake huonekana Serikali ina nguvu zaidi wakati Serikali, Mahakama na Bunge zinapaswa kuwa mihimili sawa kutokana na mamlaka zake. Hakuna mmoja wenye ruhusa ya kuuingilia mwenzake.

Kwa sasa Rais ambaye ni mkuu wa Serikali, anamteua Jaji Mkuu na majaji wengine, anateua mpaka wabunge, kwa hiyo mkuu wa mhimili mwingine, anateua wajumbe wa mhimili mwingine.

Mfumo wa Semi-Presidential ukiondoka na kushika Parliamentary System, itawezesha kupunguza manung’uniko mengi ya migongano ya kidola.

Zaidi, Parliamentary System ikitumika vizuri, inaweza kuondoa manung’uniko kuhusu Muungano kwa Tanzania kubaki na Mkuu wa Nchi lakini ikawa na wakuu wa Serikali wawili, katika Serikali Mbili za Tanzania Bara na Zanzibar. Serikali Tatu gharama za uendeshaji ni kubwa mno.

Kenya Serikali yao wamechukua mfumo wa Urais (Presidential System) kama Marekani na leo wanajuta kutokana na gharama za uendeshaji wa Serikali kuwa kubwa. Bajeti kubwa inatumika kuhudumia Serikali badala ya wananchi. Tushike Parliamentary System.

Janga ambalo Kenya wamelichuma la kuwa na Serikali kubwa inayomeza mapato mengi ya nchi, ni shule pia kwa wale wenye kupigia chapuo Serikali za Majimbo. Maana ndiyo huo mfumo ambao imeuchukua kutoka Marekani yenye Presidential System.

Nasisitiza, tushike Parliamentary System, tukiwa na mamlaka tatu. Mamlaka ya kwanza ni ya mkuu wa nchi ambaye haongozi Serikali. Mamlaka ya pili ni Serikali ya Tanzania Bara na Waziri Mkuu wake. Mamlaka ya tatu ni Serikali ya Zanzibar na Waziri Kiongozi wake.

Advertisement