Katiba mpya kipaumbele cha kwanza mwaka 2023/24

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akiliomba Bunge liidhinishe Sh383.61 bilioni za bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/2024 leo Jumanne Aprili 25, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Wizara ya Katiba na Sheria imeomba kuidhinishwa Sh383.6 bilioni kwa kwa bajeti ya mwaka 2023/24 yenye vipaumbele 30 lakini kipaumbele cha kwanza ni Kuratibu Mchakato wa Katiba Mpya.


 

Dodoma. Wizara ya Katiba na Sheria imeomba kuidhinishwa Sh383.6 bilioni kwa kwa bajeti ya mwaka 2023/24 yenye vipaumbele 30, ambapo kipaumbele cha kwanza ni kuratibu mchakato wa katiba mpya.

Taarifa hiyo imo kwenye hotuba ya maombi ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2023/24 yaliyoombwa na Wizara ya Katiba na Sheria leo Jumanne April 25, 2023.

Februari mwaka huu Waziri Dk Ndumbaro aliwaambia waandishi wa habari kuwa, Wizara imeongeza bajeti yake kwa Sh9 bilioni ambazo zitakuwa maalumu kwa ajili ya kuanza mchakato wa Katiba mpya.

Waziri wa Katiba na Sheria na katiba Dk Damas Ndumbaro ameainisha vipaumbele hivyo mbele ya bunge akitaja baadhi ya vipaumbele vingine ni kutekeleza mkakati wa kutoa elimu ya Katiba kwa umma, kutekeleza kampeni ya Mama Samia Legal Aid Campaign kwa wananchi kote nchini.

Vipaumbele vingine ni kufanya marekebisho ya Sheria za Uchaguzi na Demokrasia, kuwasilisha taarifa kwenye vikao 16 na majukwaa ya haki za binadamu na watu katika ngazi ya kikanda na kimataifa, kutekeleza programu ya kutumia lugha ya Kiswahili katika utoaji haki nchini na kuwasilisha taarifa tatu (3) za nchi kuhusu Utekelezaji wa Mikataba mitatu ya haki za binadamu ambayo Serikali imeridhia.

Kumekuwa na kilio cha wadau kuhusu madai ya katiba mpya kutoka kwa wanaharakati, wadau na vyama vya siasa nchini wengi wakitaka mchakato huo uanzishwe.

Hata hivyo, Rais Samia Suluhu Hassan na CCM walisharidhia kuhusu kuanzishwa kwa mchakato huo mapema iwezekanavyo wengi wakidai ifanyike kabla ya kuingia kwenye mchakato wa Katiba mpya.