Sheria zinazosimamia uchaguzi zafanyiwa mapitio

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro akiliomba Bunge liidhinishe Sh383.61 bilioni za bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2023/2024 leo Jumanne Aprili 25, 2023 bungeni jijini Dodoma. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Katika kuboresha masuala ya uchaguzi na demokrasia nchini, Serikali imefanya mapitio katika sheria zinazosimamia maeneo hayo, lengo ikiwa ni kubaini changamoto na kuzipatia ufumbuzi.

Dar es Salaam. Tume ya Kurekebisha Sheria imefanya mapitio ya mfumo wa sheria unaosimamia uchaguzi na vyama vya Siasa kwa lengo la kubainisha changamoto mbalimbali zinazokabili michakato ya uchaguzi na uendeshaji wa Vyama vya Siasa nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 25, 2023 na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro wakati akiliomba Bunge kuwaidhinishia Sh383.61 bilioni katika mwaka 2023/2024 kwa wizara hiyo na taasisi zake.

Amesema mapitio hayo yamefanyika ikiwa ni pamoja na kuboresha masuala ya uchaguzi na demokrasia nchini.

“Mapitio hayo yalilenga kubaini endapo mfumo wa sheria uliopo unatoa fursa stahiki kwa wanawake na makundi maalum kushiriki katika masuala ya uongozi na uchaguzi na kubainisha changamoto zinazokabili utaratibu wa upatikanaji wa wabunge na madiwani wanawake wa viti maalum,”amesema.

Amesema tafiti umefanyika kwenye wilaya 39 katika mikoa 17 na kwamba taarifa ya mapitio imekamilika na kuwasilishwa na kuwasilishwa kwake.

Dk Ndumbaro amesema nakala ya taarifa hiyo imewasilishwa katika Ofisi ya Waziri Mkuu na katika taasisi nyingine za umma ili kuendelea kuipitia na kuona namna ya kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.

“Baada ya kuipitia na kuichambua taarifa hiyo, nitaiwasilisha bungeni na kutoa taarifa ya namna Serikali itakavyoyatekeleza mapendekezo aliyotolewa,”amesema Dk Ndumbaro.