Katibu Mkuu NCCR Mageuzi akaliwa kooni

Friday May 13 2022
By Kelvin Matandiko
By Herieth Makwetta

Dar es Salaam. Mgogoro wa NCCR Mageuzi umeendelea kutifuka baada ya Jumuiya ya Wanawake na Mageuzi (Juwama) kulaani kitendo cha Katibu Mkuu wa chama hicho Martha Chiomba kukiuka Katiba inayoelekeza kutumia vikao vya chama kujadili migogoro badala ya kutumia vyombo vya habari. 

Hatua hiyo inakuja ikiwa ni siku moja baada ya Jumuiya ya Vijana wa Mageuzi (Juvima) kulaani kulaani kitendo cha kiongozi huyo kuwasilisha madai yake kwa umma, huku Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia akidai hakuna migogoro yoyote ndani ya chama.

Mei 10, Chiomba alidai kuwepo kwa mkakati wa kumwengua katika nafasi yake, alipozungumza na waandishi wa habari jijini hapa.

Leo Mei 13 Makamu Mwenyekiti wa Juwama, Angelina Mtahiwa alisema jumuiya hiyo haina uhakika na tuhuma alizotoa mbele ya wanahabari siku nne zilizopita, akisema endapo angewasilisha madai yake ndani ya vikao, yakafanyiwa uchunguzi na kuthibitika basi wangesimama upande wake. 

“Mimi (Angelina Mtahiwa) na wanawake wenzangu ndio tuliohakikisha Martha anakuwa katibu mkuu wa chama kama mwanamke kwa hiyo tulitakiwa kusimama naye, kwanza alitakiwa kutumiza majukumu yake badala ya kujificha nyuma ya mwavuli wa jinsia na kufuata taratibu kama ameonewa,” amesema.

Katika ufafanuzi wake, Martha jana alisema mgogoro huo unatakiwa kufikia ukomo na angetamani chama kinarejea kwenye utulivu na msingi wake wa utu huku akisisitiza uwezo wake kiutendaji haujabebwa na kivuli cha usawa wa kijinsia kama iilivyoelezwa na Angelina.

Advertisement

Kwa upande wake Angelina aliyewakilisha kundi la wajumbe zaidi ya 2,000 wa jumuiya hiyo alitoa tamko hilo akiwa ameongozana na Mjumbe wa Sekretarieti ya chama Loyce Giboma na Veronica Kitomari ambaye ni Mjumbe wa Juwama ngazi ya Taifa.

Mwenyekiti wa Juvima, Nicolas Clinton akidai kwamba, Martha angesubiri vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama vitakaa Mei 21, mwaka huu. Nicolas alisema hakuna aliyemlazimisha Martha kujiuzulu wakati Halmashauri Kuu ya Taifa ndio ina mamlaka ya kumuweka madarakani au kumwondoa. 

Wakati hali hiyo ikiendelea jana Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ambye ni mlezi wa vyama jana alisema anasubiri barua ya kushughulikia mgogoro huo endapo watashindwa kuumaliza. “Mie sijapokea barua yao yoyote lakini wajitathmini, wakishindwana basi watakuja kwangu.”
Advertisement