Katibu Mkuu Ujenzi awataka wakazi Magomeni Kota kuzitunza nyumba zao

Saturday January 22 2022
kotaaapic
By Pamela Chilongola

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Wizara ya ujenzi na Uchukuzi, Balozi Aisha Amour amewataka wakazi wa Magomeni Kota watakapokabidhiwa nyumba hizo wazitunze ziweze kudumu ili serikali iendelee kuboresha makazi ya watanzania.

Amour akizungumza hayo leo Januari 22 mwaka huu alipotembelea ujenzi wa nyumba hizo zilizopo eneo la Magomeni, amesema ujenzi wa nyumba hizo zimekamilika kwa asilimia 100.

Amesema wakazi hao wanapopata fursa ya kuingia kwenye nyumba hizo Serikali haitaki kuona ndani ya mwaka mmoja kila kitu kimevurugika huku zikiharibiwa.

"Tunawaomba mtakapokabidhiwa nyumba hizi mjitahidi kuzitunza bahati nzuri miundombinu yote ipo vizuri na yanaweza kutimiza malengo ya wakazi watakaokaa hapa. Wakati wowote mradi huu utafunguliwa na michakato imeshafanyika mingi na wakazi 644 wametambuliwa ni nani ataingia wapi na taratibu zote zinakamilika," amesema Amour.

Amesema kazi kubwa imeshakamilika kwa asilimia 100 kilichobakia taratibu za ujenzi wa marekebisho madog madogo ambayo yanaendelea.

Amour amesema kuna mipango mingine inaendelea kama ya aina ya mradi huo kwa sababu ni mara yao ya kwanza mradi huo kutekelezeka kwa kiwango cha ubora hivyo wakazi hao wasaidie kuitunza miundombinu ya nyumba hizo ili fedha za serikali ziweze kufanya kazi nyingine.

Advertisement

Pia amesema katika mradi huo wamefikiria tatizo kubwa la wamachinga hivyo wamejenga eneo linaloitwa 'Wamachinga Center’ ambalo watafanyia biashara hivyo wameombwa watakaofanya biashara watumie eneo hilo kwa matumizi yaliyopangwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzani (TBA), Daud Kondoro amesema mradi huo umekamilika hivyo wakazi 644 watakaa kwenye nyumba hizo.

"Wakazi wa nyumba 644 wote wataingia kwenye nyumba hizo na tuna maeneo ya uwekezaji ambalo ni Machinga Center ambalo lina vizimba 286, vyoo vya kulipia na uwekezaji wa sakafu juu na chini," amesema Kondoro.


Advertisement