Katibu Tawala awataka maofisa ugani kulinda vifaa vya Serikali

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi Frank Sichalwe akiangalia kifaa cha kupimia Afya ya Udongo (katikati) akiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Charles Fussi (kushoto) pamoja na Afisa Kilimo wa Wilayani hapa Damas Lubuva (kulia) Picha na Mary Sanyiwa
Muktasari:
- Sichalwe awasa maofisa ugani Mufindi kuwa matumizi sahihi ya vifaa vilivyotolewa na Serikali.
Mufindi. Katibu Tawala wa Wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa, Frank Sichalwe amewaasa Maafisa ugani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kutumia vyema vifaa ambavyo vimetolewa na Serikali ili kuweza kuwasaidia wakulima wa wilayani hapa.
Sichalwe ameyasema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya, Dk Linda Salekwa Katika shughuli ya ugawaji wa vitendea kazi kwa maafisa ugani hao iliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo wilayani hapa.
Aidha Sichalwe amesema kuwa maofisa hao wanapaswa kuwaeleza wakulima kuwa huduma ya upimaji wa afya ya udogo itapatika bila malipo yoyote hivyo ni muhimu maafisa hao kuzingatia matumizi sahihi ya kifaa hicho.
"Mkatumie vyema kifaa hiki cha kupimia Afya ya udogo kwa malengo yaliyokusudiwa na badala yake msibadiri matumizi yake kuwa sehemu ya biashara," amesema Sichalwe.
"Wananchi wanatakiwa kufahamu kifaa hicho kipo katika halmashauri yao kwa sababu Rais Samia suluhu Hassan ametoa bure kwa ajili ya kuwasaidia wakulima waweze kupata huduma hiyo," amesema Sichalwe.
Afisa Kilimo wa Wilaya, Damas Lubuva amesema changamoto kubwa ya wakulima walikuwa wanatumia pembejeo kwa kukadiria kiwango kinachohitajika katika mashamba yao hivyo Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imetoa kifaa hicho cha kupimia afya ya udongo katika halmashauri hiyo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima hao.
Lubuva amesema kuwa kutolewa kwa Kifaa hicho kitawasaidia maafisa ugani kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ili kuweza kutimiza malengo ya agenda 10/30 katika halmashauri hiyo.
" Kifaa hicho kitawasaidia maafisa ugani wetu katika kutekeleza majukumu yao kwa sababu ni kifaa cha kisasa ambacho kinatoa sampuli ya udongo na kinatoa majibu hapo hapo ya kiwango cha madini lishe ya mmea yaliyopo na namna ya kurekebisha iwapo kuna mapungufu," amesema afisa huyo.
Pia ametaja vifaa ambavyo vimetolewa kwa maofisa ugani hao kuwa nguo za kujikinga na mvua, mabuti na pampu pamoja na vifaa vya ofisi hiyo ikiwemo kifaa cha kupima afya ya udongo, kompyuta moja, printa na kishikwambi kimoja ili kuwarahisia namna ya ufanyaji wa kazi zao.
Afisa pembejeo wa Halmashauri hiyo, Paulo Hyera amesema kuwa kifaa hicho kitakuwa masaada mkubwa kwa wakulima kuweza kujua kiasi cha mbolea ambacho wataweza kutumia katika mashamba yao.
"Ukishapima afya ya udongo na kujua umepungukiwa kitu gani ni rahisi kwa makulima kufahamu shamba lake anaweza kutumia mifuko mingapi baada ya kupima na kupewa majibu ya udogo wa shamba lake," amesema Afisa huyo.