Kauli ya Dk Malasusa moto kisiasa, yeye ajibu

Mkuu mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Dk Alex Malasusa akizungumza jana Januari 21, 2024 wakati wa ibada maalum ya kumuingiza kazini iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam.

Dar/Moshi. Kauli ya Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa kwamba, hajalelewa kuwa kinyume na Serikali, imewasha moto wa kisiasa na kithiolojia huku baadhi ya wakosoaji wakisema ni ya kuliweka kanisa njiapanda.

Tangu atoe kauli hiyo juzi katika Kanisa Kuu la Azani Front, Dar es Salaam baada ya kuingizwa kazini katika ibada iliyohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na kauli za kumshambulia hasa katika mitandao ya kijamii nchini.

Wengi wanaokosoa kauli hiyo, wanaona kama Askofu Malasusa analiingiza kanisa katika ushirika na Serikali utakaolifanya kanisa likose meno ya kuikosoa pale baadhi ya watendaji watakapokiuka haki za wananchi.

Hata hivyo, alipoulizwa na gazeti hili jana kuhusu kauli hiyo ilivyoleta sintofahamu kwa baadhi ya waumini wa KKKT na Watanzania, Askofu Malasusa alisema inawezekana ambao hawakumwelewa wana uelewa mdogo.

“Labda ni uelewa mdogo wa watu. Kupinga au kuwa kinyume ni nini? Na kupinga sio kukosoa labda ni uelewa mbaya tu kwa watu. Kusema sijazaliwa kuwa kinyume na Serikali sikumaanisha kutoikosoa,”alisema Askofu Malasusa ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

“Kukosoa kutabaki palepale kama itatokea na ndio kazi tuliyonayo.”

Hata hivyo, baadhi ya wakosoaji wametumia kauli yake hiyo kukumbushia waraka wa kitume wa Pasaka wa Baraza la Maaskofu wa KKKT wa Machi 24, 2018 uliotakiwa kusomwa katika sharika zote nchini, lakini haukusomwa katika sharika za dayosisi yake.

Walidai ilifanyika hivyo kutokana na ukaribu ambao Askofu Malasusa alikuwa nao na Serikali, hivyo wanaona kauli yake ya Jumapili inathibitisha kile ambacho waumini walihisi ndicho kiini cha waraka kutosomwa.

Mbunge wa zamani wa Arusha mjini (Chadema), Godbless Lema alikwenda mbali na kudai malezi mazuri ni kuwa kinyume na dhambi na kuwa msitari wa mbele katika kudai haki na usawa, akisema hivyo ndivyo Biblia takatifu inavyotaka.

Hotuba ya Dk Malasusa

Kipande cha hotuba ya Dk Malasusa ambacho kimeibua hisia tofauti huku wengine wakikosoa na kupongeza ni cha dakika mbili tu, lakini mwangwi wake katika mitandao ya kijamii unaonekana kulitikisa kanisa hilo kubwa nchini.

“Hii ndio nchi ambayo waliotangulia walisema nakupenda Tanzania nakupenda, nchi iliyojaa upendo kati ya viongozi wa kitaifa na wananchi wanaoongozwa,” alisema Askofu Malasusa katika sehemu ya hotuba yake mbele ya Rais Samia aliyekuwa mgeni maalumu.

“Uwepo wako wewe kama mgeni rasmi na mgeni maalumu ni kuonyesha pia kwa vitendo ni jinsi gani unatuheshimu sisi kama kanisa, lakini pia Serikali yako inavyoshirikiana kwa karibu sana na madhehebu yote ya dini na taasisi zake”

“Lakini uwepo wako hapa leo (juzi) ni mwendelezo wa Taifa letu kuonyesha ulimwengu kuwa Serikali na dini zinavyoweza kushirikiana kwa upendo amani katika mambo mbalimbali,”alieleza Malasusa.

“Nilipochaguliwa, mmoja wa waumini wangu alitafuta kila namna akanirushia ujumbe akaniambia tunakupongeza askofu lakini tumesikia uko karibu sana na Serikali. Na mimi siwezi nikawa mnyimi wa kusema hilo kwa sababu sijalelewa kuwa kinyume na Serikali.

“Sijalelewa kutokuwa karibu na Serikali lakini kwa kiongozi yeyote hata wewe ambaye hauko serikalini. Hivyo, ukaribu wako ambao umemuonyesha mheshimiwa Rais mimi natamka neno moja tu, Mungu akubariki sana wewe na wasaidizi wako.”


Mjadala ulivyokuwa, wana-KKKT

Mmoja wa maaskofu wa KKKT ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema duniani kote kanisa linalosimama katika haki haliwezi kupendwa na watawala na linalokuwa na urafiki wa moja kwa moja bila kuhoji, lina walakini.

“Ameanza vibaya. Hii kauli sijui kwa nini ameitoa wala hakuwa na haja ya kuisema katika mazingira ya sasa ya kisiasa na kanisa ni la wote. Kiongozi wa kiroho hupaswi kuwa rafiki wala adui wa Serikali, bali unasimama katikati,”alisema.

Muumini wa KKKT na mzee wa kanisa hilo, Amani Ngowi alipoulizwa na Mwananchi amesema, “sisi wana KKKT (askofu) ni kiongozi wetu tumeipokea kauli yake tunaamini yeye na viongozi wengine watafafanua pale ambapo hakueleweka.”

Mchungaji kiongozi wa Dayosisi ya Kaskazini alisema, “kiukweli hii kauli inatusumbua hasa kwa sababu kulikuwa na fununu kuwa ni mtu wa Serikali, kwa hiyo ile role (wajibu) ya kanisa kukemea dhidi ya watawala ndio basi tena.

“Wala asisubiri. Anatakiwa haraka sana aifafanue vinginevyo italigawa sana kanisa. Naamini ameteleza tu katika kuitoa atairekebisha. Sisi tulio na washarika tunai-feel (kuihisi) mioyo ya waumini ilivyoumia,”alisema mchungaji huyo.

“Haikatazwi kushirikiana na Serikali, lakini kauli yake ni kama inapeleka ujumbe kuwa hata Serikali au kiongozi wa Serikali avunje haki za raia hatasimama kukemea kwa sababu hajalelewa hivyo. Ni kauli haijakaa vizuri. Huo ndio ukweli.”

Katika mitandano ya kijamii hasa X zamani Twitter na makundi ya WhatsApp, baadhi ya wachangiaji waliichukulia kauli hiyo haikustahili kutolewa na kiongozi wa kiroho anayetambua hali ambayo Taifa inapitia kwa sasa nchini.

Lema katika ukurasa wake wa X, aliandika “malezi mazuri ni kuwa kinyume na dhambi na kuwa msitari wa mbele katika kudai haki na usawa. Hivi ndivyo Biblia inavyotaka. Yesu alisulubiwa na mamlaka. Rudini Bible school mkajifunze.”

“Na ombeni Roho mtakatifu awasaidie. Hamtaenda mbali kama mtakaa kimya dhidi ya uovu unaotendwa na Serikali huku mkiwa mmesimama madhabahuni mkihubiri amani isiyojali haki,”ameandika Lema.

Katika ukurasa wake wa X, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba aliandika “Hongera sana kwa kuwa mkuu wa KKKT. Hongera kwa maneno yako ya kitaifa kuwa amani haina mbadala.

“Hongera sana mheshimiwa Rais kwa kauli thabiti kuwa yeyote hatavumiliwa kuchezea amani. Nchi (Tanzania) yetu sote.”

Mchangiaji Hanex Muhanuka akaandika kuwa, “kupongezana kwa mema si dhambi bali ni uungwana. Hata hivyo, kumbukeni kuhubiri amani bila kutenda haki ni sawa na kujenga kuta imara juu ya msingi wa tope la udongo.”

Mwanaharakati Martin Maranja Masese ameandika, “kwa kauli hii ya Alex Malasusa, Askofu mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), rasmi sasa kanisa litakuwa mateka chini ya mikono ya Serikali. Poleni sana walutheri.”

Shikilie Shikilie ameandika, “kwa sasa KKKT tuna kiongozi wa dini na sio kiongozi wa kiroho. Hapo ndio kuna tofauti kubwa. Madhehebu wanapaswa kuchagua viongozi wa kiroho kwa sababu ni wa kweli wanasimama katika haki.”


Walichokisema wasomi

Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Dk Faraja Kristomus alisema kauli hiyo inaweza kuwa na athari kwa pande zote mbili.

“Wasiwasi mkubwa ni kuonekana kama dini kuingilia siasa, inaweza kuleta shida, ingawa naiona kuwa na athari hata kwa Serikali kuonyesha taswira ya udini,”

Alisema alipoisikia aliona kuna vitu viwili, kwanza watu kutofautiana kwa kufikisha ujumbe na upande wa pili ni kutafuta kukubalika zaidi kwenye Serikali.

Mchambuzi mwingine wa masuala ya kisiasa kimataifa, Said Msonga alisema kwa nafasi ya Dk Malasusa ambaye ni kiongozi wa dini na kanisa ambalo ni kubwa, anapozungumza sio maoni binafsi.

“Kiongozi kama yeye akisema yale ni maagizo au maelekezo kwa wafuasi wako, ni kama unatoa maelekezo kwa waumini waishi hivyo na hawawezi kwenda kinyume, kama ndivyo kiujumla sasa tuangalie nafasi ya kanisa kwenye jamii ni ipi? Ni kuwasemea wanajamii wale ambao ni waumini wake na hata wasio waumini, Serikali inapofanya vizuri, kanisa kama taasisi litasema, inapokuwa tofauti pia kanisa litasema na kanisa kama mdau wa jamii linaweza kuiambia Serikali, kwenye hili hapana, na kutoa maoni kama kuna makosa basi irekebishe.

“Kama kiongozi kusema hajazaliwa kuwa kinyume nayo, inaleta tafsiri tofauti na inavyotakiwa kuwa,” alisema Msonga.