Askofu Malasusa aingizwa kazini, apewa zigo la changamoto

Rais Samia Suluhu Hassan akimpongeza Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Askofu Alex Malasusa mara baada ya kuingizwa kazini wakati wa Ibada Maalumu iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Azania Front jijini Dar es Salaam leo Jumapili Januari 21, 2024. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) limemsimika na kumuingiza kazini, Dk Alex Malasusa kuwa mkuu wa kanisa hilo, huku akitakiwa kuhakikisha analiongoza kanisa hilo kwa haki na kushughulikia changamoto zilizopo.

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la New Jerusalem India, Dk Christian Samraj amemtaka Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Alex Malasusa kuhakikisha anazishughulikia changamoto mbalimbali zinazoisumbua dunia kwa sasa.

Askofu Samraj ametoa wito huo leo Jumapili, Januari 21, 2024 wakati akihubiri kwenye ibada maalumu ya kumuingiza kazini Askofu Malasusa iliyofanyika kwenye viwanja vya Kanisa Kuu la Azania Front, Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Hafla hiyo ya kumsimika Dk Malasusa ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki, imefuata baada ya Agosti, 25, 2023 mkutano mkuu wa 21 wa KKKT kumchagua kuwa mkuu wa kanisa hilo nchini.

Askofu Samraj amemtaka Dk Malasusa kuwa kiongozi atakayetenda haki na kuhakikisha anazishughulikia changamoto.

“Hata sasa ulimwengu una changamoto na katika hizo, Dk Malasusa umeitwa kukabiliana nazo na kutumia mamlaka ambayo Mungu mwenyewe amekupa. Umetakiwa uzae matunda katika uongozi wako na yadumu milele, ikiwemo wokovu wa watu hata wafikie uzima wa milele,” amesema.

“Katika huduma hii hata kufikia uwezo wa kuzaa matunda, namtaka Dk Malasusa asikilize roho wa Mungu na mamlaka aliyopewa na Yesu Kristo, kwani umepewa na kanisa lako litaendelea kukuombea.”

Katika mahubisi hayo, Askofu Samraj ametoa ujumbe wa neno la Mungu kutoka kitabu cha Yohana 15:16 linalosema “Si ninyi mlionichagua, bali mimi ndiye niliyewachagua ninyi na kuwaweka mwende mkazae matunda na matunda yenu yapate kudumu.”

Askofu Samraj amesema viongozi wa kanisa wameitwa katika huduma hiyo: “Hatukujichagua na Malasusa hajaitwa kwa kujichangua bali amechaguliwa na Mungu na uchaguzi wa Mungu huja kwa haki.”

“Ameitwa katika huduma si kwa kujichagua bali amechaguliwa na Mungu mwenyewe, uchaguzi wa Mungu huja kwa namna ya ajabu tusiyoielewa kama alivyomchagua Mussa kuwatoa wana wa Israel na wengine kuwa wavuvi wa samaki,” amesema.

Akiongoza shughuli ya kumsimika Dk Malasusa, Askofu Fredrick Shoo anayemaliza muda wake, amesema ameliacha kanisa mikononi mwake na anakwenda kutumia dayosisi yake kwa ukaribu.

“Nimemaliza muda wangu, sasa ni muda wangu wa kuitumikia Dayosisi ya Kaskazini kwa ukaribu zaidi. Tulipokuchagua pale Makumira, wewe Dk Malasusa kuwa mkuu mpya wa kanisa utakuwa na jukumu la kutekeleza wajibu kama inavyoonekana katika kanuni ya 12 ya kifungu A ya katiba ya kanisa hili,” amesema Askofu Shoo.

Maaskofu mbalimbali walisogea katika madhabahu na kusoma neno kwa kupokezana kabla Askofu Shoo hajaendelea na kumsimika mkuu mpya wa kanisa hilo.

Ibada hiyo maalumu imehudhuriwa wa viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo, Spika wa Bunge la Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dk Tulia Ackson, Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emannuel Nchimbi, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma, mawaziri na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na makanisa mbalimbali.