Mambo matano yaliyoibuka miaka 60 ya KKKT

Raia Samia Suluhu Hassan akiwa katika picha ya pamoja na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) mara baada ya  kuzungumza nao kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa hilo yaliyofanyika Makumira mkoani Arusha.

Muktasari:

  • Hafla ya maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yameibuka na mambo matano muhimu.

Dar es Salaam. Wakati Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), likiadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwake, mambo matano yameibuka katika hotuba za viongozi kwenye hafla hiyo, likiwemo sakata la mkataba wa uwekezaji bandari.

Mengine yaliyoibuka ni kuchanganya dini na siasa, ustawi wa demokrasia ndani ya vyama, kudumishwa kwa amani na uwekezaji kwa kutegemea sekta binafsi.

Mambo hayo yamezungumzwa na mkuu wa KKKT, Askofu Fredrick Shoo na Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba walizozitoa.

Uwekezaji bandari

Akihutubia hafla hiyo jijini Arusha leo, Jumatatu Agosti 21, 2023, Mkuu wa KKKT, Askofu Frederick Shoo amesifu hatua ya Rais Samia kukaa kimya dhidi ya kauli zinazotolewa kupinga mkataba huo.

Ameeleza ni imani yake kuwa, ukimya huo hauna maana ya kutofanyia kazi kinachopendekezwa, bali inahitajika hekima ya kuliendea jambo hilo na kwamba muafaka utapatikana.

Katika hotuba yake hiyo, Askofu Shoo ameeleza uwepo wa hali inayokaribia kuligawa taifa, wengine wakitumia sababu za kidini, wapo wenye maslahi yao ya kisiasa na yale ya kiuchumi.

“Nashukuru Mungu amekujaalia hekima kama mama na kiongozi umekaa kimya lakini kimya chako hicho sio kwamba hufanyii kazi, mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendelea na sisi tunakuombea kwa Mungu ili heshima yote itumike ili kuliendea jambo hili ili muafaka upatikane,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza juu ya kanisa kuunga mkono uwekezaji, akieleza halipingi hilo na wanatambua nia ya Rais kuhusu uwekezaji.

“Hata hivyo jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi, katika vyombo vya habari, viongozi wa dini, lakini tunatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote kwa uwakilishi tuliomba kuja kukuona pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili.

“Kwa uungwana wako na unyenyekevu na utayari wa kusikiliza ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini, madhehebu yote, tukiwa CCT, TEC na Bakwata mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea, amesema Askofu Shoo.

Baaada ya maoni hayo, Askofu huyo amesema Rais Samia aliahidi kuyapeleka kwa wataalamu na kuyafanyia kazi kwa uzito kwa maslahi ya taifa na kwamba anaamini hilo litafanyika.

“Mheshimiwa Rais kanisa lipo pamoja na wewe, tutaendelea kukuombea na kukuunga mkono katika kulisukuma gurudumu la maendeleo ya nchi kwa maslahi mapana ya nchi,” amesema

Dini na siasa

Hata hivyo, Askofu Shoo amesema kazi ya viongozi wa dini ni kuliombea taifa na pale penye kasoro hawataacha kuwashauri na kama kuna pa kukemea watafanya hivyo.

“Na hapa ndipo naposema, ikifika kwenye hatua hiyo tusiambiwe msichanganye didi na siasa,” amesema.

Demokrasia ndani ya vyama

Katika hotuba yake hiyo, Askofu Shoo amemsifu Rais Samia kwa hatua yake ya kujenga demokrasia ndani ya vyama vya siasa na kuvipa uhuru wa kutoa maoni.

Amesema katika utawala wake, pamoja na kupokea kijiti katika mazingira magumu, lakini amefanya kazi kubwa kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kisiasa.

Amani na utulivu

Amesema ni jukumu la viongozi wa dini kuombea amani na utulivu nchini na kwamba, katika uongozi wa Rais Samia amefanikiwa kuliendeleza hilo.

Jambo lingine liloibuka ni uwekezaji wa kutegemea sekta binafsi, Askofu Shoo amesema KKKT iliwahi kuandika waraka kuhusu jambo hilo.

Ameeleza huo ndiyo msingi wa kuzalisha ajira na kuinua uchumi wa taifa, akisisitiza ni vema kuendelezwa.

Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Samia pamoja na kuahidi kuendelea kuwa kimya kuhusu kauli dhidi ya upinzani wa mkataba wa bandari, amewahakikishia watanzania kutokuwepo yeyote atakayeligawa taifa.

“Niliamua kunyamaza kimya na naendelea kunyamaza kimya, nachotaka kuwahakikishia, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa taifa hili.

Pamoja na ukimya wake, ametoa hakikisho kuwa, hatatokea yeyote mwenye msuli na ubavu wa kuuza taifa, kadhalika kuharibu amani na usalama wa nchi.

“Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza taifa hili, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye taifa hili, sasa hayo itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu,” amesema Rais Samia.