Samia: Hakuna mwenye misuli, mabavu kuligawa Taifa

Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pamoja na Waumini wa Kanisa hilo kwenye maadhimisho ya miaka 60 ya  Kanisa hilo yaliyofanyika Makumira mkoani Arusha.

Muktasari:

  • Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), limesifu hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kukaa kimya kuhusu sakata la bandari.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema aliamua kukaa kimya kuhusu mijadala inayoendelea nchini, akisema hakuna mwenye misuli ya kuligawa Taifa.

 Rais Samia ameyasema hayo leo Agosti 21 katika maadhimisho ya miaka 60 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) yaliyofanyika katika Makumira mkoani Arusha.

 “Ndugu zangu na hasa Baba Askofu Shoo (Frederick) nimeyasikia yote uliyoyasema kuhusu usalama, amani, umoja na muendelezo wa Taifa letu.

“Niliamua kunyamaza kimya na naendelea kunyamaza kimya, nachotaka kuwahakikishia, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuligawa Taifa hili,” amesema Rais.

Pamoja na ukimya wake, ametoa hakikisho kuwa, hatatokea yeyote mwenye msuli na ubavu wa kuuza Taifa, kadhalika kuharibu amani na usalama wa nchi.

 “Hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuuza taifa hili, hakuna mwenye misuli na ubavu wa kuharibu amani na usalama tuliojenga kwenye Taifa hili, sasa hayo itoshe kuwa ni ujumbe wangu kwenu,” amesema Rais Samia.

'Hakuna mwenye misuli, mabavu kuligawa Taifa'

Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Samia, Askofu Shoo amempongeza kwa kuwa kimya dhidi ya kauli kutoka taasisi na wananchi mbalimbali wanaokosoa makubaliano ya uwekezaji wa bandari kati ya Tanzania na Dubai.

“Nashukuru Mungu amekujaalia hekima kama mama na kiongozi umekaa kimya lakini kimya chako hicho sio kwamba hufanyii kazi, mimi nasema jambo hili linahitaji hekima kubwa ya kuliendelea na sisi tunakuombea kwa Mungu ili heshima yote itumike ili kuliendea jambo hili ili muafaka upatikane,” amesema.

Hata hivyo, amesisitiza juu ya kanisa kuunga mkono uwekezaji, akieleza halipingi hilo na wanatambua nia ya Rais kuhusu uwekezaji.

“Hata hivyo, jambo hili limekuwa na maoni mbalimbali ya wananchi, katika vyombo vya habari, viongozi wa dini, lakini tunatambua kwamba sisi viongozi wa dini zote kwa uwakilishi tuliomba kuja kukuona pale mwanzoni kabisa mwa jambo hili.

“Kwa uungwana wako na unyenyekevu na utayari wa kusikiliza ulitupokea na tulikuletea maoni yetu kama taasisi na viongozi wakuu wa dini, madhehebu yote, tukiwa CCT, TEC, Bakwata mimi nakumbuka jinsi ulivyotupokea, amesema Askofu Shoo,” amesema.

Baada ya maoni hayo, Askofu huyo amesema Rais Samia aliahidi kuyapeleka kwa wataalamu na kuyafanyia kazi kwa uzito kwa maslahi ya taifa na kwamba anaamini hilo litafanyika.