Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli ya Jaji Mkuu kwa wanaopeleka changamoto za kisheria kwa Rais

Muktasari:

  • Jaji Mkuu aeleza shughuli zote za Mahakama zinaanzia na zinaishia kwenye masijala.

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema Msajili Mkuu wa Mahakama ndiye injini ya Mahakama, hivyo wenye changamoto za kisheria wazipeleke kwake na si kwa Rais.

 “Nitumie fursa hii kuwaomba wale wanaopeleka changamoto za kisheria kwa Rais, wazipeleke kwa Msajili Mkuu wa Mahakama, huyu ndiye anashikilia injini ya Mahakama na anajua wapi inapoelekea,” amesema.

Profesa Juma amesema hayo leo Aprili 4, 2024 Ikulu, Dar es Salaam, wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipowaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.

Jana Jumatano, Aprili 3, 2024 Rais Samia alimteua Eva Nkya kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, kabla ya uteuzi huo alikuwa mkurugenzi wa kitengo cha huduma za sheria, Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Rais Samia pia alimteua Chinganga Tengwa kuwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita.

“Kwa hiyo leo umetupa watu ambao wana umuhimu mkubwa kwa sababu shughuli zote za Mahakama zinaanzia na zinaishia kwenye masijala,” amesema Profesa Juma.

Amesema Mahakama itawapa ushirikiano wa hali ya juu, akimshukuru Rais kwa kuwaongezea nguvu kwa kuwapa watendaji.

“Niwaombe walioteuliwa tumieni imani hiyo mliyopewa kwa kuhakikisha mnatenda haki na wananchi wawe na urahisi wa kufika kwenye masijala zetu,” amesema.

Amesema Ofisi ya Msajili wa Mahakama ni kiungo, yeye ndiye anaunganisha Bunge, Mahakama na Serikali.

Mwingine aliyeapishwa ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Sylvester Kainda, ambaye kabla ya uteuzi huo, alikuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani na pia Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.