Kauli ya Serikali miili ya raia wa kigeni ajali ya Arusha
Miili ya waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Youth with a mission (YWAM), ikiwa katika ukumbi wa Shule ya New Vision, wilayani Arumeru leo, Februari 28, 2024. Picha na Janeth Mushi
Muktasari:
- Miili tisa bado haijasafirishwa, Uhamiaji yaendelea kukamilisha utaratibu wa vibali.
Arumeru. Serikali imesema inasaidia maandalizi ya kusafirisha miili ya raia wa kigeni waliofariki dunia katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari manne, iliyotokea mkoani Arusha.
Ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 25 wakiwamo raia 10 wa kigeni, ilitokea Februari 24, 2024 eneo la Kibaoni (Ngaramtoni), wilayani Arumeru.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emanuela Kaganda, amesema hayo leo, Februari 28, 2024 alipoongoza waombolezaji kuaga miili miwili ya waliokuwa wafanyakazi wa Shirika la Youth with a Mission (YWAM).
Ibada na shughuli ya kuaga miili hiyo ilifanyika katika shule ya mchepuo wa kiingereza ya New Vision iliyo chini ya shirika hilo.
Walioagwa katika ibada hiyo ni aliyekuwa Mkurugenzi wa YWAM Arusha, John Mukolwe (55), raia wa Kenya na Vincent Kazungu (36), aliyekuwa msaidizi wake, raia wa Tanzania.
Akiwasilisha rambirambi, mkuu wa wilaya amesema kwa sasa wameanza na suala la vibali linalotelelezwa na Uhamiaji, ili kukamilisha taratibu za kuwasafirisha raia hao wa kigeni.
"Tunajua hili ni pigo kubwa ambalo shirika limepata, tunajua kwa sababu wote mna imani na mnamwamini Mungu. Serikali tutaendelea kusaidia maandalizi ya miili itakayosafirishwa kwenda nje ya nchi," amesema na kuongeza:
"Tumeanza na vibali, wenzetu wa Uhamiaji wanafanyia kazi, kwa hiyo popote mtakapopata changamoto msisite, tuko tayari kuhakikisha hili linafanyika bila kuchelewa na kukwama mahali popote, ili kazi ya kuwasifirisha wenzetu nchini kwao ifanyike bila kukwama," amesema.
Amewashukuru wananchi na hasa wa Ngaramtoni ambao siku ya ajali walifanya kazi kubwa kusaidia majeruhi kabla Serikali haijafika eneo hilo.
Askofu wa Kanisa la TAG Galilaya, Solomon Mwagisa amesema kanisa limepoteza viongozi muhimu waliokuwa na mchango mkubwa kwa jamii.
Mkurugenzi wa YWAM Tanzania, Jeremiah Kiwinda ambaye ni mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo nchini, amesema shirika limepoteza watu 12 akiwamo dereva wa gari la shule ambaye amezikwa jana, Februari 27, 2024.
Amesema miili ya raia wa kigeni imebaki tisa baada ya wa Mukolwe kuagwa leo.
"Ni wakati mgumu, lakini kwa maombi yenu yametusaidia sana na tunashukuru Serikali kwa kuungana nasi katika kipindi hiki na kusaidia kila familia iliyopoteza mtu wake hadi raia wa kigeni," amesema.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Kazungu, kaka mkubwa wa familia hiyo, Dk January Kazungu, amesema wanatarajia kusafirisha mwili huo leo kwa ajili ya maziko kesho, Februari 29, 2024 mkoani Mwanza.
"Ilikuwa kwenye 'social media' tumeona ajali kubwa sana tukafikiri haituhusu, usiku nikapigiwa simu kwamba mdogo wetu amefariki, nikalazimika kutoka Dodoma kuanza safari kuja Arusha. Tunatoa shukrani kwa jumuiya na Serikali kwa ujumla," amesema.
Mke wa aliyekuwa Mkurugenzi wa YWAM Arusha, John Mukolwe,Yasinta Mukolwe akisaidiwa kuingia katika ukumbi wa Shule ya New Vision ambapo mwili wa mumewe ulikuwa unaagwa kabla ya kusafirishwa kupelekwa nchini Kenya kesho kwa maziko yanayotarajiwa kufanyika Machi 9,2024 nchini humo. Picha na Janeth Mushi
Mchungaji Joseph Mukolwe ambaye ni mdogo wa Mukolwe, amesema wanashukuru Serikali ya Tanzania kwa kutoa mkono wa pole na kulipa gharama za hospitali.
Amesema wanatarajia kusafirisha mwili huo kuelekea Kenya kesho na wanatarajia kumzika Machi 9, 2024.
"Leo Februari 28, 2024 ilikuwa ni kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa unaweza kuona jinsi ambavyo ni ngumu kwetu. Kaka ameniachia majukumu makubwa, ikiwemo watoto yatima na wajane waliokuwa wakimtegemea kule Kenya na hapa Tanzania, mama anaumwa," amesema.
Mwakilishi wa ubalozi mdogo wa Kenya nchini, Nancy Sifa amesema wamepokea habari za msiba huo kwa huzuni kubwa, na kwa niaba ya ubalozi wanaungana na Watanzania kuomboleza msiba huo mkubwa.