Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kauli za Jaji Mkuu, Mwabukusi na AG kwa mawakili wapya

Sehemu ya Mawakili wapya wakitoa heshima kwa Jaji Mkuu (hayupo kwenye picha).

Muktasari:

  • Weledi, ujasiri na uaminifu vyatajwa kuwa nguzo kwa wakili.

Dar es Salaam. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema moja ya nguzo muhimu za weledi wa wakili ni kufanya kazi zake kwa uhuru na kukataa mashinikizo.

Amesema hayo leo Alhamisi, Desemba 12, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwakubali na kuwapokea mawakili wapya wa kujitegemea.

Profesa Juma amesema uhuru wa wakili ni pamoja na kusimama upande wa sheria inavyotaka hata pale mteja wake atakuwa tayari kumlipa zaidi ili kuivunja.

“Kwa mfano, wakili unashinikizwa na mteja wako kutayarisha mikataba miwili ya mauzo ya ardhi, mkataba mmoja umeonyesha thamani ndogo ili kukwepa kodi na mkataba wa pili ndiyo unaonyesha kiasi halisi cha fedha mnunuzi aliyomlipa muuzaji,” amesema.

Akitoa mfano wa jengo la ghorofa lililoporomoka Novemba 16, 2024 katika mtaa wa Mchikichi na Congo, eneo la Kariakoo na kuua watu 31, amesema licha ya ripoti ya uchunguzi wa chanzo cha kuanguka kwake bado inasubiriwa lakini kuna mambo mengi ya weledi na uadilifu ambayo yalikosekana ndiyo maana likaporomoka.

“Jengo lile halikuporomoka kwa amri ya Mungu. Sasa sisi ambao ni wanataaluma wanasheria, wahandisi tulishiriki kwa namna moja au nyingine.

“Ukiona jengo linaporomoka ambalo siyo act of God (amri ya Mungu) sisi wanataaluma tunatakiwa kujiangalia. Je tumefanya kazi zetu kiuadilifu, kiuweledi, kwa kutumia uwezo wetu wa hali ya juu?” amehoji.

Profesa Juma amesema nguzo nyingine muhimu ya wakili mwenye weledi ni uaminifu, kuaminika na ujasiri.

“Wakili mwenye weledi husimama upande wa haki na kumtetea mteja mahakamani hata pale huyo mteja wake ametenda uhalifu mkubwa kiasi cha kuchukiwa na jamii kwa vitendo vyake vilivyomfikisha katika vyombo vya kisheria au mahakamani,” amesema na kuongeza:

“Hapa wakili mwenye weledi ataendelea na utetezi bila kujali shinikizo kutoka kwa watu wengine, kutoka kwenye vyombo vya habari au shinikizo kutoka katika mitandao ya kijamii.”

Akizungumzia mawakili wanaokiuka maadili, amesema atamuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali amuagize Mwandishi wa Sheria wa Bunge zitafsiriwe kwa Kiswahili Kanuni za Maadili, Weledi, Nidhamu na Tabia Njema za Mawakili za TLS (Chama cha Wanasheria wa Tanganyika).

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwawezesha wananchi wakizisoma wawe katika nafasi ya kuwapima na kuwatathmini mawakili ili wajue kama wamefikia madaraja ya weledi na uadilifu.

Rais wa TLS, Boniface Mwabukusi amewataka mawakili kutokuwa waoga, akisema wamepokea jukumu kubwa katika mnyororo wa utoaji haki nchini.

Amesema taalumu ya sheria ni jukumu takatifu na ni wito wa kuhudumia, kulinda utawala wa sheria, kuhakikisha haki na uhuru wa kila mmoja na utawala bora unaozingatia misingi ya demokrasia, sheria na Katiba katika nchi.

Amesema ni kazi yenye majukumu ya kuhudumia umma katika mazingira yote, mazuri na mabaya, salama na hatarishi katika misingi ya kisheria bila woga wala hofu.

Mwabukusi amesema wanabeba imani ya jamii kuwa walinzi wa usawa, uadilifu na ukweli.

Amewataka kutumia nguvu, ujuzi na muda wa kutosha wa taaluma yao kuleta tija kwa Taifa katika maeneo ya kiuchumi, ulinzi wa rasilimali asili za Taifa na uhuru wa mihimili ya Bunge, Mahakama na Serikali ili kuwa na mfumo thabiti wa kuwajibishana utakaolinda Katiba na sheria.

“Mawakili tuna nafasi ya kupiga kelele kwa sababu hiyo mihimili isipokuwa stable (imara) na kufanya kazi yake, hata kazi yako haina maana. Hakuna atakayekuamini kukuletea kazi, watu wataanza kwenda kupiga ramli.

“Wote tupige kelele Mahakama iwe huru ipate bajeti yake ya kutosha, ifanye kazi yake bila kuingiliwa, mahakimu na majaji walipwe sawasawa, renumiration order (ujira) ya mawakili iboreshwe kwa sababu mtu mwenye njaa hata nguvu ya kubweka hakuna,” amesema na Kuongeza:

“Kwa hiyo tuhakikishe kwamba kila sehemu kipato na wajibu vinaendana, lakini tukihakikisha kuwa tunalinda intergrity (uadilifu) wa mihimili yetu, Bunge na Mahakama ifanye kazi yake kama Mahakama. Kunapokuwa na mwingiliano usiofaa tukemee siyo uasi. Kemea bila hofu ili mradi unajua ni misingi gani haijazingatiwa.”

Pia amewataka kuheshimu mahakama na maamuzi yake hata kama ni mabaya au mazuri na kwamba, kama hawajaridhika wanapaswa kufuata utaratibu wa kukata rufaa au kulalamika kwa mujibu wa taratibu kama ni jambo la kiutawala.

Mwabukusi amewaasa kuzingatia thamani ya huduma ya kutoa msaada wa kisheria kwa kuwa kuna watu wengi katika jamii ambao hawapati na hawana uwezo wa kupata huduma za kisheria na haki.

“Tusisahau jukumu letu la kuinua na kusaidia wasiojiweza. Nawaasa kuhakikisha mnatimiza wajibu wenu kwa jamii kwa kutoa msaada wa kisheria kwa wale wasio na uwezo wa kumudu gharama za kisheria,” amesema.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari amesema mawakili watasaidia kuondoa changamoto mbalimbali za kisheria.

Amesema ofisi yake itakuwa bega kwa bega kutekeleza azma ya Serikali kuhakikisha mfumo wa haki jinai na haki madai nchini unaboreshwa.

Johari amesema mawakili ni wahusika muhimu katika kudumisha ustawi wa sheria na kama watatekeleza majukumu yao ipasavyo hakuna nafasi ya kufanya maamuzi yanayokiuka haki za binadamu au matumizi mabaya ya mamlaka.

Amesema kila hatua wanayochukua inapaswa kuzingatia haki, uwazi na usawa.

Kwa mujibu wa Johari, mawakili ni kiungo muhimu kati ya Mahakama na wananchi katika kuchambua na kutekeleza haki.

Amesema wakiwa maofisa wa mahakama wanapaswa kuhakikisha wanaisaidia kutekeleza jukumu lake kwa kutoa tafsiri sahihi ya sheria.

“Ninyi ni walinzi wa haki, wawakilishi wa uadilifu na watetezi wa sheria. Mambo muhimu ambayo ni lazima myazingatie ni uadilifu, mkiyazingatia malalamiko ya wananchi yatapungua,” amesema.

Amewataka kushiriki kampeni ya utoaji msaada wa sheria kwa wananchi ili kuwasaidia kupata haki zao na kupunguza malalamimo yao kwa Serikali.

Amewasihi kuwa na nidhamu ndani ya Mahakama na katika jamii na kuzingatia kanuni za maadili ya wanasheria akieleza kwa mamlaka aliyopewa ataendelea kudhibiti nidhamu ya mawakili ili kuhakikisha wanaozalishwa ni wenye nidhamu na weledi.

Hata hivyo, amewataka wasiogope kufanya vitendo wanavyoamini ni sahihi wanapotekeleza majukumu yao ya uwakili.