Kaya 130 za Tasaf zapata ajira ya muda Sengerema

Muktasari:
Kaya 130 za walengwa wa Tasaf Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza zimeanza kunufaika na ajira za muda zitakazo waongezea kipato cha Sh3, 000 kwa siku.
Sengerema. Mpango wa kunusuru kaya masikini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) umeanza matengezo ya barabara ya Beipoa Makonge iliyopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza yenye urefu wa kiliometa 2.8 utakaogharimu Sh64.9 milioni
Matengenezo ya barabara hiyo iliyopo Kata ya Nyatukala yanafanywa na walengwa wa Tasaf wilayani humo wenye miaka kati ya 18 hadi 60 ikiwa ni kutekeleza mradi wa ajira za muda kwa walengwa wake 130 watakaolipwa Sh3, 000 kwa siku.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 14, 2023 wakati wa matengenezo ya barabara hiyo, Mratibu wa Tasaf Wilaya ya Sengerema, Malisa Nduga amesema mradi huo ni sehemu ya walengwa kujiongezea kipato ambapo watu wanaotakiwa kufanya kazi hizo ni wale wanaotoka kwenye kaya maskini pekee.
Malisa amesema matengezeo ya barabara hiyo yanatarajiwa kukamilika Mei, 30 mwaka huu ili wananchi waweze kuitumia.
“Kumalizika kwa matengenezo ya barabara hiyo kutafungua fursa za kiuchumi kwa wananchi kupitisha mazao yao kupeleka sokoni bila buguza yoyote tofauti na sasa wanalazimika kutoka Kijiji cha Butonga kwenda sokoni mjini Sengerema wanatumia kilomita sita kuzungukia barabara ya lami,” amesema Malisa
Mmoja wa wanufaika wa Tasaf wilayani humo, Cesilia Bwiti amesema licha ya kunufaika kwa kujiongezea kipato kwa kutengeneza barabara hiyo kwa jembe la mkono, kumalizika kwa barabara hiyo kutafungua fursa ya biashara kwa wananchi wa maeneo hayo wanaojihusisha na masuala ya kilimo.
“Tunashukuru Serikali kwa kutuona na kutupatia mradi wa kutuongezea kipato. Tunaufanya kwa ufanisi mkubwa,”amesema Bwiti
Kwa upande wake muwakilishi wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) wilayani humo, Fraza Simoni amesema wamepitia barabara yote na kutoa ushauri juu ya matengenezo yake lengo ni kuhakikisha matengezo hayo yanafanyika kwa ubora unaotakiwa.