Kazi ya Museveni, kauli ya Mkapa kuhusu Chato
Muktasari:
- Katika hii sehemu ya sita ya mapitio ya kitabu 'I am the State, leo tunaangazia alichofanya Museveni akiwa Chato, alichosema Mkapa kuhusu eneo hilo na kuyeyuka Chuo Kikuu Chato.
Waandishi katika sura hii wanajadili kwa ufupi jinsi baadhi ya huduma za kijamii zilivyokuwa kivutio au kikwazo kwa watu wa ndani na nje ya nchi, hasa jinsi baadhi ya maeneo ndani ya Wilaya ya Chato yalivyopewa upendeleo kuliko mengine. Ni hadithi ya mji unaokua kwa kasi, mipango, ujenzi wa haraka, ujanja, uharibifu na kutelekezwa.
Miradi iliyojadiliwa ni kiwakilishi tu cha mingine mingi ya mfano huo.
Waandishi hao wakongwe—Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu—wanazidi kuangazia upendeleo wa aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kwa Chato alikozaliwa.
Mojawapo ya mradi unaoguswa katika sura hiyo ya tano ni ujenzi wa Chuo Kikuu cha Chato ambao umenyauka baada ya kwa kifo cha Rais Magufuli.
Chuo hicho kilisababisha hata kubadishwa kwa jina la Mtaa wa Mpogoroni katika Kijiji cha Kasagara Kata ya Bwina na sasa unajulikana kama Chuo Kikuu Street ambao unakupeleka kwenye eneo la chuo kikuu kiteule cha Chato, kilichopo takriban kilomita mbili kutoka mji mdogo wa Chato, unapoelekea Ziwa Victoria upande wa kulia, ukipita Hospitali ya Rufaa ya Chato. Ni mtaa mmoja na wenye shule inayoitwa Janeth Magufuli Girls Secondary School.
Kabla ya mradi huu wa chuo kikuu, kinaeleza kitabu hicho, yalikuwepo majengo na viwanja kadhaa vya makazi ya wakazi wa Kasagara.
Kitabu hicho kinamnukuu Mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani akisema eneo hilo lina ukubwa wa hekta tano na kuwa tayari Serikali ilishatoa Sh8.9 bilioni za fidia kwa wakazi waliolazimika kutoa maeneo yao.
Agosti 2019, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel alitoa wazo la kuwa na chuo kikuu Chato ili kuamsha ari ya elimu katika mkoa wake kwa msingi kwamba ulikuwa nyuma kwa muda mrefu. Lakini kilichoshangaza ni pendekezo lake la mradi huo kufanyika katika Wilaya ya Chato, na chuo hicho kipewe jina la Chato na si Mkoa wa Geita.
Kitabu kinaandika kuwa kama ilivyotarajiwa, pendekezo hilo liliungwa mkono na Naibu Waziri wa Elimu, William Elinasha, ambaye alikuwa katika ziara ya mkoa kukagua miradi ya elimu mkoani Geita.
Naibu Waziri alizishauri mamlaka za mkoa wa Geita ziendelee na taratibu za manunuzi ya ardhi kwa ajili ya mradi huo na aliahidi wizara kushughulikia suala hilo haraka. Miezi miwili baadaye, Oktoba 2, 2019, Dk Kalemani alithibitisha kuwa Serikali tayari imeshatenga maeneo kwa ajili ya chuo hicho.
Ujenzi wa Chuo Kikuu ulikuwa umeanza, lakini ghafla ukayeyuka baada ya kufariki kwa Rais Magufuli Machi 17, 2021. Tumaini lililokuwako mwanzo likatoweka.
Waandishi wa kitabu hicho wanasema timu yao ya uchunguzi ilipotembelea eneo la ujenzi huko Kasagara Novemba 2022, walichokikuta ni cha kuvunja moyo. Hakuna ujenzi uliokuwa ukifanyika na jengo lilionekana kutelekezwa.
Baadhi ya vifaa vya ujenzi pia vilitelekezwa kwenye eneo hilo huku vingine, kwa mujibu wa majirani wa eneo hilo, viliripotiwa "kuondolewa" na maofisa wa Serikali.
Kulingana na kile waandishi wanakiita “upekuzi wetu”, Chuo Kikuu cha Chato hakionekani popote kwenye mfumo wa elimu. Wameandika kuwa “inaonekana ujenzi wake ungeanza sawa na ujenzi wa Uwanja wa ndege wa Chato bila kufuata taratibu za Serikali na bila hati.”
Mradi mwingine uliotajwa na kitabu hicho ni Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM). Huo ni mradi mwingine wa Dk Magufuli ulioanzishwa Chato na ulitakiwa kukamilika Februari mwaka huu. Wanasema kuwa angalau chuo hiki kilipewa jina la Geita, lakini kilikuwa katika Kijiji cha Rubambangwe, wilayani Chato.
Ukiacha miradi mingi iliyoelekezwa Chato iliyotajwa na kitabu hicho, kuna Shule ya Awali na Msingi ya Museveni. Rais Magufuli aliwaalika viongozi wengi wa kigeni kwenda Chato, lakini mmoja wao aliacha alama isiyofutika.
Huyo ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda. Alijitolea kufadhili na kujenga shule ya msingi ili kuunga mkono azma ya Magufuli ya kuendeleza mahali alipozaliwa. Kazi hiyo ilianza Februari 11, 2020 na Novemba 29, 2021 Museveni alikabidhi shule hiyo kwa Rais Samia katika hafla iliyofanyika Kijiji cha Nyabirezi, Chato.
Shule hiyo ikaitwa Museveni Pre & Primary School ambayo inaanzia chekechea hadi darasa la saba.
Katika kitabu hicho imetajwa pia “miradi ya maji ya kimkakati Chato” kikieleza kinaganaga na kwa uchambuzi kiasi cha fedha zilizotumika katika miradi hiyo ya maji na kwa njia ambayo waandishi wanaona ni upendeleo kwa Chato.
Chato ilianza kupata maendeleo ya haraka kiasi kwamba mbunge wa eneo hilo, Dk Kalemani, katika hafla moja mjini humo ambayo pia Rais Magufuli alihudhuria, alisema:
“Miaka kumi iliyopita Chato haikuwa hivi, tangu uwe Rais umefanya maajabu Chato, kumekuwa na mabadiliko makubwa... barabara nzuri, shule kubwa, majengo ya mahakama yenye hadhi ambayo pia ulizindua leo... asante! Sisi watu wa Chato tunakutakia afya njema na maisha marefu."
Maendeleo ya Chato yalikwenda kasi sana kiasi kwamba, kulingana na kitabu hicho, Rais Mstaafu Benjamin Mkapa alipofika Chato kuhudhuria maziko ya dada yake Rais Magufuli, Monica, Agosti 2018, alielezwa kushangazwa na jinsi Chato ilivyokuwa ghafla kuwa mji wa kisasa katika muda mfupi.
Kkitabu kinasema Mkapa alipoona makazi mapya ya kifahari ya Rais Magufuli, alimnong'oneza msaidizi wake akisema, "Sikujua Ikulu kuna utajiri."
Kitabu hicho kinahitimisha sura ya tano kikisema “kwa wale waliomsikia (Mkapa) na kuelewa alichomaanisha; ujumbe mzito unaomhusisha Rais Magufuli na ufisadi na matumizi mabaya ya madaraka ulikuwa umetumwa.”
Kesho tutafanya mapitio ya sura ya sita na ya mwisho ya kitabu tukiangalia jinsai ndoto ya kukuza utalii Chato ilivyofifia.