Kero urasimishaji ardhi Dar kupatiwa ufumbuzi

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa
Muktasari:
- Siku saba zimepangwa kumaliza Suluhu ya changamoto ya urasimishaji ardhi katika Jiji la Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Siku saba, zinatarajiwa kutoa jawabu la changamoto ya migogoro ya ardhi katika Jiji la Dar es Salaam, baada ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jerry Silaa kuahidi kutumia siku hizo kutekeleza hayo.
Utekelezaji huo, Silaa ameahidi kuufanya kwa kushirikiana na watumishi wengine wa Wizara hiyo, akiwaagiza wasifanye kazi nyingine kwa kipindi hicho zaidi ya kusaka suluhu ya migogoro ya ardhi Dar es Salaam.
Chimbuko la ahadi hiyo ni kukithiri kwa malalamiko ya migogoro ya ardhi katika Jiji hilo, yaliyoibuliwa na Mwenyekiti wa CCM Dar es Salaam, Abbas Mtemvu.
"Dar es Salaam ina Kata 102, tumetembelea Kata 80 kwa sehemu kubwa malalamiko yalikuwa ni migogoro ya ardhi na ndiyo sababu tumekuita (Silaa)," amesema.
Silaa ametoa ahadi hiyo jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 4, 2023 alipozungumza na viongozi wa CCM wa Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika maelezo yake, Silaa amemtaka Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Lucy Kabyemela pamoja na watendaji wengine kuanza kufanyia kazi migogoro hiyo.
Amekiri ukubwa wa kero hasa ya urasimishaji katika Jiji la Dar es Salaam na kwamba siku saba zinatosha kuja na jawabu lake.
"Kama kuna kampuni zimefanya vibaya tupate taarifa kwa ajili ya hatua na kwa kuwa haha tumeyazungumza hadharani basi wakati wa kutoa taarifa baada ya siku saba, tutatoboa hadharani," amesema.
Ameongeza kwa maeneo yatakayohitaji fedha, watendaji wanapaswa kuyabainisha ili ziombwe au kutafuta namna ya kujibana ndani ya wizara ili zipatikane.
Kuhusu kero ya urasimishaji, amesema kati ya simu 10 anazopokea saba zinalenga eneo hilo.
Amesema linalenga kusogeza karibu huduma za ardhi na wananchi kwa kuwa kumekuwa na mahitaji yasiyoendana na idadi ya watumishi
Mathalan, kwenye utoaji hati amesema kwa mwaka ofisi zilizopo Dar es Salaam zina uwezo wa kutoa 16,000 kwa mwaka, lakini ni chini ya zinazohitajika ingawa hakuzibainisha.
Awali, akifungua mkutano huo, Mtemvu amesema wingi wa migogoro ya ardhi katika Jiji hilo, ndiyo sababu ya kuitwa kwa waziri huyo.
Hata hivyo, amesema migogoro yote inayohusiana na CCM, itawasilishwa kwa Katibu Mkuu, Daniel Chongolo atakayewasiliana moja kwa moja na Silaa.
Kero za ardhi katika mkutano huo, ziliibuliwa pia na Mbunge wa Segerea, Bonna Kamoli aliyesema wapo warasimishaji waliochukua fedha za wananchi na kutoweka bila kutekeleza kazi.