Kero ya wafanyabiashara Zanzibar kutozwa kodi mara mbili yaondolewa

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akiwasilisha bungeni Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024, jijini Dodoma Juni 15, 2023. Picha na Edwin Mjwahuzi
Muktasari:
- Serikali yasema hoja nne kati ya nane ambazo ni kero za Muungano zimepatiwa ufumbuzi ikiwemo ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.
Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imezipatia ufumbuzi hoja nne za Muungano ikiwemo ya malalamiko ya wafanyabiashara wa Zanzibar kutozwa kodi mara mbili.
Dk Nchemba amezitaja kodi hizo ni pamoja na Kodi ya mapato kadri unavyopata na kodi ya zuio mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Karume (Terminal III).
"Pia ongezeko la gharama za umeme kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwenda Shirika la Umeme la Zanzibar (Zeco)," ameeleza Dk Mwigulu
Waziri huyo ameeleza hayo leo Alhamisi Juni 15, 2023 wakati akiwasilisha bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/23 akisisitiza Serikali inatambua Muungano ni Tunu ya Taifa letu na ndio utambulisho Tanzania duniani.
"Hivyo ni jukumu letu sote kuulinda, kuudumisha na kuuenzi.Katika kuendelea kudumisha Muungano, Serikali imekuwa ikifanya vikao mbalimbali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa hoja za Muungano,"amesema.
Ameongeza kuwa katika mwaka 2022/23, Serikali ilijadili hoja nane za Muungano ambapo nne zilipatiwa ufumbuzi na kuondolewa katika orodha ya hoja za Muungano.