Kesi mauaji ya Alphonce Mawazo wa Chadema yahamia Mahakama Kuu

Muktasari:
Washtakiwa watano wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo wamefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza leo Jumatano Agosti 28, 2019
Geita. Washtakiwa watano wa kesi ya mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Geita, Alphonce Mawazo wamefikishwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza leo Jumatano Agosti 28, 2019.
Leo ni mara ya kwanza kwa kesi hiyo kusikilizwa mahakama kuu baada ya kuhamishwa kutoka mahakama ya hakimu mkazi Geita ambayo haina sifa ya kusikiliza kesi ya mauaji.
Katika kesi hiyo namba 8 ya mwaka 2019 iliyosikilizwa katika mahakama ya hakimu mkazi Geita, kwa pamoja wanashtakiwa kwa kosa la mauaji kifungu namba 196 ya sheria ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002.
Kesi hiyo inasikilizwa na Omary Kingwele, naibu msajili wa mahakama kuu aliyepewa mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Akisoma maelezo ya awali wakili wa Serikali mwandamizi, Hemed Halidi akishirikiana na Clemency Katto ameieleza mahakama hiyo kuwa Novemba 14, 2015 eneo la Ludete Katoro washtakiwa walimuua Mawazo kwa kukusudia.
Washtakiwa wote wamekana kutenda kosa hilo na kesi imeahirishwa hadi kikao kingine cha mahakama kuu.