Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kesi polisi wanaodaiwa kuomba rushwa Sh200 milioni kuanza kusikilizwa Aprili 6

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Aprili 6, 2020 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh200 milioni inayowakabili askari polisi wanne wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga Aprili 6, 2020 kuanza kusikiliza ushahidi katika kesi ya kuomba rushwa ya Sh200 milioni inayowakabili askari polisi wanne wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai.

Hatua hiyo inatokana na upelelezi wa kesi hiyo ya jinai, kukamilika na washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Kati ya polisi hao yupo mkaguzi msaidizi wa jeshi hilo, Shaban Shillah  ambaye ni mkuu wa upelelezi wa Kituo cha polisi Kawe.

Yeye na  wenzake wanakabiliwa na mashtaka tisa, likiwemo la kushawishi rushwa ya Sh200 milioni na kupokea Sh15 milioni.

Wakili kutoka Takukuru, Nickson Shayo  amewasomea maelezo ya awali leo Ijumaa Machi 6, 2020 mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi, Rashid Chaungu.

Washtakiwa baada ya kusomewa mashtaka yanayowakabili walikubali majina yao, vyeo vyao, kazi zao na siku waliyofikishwa mahakamani lakini  walikana mashtaka yanayowakabili.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Chaungu, ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 6, 2020 itakapoanza kusikilizwa ushahidi.

Mbali na Shillah, washtakiwa wengine  ni D 2910 sajenti Emmanuel Njegele,  WP 3246 Joyce Kitta  na F 3346 D/ Coplo Ulimwengu Rashid.

Kati ya mashtaka tisa yanayowakabili yapo ya kushawishi rushwa, kupokea rushwa,  kughushi nyaraka za uongo, kujihusisha na miamala ya rushwa na kutotii amri  halali ya ofisa wa Takukuru.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa, Desemba 17, 2018 eneo la Social Club Rainbow Kinondoni walishawishi rushwa ya Sh200 milioni kutoka kwa Diana Naivasha, wakidai amekamatwa na nyara za Serikali, ili asichukuliwe hatua za kisheria walimshawishi awapatie kiasi hicho jambo ambali ni kinyume.

Pia wanadaiwa kujihusisha na miamala ya rushwa, tukio wanalodaiwa kulitenda  Desemba 17, 2018 katika kituo cha Polisi Kawe jijini Dar es Salaam ambapo kwa pamoja waliomba rushwa ya Sh6 milioni kutoka kwa Diana kama kishawishi kumsaidia asichukuliwe hatua za kisheria baada ya kukamatwa na nyara za Serikali.

Katika kosa la nne, tano na sita ya kujihusisha na rushwa inadaiwa wanadaiwa kutenda Desemba 19, 23 mwaka 2018 na Januari 3, 2019.

Wanadaiwa wakiwa kituo cha Polisi Kawe na sehemu ya chakula, kama waajiriwa katika nafasi zao walipokea  Sh2 milioni kutoka kwa Diana kama kishawishi cha rushwa kwa madai anajihusika na nyara za Serikali.

Katika kosa la kughushi nyaraka linalomkabili Joyce, anadaiwa Desemba 2018 na Aprili 3, 2019 katika maeneo ya Kinondoni akiwa mwajiriwa wa polisi, alighushi nyaraka kwa lengo la kudanganya na kuonyesha kuwa ni ya kweli na imewekwa sahihi na Diana, wakati akijua kuwa sio kweli.

Katika shtaka la kutotii amri halali ya ofisa uchunguzi wa Takukuru, washtakiwa Shillah na Njegele wanadaiwa Aprili 2019 wakiwa Kinondoni, walishindwa kutii amri halali ya kukamatwa ambayo ilitolewa na mpelelezi wa Takukuru, Colman Lubisi.

Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa Kisutu, Oktoba 3, 2019, kujibu mashtaka yao.