Kesi ya kina Mbowe kuanza kesho kwa uamuzi

Muktasari:

Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi  inatarajiwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kesho Jumatatu Januari 10, 2022 baada ya kusimama kwa siku 20 kupisha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2022.

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi  inatarajiwa kuendelea na usikilizwaji wa kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu kesho Jumatatu Januari 10, 2022 baada ya kusimama kwa siku 20 kupisha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2022.

Katika mwendelezo huo wa usikilizwaji wa kesi hiyo kesho mahakama hiyo inatarajiwa kuanza kwa kutoa uamuzi wa pingamizi kuhusiana na upokeaji wa sare za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na za Jeshi la Kujennga Taifa (JKT).

Mbali na sare hizo pia kuna vifaa vingine vya Jeshi la Wananchi, pamoja na kidaftari kidogo ambacho kinadaiwa na upande wa mashaka kuwa kina taarifa zinazohusiana na mpango wa utekelezaji wa makosa vya vitendo vya wanayotuhumiwa.

Upande wa mashtaka unaiomba mahakama hiyo izipokee sare hizo na vifaa hivyo zinazodaiwa kukutwa na mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ya Uhujumu Uchumi, Halfani Bwire Hassan, ziwe kielelezo cha ushahidi wake.


Lakini jopo la mawakili wa utetezi linapinga upokewaji wa sare hizo na vifaa hivyo kuwa vielelezo vya ushahidi wa upande wa mashtaka pamoja na mambo mengine wakidai kuwa uwasilishwaji wake mahakamani hapo haukuzingatia matakwa ya kisheria, hivyo wanaiomba mahakama hiyo ikatae kuzipokea.

Pingamizi hilo liliibuliwa na upande wa utetezi Desemba 17, 2021 baada ya upande wa mashtaka kupitia kwa shahidi wake wa nane, Mkuu wa Upelelezi wa Polisi Wilaya (OC-CID) Arumeru, Mrakibu wa Polisi (SP), Jumanne Malangahe.

SP Malangahe aliiomba mahakama hiyo izipokee sare hizo kuwa sehemu ya ushahidi wake, na hivyo kuwa vielelezo vya upande wa mashtak, wakati akitoa ushahidi wake, akiongozwa na kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Robert Kidando.

Katika ushahidi wake, SP Malangahe aliieleza mahakama alimkuta Bwire na sare hizo na vifaa hivyo walipomfanyia upekuzi nyumbani kwake Yombo Kilakala, wilayani Temeke, Agosti 10, 2020, baada ya kumtia mbaroni kwa tuhuma hizo eneo la Changombe.

Baada ya maelezo hayo ndipo shahidi huyo alipoiomba mahakama hiyo izipokee sare hizo na vifaa hivyo viwe sehemu ya ushahidi wake, ombi ambalo lilipingwa vikali na mawakili wa utetezi na kuibua mvutano mkali wa hoja za kisheria.

Mvutano huo ulihitimishwa Desemba 20, 2021, baada ya mawakili wa pande zote kumaliza kuwasilisha hoja zao na Jaji Joachim Tiganga anayesikiliza kesi hiyo akaiahirisha hadi kesho kwa ajili ya kutoa uamuzi wa pingamizi hilo na kisha kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo.

Katika pingamizi lao, jopo la mawakili wa utetezi linaloongozwa na Wakili Peter Kibatala pamoja na mambo mengine walidai kuwa, shahidi huyo hakujenga msingi wa upokewaji wa vielelezo hivyo vinavyokusudiwa kwa kuwa hakueleza mnyororo wa utunzaji wake tangu zilizokamatwa, kuwa vilihifadhiwa wapi na nani alikuwa akivilinda.

Wanadia kuwa hilo ni takwa muhmu sana la kisheria linalopaswa kutimizwa kwanza. 

Pia wanadai kuwa ambapo shahidi huyo si shahidi anayestahili kwa kuwa hakuweza kuonesha kuwa na ufahamu ana au ujuzi wa utambuzi wa saree hizo kama kuwa ni za JWTZ.

Upande wa mashtaka ulidai kuwa hoja za pingamizi hilo hazina msingi na dhaifu na kwamba mawakili wa utetezi walishindwa kuelewa misingi ya kisheria ya uwasilishaji vielelezo mahakamani.

Walidai kuwa kwa kuwa, wakidai kuwa katika ushahidi wake wa msingi shahidi huyo alieleza mnyororo wa utunzaji wa vielelezo hivyo tangu vilipokamatwa na kwamba katika kuthibitisha hilo aliwasilisha mahakamani hati ya ukamataji mali ambayo imeorodhesha vitu vyote vilivyokamatwa na saini za mashuhda walioshuhudia upekeuzi.

Baada ya uamuzi huo, bila kujali matokeo yake kwamba mahakama itakubaliana na hoja za pingamizi la utetezi na hivyo kukataa kupokea vielelezo hivyo au kwamba itatulipilia mbali pingamizi hilo na hivyo kuvipokea, kasha itaendelea na usikilizwaji wa ushahidi kutoka kwa shahidi huyo wa nane.

Mbali na Mbowe (ambaye ni mshtakiwa wa nne) na Bwire (mshtakiwa wa kwenza) wengine katika kesi hiyo ni Adamu Hassan Kasekwa (wa pili) na Mohamed Abdillahi Ling’wenya (wa tatu).

Wote wanakabiliwa na jumla ya mashtaka sita, ya kula njama kutenda vitendo vya kigaidi, kushiriki na kufadhili vitendo vya kigaidi, kutaka kulipua vituo vya mafuta, kuhamaisha maandamano yasiyokoma kukata miti na kuiweka barabarani kuzuia barana na kutaka kumdhuru aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya.

Wanadaiwa kula njama za kutenda vitendo hivyo kwa nyakati na mahalitofautitofauti mwezi Agosti, 2020, katika mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaama na Morogoro na kwamba walipanga kutekeleza vitendo hivyo katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Kilimanjaro na Mbeya.