Kesi ya uhaini 1985: Oscar Ngaiza aeleza baba yake ni mtiifu-41

Sunday April 04 2021
uhaini pc
By William Shao

Jana tuliona namna shahidi wa 43 kwa upande wa mashtaka, Oscar Ngaiza ambaye ni mtoto wa mshtakiwa wa 13 katika kesi hiyo, Christopher Pastor Ngaiza alivyoanza kutoa ushahidi wake akielezea jinsi Pius Lugangira alivyoomba kutumia nyumba ya baba yake ya Masaki kwa mikutano ya biashara na wateja wake.

Akimalizia kutoa ushahidi wake, shahidi wa 43 wa upande wa mashtaka, Oscar aliiambia Mahakama kuwa baba yake alikuwa mwaminifu kwa Rais na Serikali na hakuwa na tamaa ya mambo makubwa ya kisiasa.

Akihojiwa na Wakili Hussein Muccadam, Oscar alisema kutokana na mazungumzo ya baba yake nyumbani, ilikuwa ni dhahiri anaridhika na kazi yake na alikuwa anaipenda.

Oscar alieleza kuwa, kuridhika kwa baba yake kulitokana na kuwa na kazi nzuri, gari nzuri na nyumba nzuri.

Alipoulizwa kazi ambayo baba yake alikuwa akifanya kabla ya kukamatwa, alisema alikuwa msaidizi wa Rais na Kamishna wa Mamlaka ya Uendeshaji wa Bonde la Mto Kagera.

Muccadam: Je, unamfahamu Lugangira?

Advertisement

Oscar: Ndiyo.

Muccadam: Unamfahamu kwa muda gani?

Oscar: Namfahamu tangu utoto wangu. Yeye ni ndugu yangu. Namwita kaka yangu.

Muccadam: Je, aliitwa Pius Lugangira?

Oscar: Hapana.

Muccadam: Uncle Tom au Father Tom?

Oscar: Sikuwahi kusikia akiitwa hivyo.

Muccadam: Lugangira alikuwa anafanya shughuli zake wapi?

Oscar: Nairobi na London.

Muccadam: Unajua anafanya shughuli gani?

Oscar: Nilijua ni mfanyabiashara.

Muccadam: Je, uliionaje hali yake ya kifedha?

Oscar: Niliiona ni nzuri kwa sababu alikuwa akisafiri sana na alikuwa anamudu kukaa katika hoteli kubwa.

Muccadam: Aliwahi kukaa nyumbani kwenu?

Oscar: Aliwahi kukaa nyumbani kwetu mwaka 1978 na baadaye akija akawa anafikia hoteli.

Muccadam: Uliona ajabu Lugangira kuja nyumbani kwenu?

Oscar: Haikuwa ajabu kuja nyumbani.

Muccadam: Uliiambia Mahakama kama Desemba 18, 1982 ulikwenda Bukoba. Baba yako alikuwa wapi?

Oscar: Baba na mama walikuwa Bukoba.

Muccadam: Ulirejea lini Dar es Salaam?

Oscar: Nilirejea Desemba 27, 1982 pamoja na mdogo wangu.

Muccadam: Lugangira alifanya mkutano lini nyumbani kwenu?

Oscar: Alifanya mkutano Desemba 30, 1982 wakati baba na mama wakiwa Bukoba.

Muccadam: Baba yako alimruhusu Lugangira kufanyia mkutano nyumbani?

Oscar: Hapana.

Muccadam: Nani aliyemruhusu?

Oscar: Mimi na Buberwa.

Muccadam: Lugangirwa alisema mkutano wake unahusu nini?

Oscar: Alisema anakutana na wakala wake wa biashara ili kufunga mwaka.

Muccadam: Wewe uliamini hivyo?

Oscar: Ndiyo. Niliamini kwa sababu huo ulikuwa ni mwisho wa mwaka.

Alisema hakuona mkutano uliofanyika Desemba 31, 1982 nyumbani kwao isipokuwa aliambiwa ulikuwapo na kuwa Januari 2, 1983 alirejea Chuo Kikuu alipokuwa akisoma na kubaki hadi Januari 9, 1983. Aliongeza kuwa Lugangira alikuja nyumbani kwao Januari 9, 1983 na baba yake na mama yake walikuwapo.

Alisema wakati polisi walipokuja nyumbani kwao Januari 10, 1983, yeye hakuwapo nyumbani.

Akijibu swali la Mzee wa Baraza, Anne Kirunda, iwapo mtu aliyemtambua kwenye gwaride la utambulisho kuwa ndiye aliyekuwa amekuja nyumbani kwao Desemba 31, 1983 kumsubiri Lugangira, ndiye huyo huyo aliyemtambua mahakamani juzi yake, Oscar alisema ndiye huyo huyo. Oscar alimtambua mshtakiwa wa sita, Kapteni Roderic Rousham Roberts.

Ushahidi wa Oscar ulifanana na ule wa Stephen Buberwa, ambaye ni mpwa wa Ngaiza, aliyeiambia Mahakama Kuu jinsi Pius Lugangira au Father Tom alivyoitumia nyumba ya Ngaiza kufanya mikutano wakati Ngaiza mwenyewe akiwa safarini Bukoba.

Lugangira alikuwa mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza, lakini alitoroka gerezani Juni 1983 na alikuwa bado hajapatikana wakati kesi hiyo ilipoanza upya.

Buberwa, aliyekuwa shahidi wa 36 wa upande wa mashtaka alidai kuwa, kwa vile alimfahamu Lugangira ambaye alikuwa binamu yake, hakuwa na wasiwasi naye na alimkubalia ombi lake la kufanya mkutano na wenzake kadhaa katika nyumba hiyo Desemba 29, 1982.

Baada ya Oscar kumaliza ushahidi wake kama shahidi wa 43, baadaye aliingia shahidi wa 44, Ramadhani Meli ambaye ni derava.

Meli aliiambia Mahakama Kuu kwamba alimpeleka mshtakiwa wa tatu, Luteni Eugene Maganga kwenye safari zake mbalimbali mjini Dar es Salaam, mojawapo ikiwa ni kupeleka sanduku la bia na mguu wa mbuzi nyumbani kwa Meja Jenerali Silasi Mayunga.

Meli ambaye ni shahidi wa 44 wa upande wa mashtaka, aliiambia Mahakama kwamba yeye ni dereva wa gari la kukodi la Kampuni ya Evergreen, na gari aliyokuwa anaendesha lilikodiwa na Pius Lugangira Desemba 1982 kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi.

Alisema mshtakiwa wa kwanza, Thomas Pius Mtakubwa Lugangira (Father Tom, Uncle Tom) ndiye alimwagiza kumpeleka Luteni Eugene Maganga (mshtakiwa wa pili) kwenye safari zake.

Alisema safari nyingi alizokuwa akimchukua Maganga zilikuwa ni kumrudisha Chuo Kikuu alikokuwa anasoma isipokuwa safari aliyompeleka Lugalo Jeshini kwenye bwalo na hatimaye Sinza na kumrejesha Motel Agip kupitia nyumbani kwa Mayunga na baadaye kumpeleka Chuo Kikuu.

Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Kulwa Massaba, shahidi huyo alisema alipompeleka Maganga kambini Lugalo Jeshini kwenye bwalo, mshtakiwa alinunua sanduku moja la bia na kulipakia kwenye gari wakaondoka kuelekea Sinza.

Alisema walipowasili Sinza walikwenda kwenye baa ya jirani ambayo haikumbuki jina na Maganga akanunua mguu wa mbuzi na kuupakia kwenye gari, kisha wakaondoka kuelekea mjini.

Alisema sanduku lile la bia na mguu wa mbuzi, Maganga alivipeleka kwenye nyumba aliyoishi Mzee Mayunga karibu na ubalozi wa Msumbiji.

Massaba: Ulijuaje kwamba mahali hapo Maganga alipoacha bia na mguu wa mbuzi ni nyumbani kwa Mzee Mayunga?

Meli: Maganga ndiye aliyeniambia kwamba hapo tulipoacha bia ni kwa Mayunga.

Massaba: Maganga alikuambia Mayunga anafanya kazi gani?

Meli: Aliniambia kuwa ni mwanajeshi.

Massaba: Alikutajia cheo chake?

Meli: Cheo alinitajia ila nimesahau.

Massaba: Baada ya kushusha bia mlikwenda wapi?

Meli: Tulirudi Motel Agip.

Massaba: Mlipofika Motel Agip mlifanya nini?

Meli: Lugangira aliniagiza nimpeleke Maganga Chuo Kikuu.


Itaendelea kesho.

Advertisement