Kesi yawagonganisha Polisi, Chadema

Wednesday August 04 2021
chademapic

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP) Simon Sirro akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tuhuma zinazomkabili mwenyekiti wa Chadema Freeman mbowe, jijini Dar es Salaam.Picha na Sunday George

By Waandishi Wetu

Dar/Mbeya. Wakati Chadema kikihamasisha wanachama wake kujitokeza siku ambayo kesi ya Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe itatajwa mahakamani Agosti 5, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Simon Sirro amewaonya watu watakaohamasisha mikusanyiko isiyo rasmi siku hiyo.

Julai 31, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika alitangaza hatua za chama hicho kupinga kesi hiyo ambayo Mbowe anatuhumiwa kuhusika na makosa yahusuyo ugaidi, ambapo pia aliwataka wanachama na wapenzi wa chama hicho kujitokeza kusikiliza kesi hiyo itakayosikilizwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari jana, IGP Sirro alisema, Jeshi la Polisi halitegemei mtu wala kikundi cha watu kwa namna yoyote kutoa shinikizo kwa mahakama ya kuachiwa huru Mbowe au kupewa dhamana.

“Kuhusu Mbowe na wenzake tuhuma dhidi yao kwa sasa ziko chini ya mamlaka ya Mahakama, suala la dhamana kwa kesi inayowakabili ni la kisheria nalo linasimamiwa na mahakama,” alisema Sirro.

“Jeshi la polisi linatoa onyo kali kwa mtu au kikundi cha watu kitakachojaribu kuhamasisha mikusanyiko isiyo rasmi au kuandamana au kwa namna yoyote kutoa shinikizo lolote,”alisema.

Sirro alisema Julai 17 hadi 22, Mbowe na wanachama wengine 15 walikamatwa mkoani Mwanza kwa kosa la kutoa matamshi yenye kuashiria uvunjifu wa amani, ikiwemo kuhamasisha wananchi kwa vitisho na sharti kuhusu Katiba mpya .

Advertisement

“Baada ya kukamatwa aliletwa Dar es Salaam ambapo kulikuwa na kesi nyingine inayopelelezwa dhidi yake kuhusiana na kula njama na kufadhili vitendo vya kigaidi; watuhumiwa wenzake sita walikuwa mahabusu na walishafikishwa mahakamani,”alisema.

Hata hivyo, Sirro alibainisha kuwa watuhumiwa wengine waliokamatwa jijini Mwanza pamoja mwenyekiti huyo, baada ya upelelezi kukamilika jalada la kesi litawasilishwa ofisi ya mashitaka kwa hatua za kisheria.

Chadema wajibu

Akijibu kauli za IGP Sirro jana, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema wanashangaa kuona jambo lililo mahakamani linajadiliwa kwenye vyombo vya habari.

Kuhusu watu kwenda kusikiliza kesi hiyo, Mrema alisema hawakubaliani na Jeshi la Polisi kuwakataza kwa kuwa mahakamani siyo kituo cha polisi.

Hali ya usalama nchini

Kwa upande mwingine, IGP Sirro alizungumzia hali ya usalama nchini akisema, jeshi hilo lilifanya operesheni Mei na Juni baada ya kuwepo kwa viashiria vya uhallifu na kufanikiwa kukamata watuhumiwa 5,429 waliohusika na makosa makubwa ya jinai.

“Operesheni hii ilihusisha wale wa unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa magari, mauaji, kubaka na dawa za kulevya ambapo tulifanikiwa kupata silaha 37 za aina mbalimbali, dawa za kulevya aina ya heroine kilo 540, lita 13612 za gongo pamoja na mitambo 94 yake, alisema.

Advertisement